WENZA WA VIONGOZI WAWASHIKA MKONO WAATHIRIKA WA MAFURIKO HANANG.
Umoja wa Wenza wa viongozi “New Millenium Women Group” wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyokabiliana mafuriko yaliyosabisha maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang, Mkoani Manyara.
Akizungumza na waathirika katika kambi iliyopo shule ya sekondari Katesh, Wilayani Hanang Mkoani Manyara kwa Mlezi wa Umoja huo ambaye ni mke wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mama Mary Majaliwa amesema kitendo cha Rais Dkt. Samia kuacha majukumu yake tena akiwa nje ya nchi na kurejea kwenda kuwapa pole waathika, ni kitendo cha upendo mkubwa alionao kwa Watanzania.
Mama Majaliwa amesema hayo jana (Disemba 18, 2023) wakati akizungumza na Waathirika wa maafa hayo kwa niaba ya wenza wengine wa viongozi. Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu 89 na wengine zaidi ya 600 kukosa makazi katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara.
“Tumeguswa sana na madhila yaliyowapata na tumekuja kuwapa pole lakini pia tumekuja kuungana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na tunamshukuru kwa namna alivyoweza kukabiliana na matokeo ya janga hili na kuhakikisha waathirika wote wanapata huduma kwa haraka kwa kuleta Serikali yake hapa na tunashukuru kuona Hanang imetulia, na shughuli zinaendelea kuimarika.”
