ZAIDI ya shilingi bilioni 3.7 zimechangwa ikiwa ni fedha taslimu na ahadi katika hafla ya kuzichangia timu za Taifa za Tanzania ambapo kati ya hizo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amechangia shilingi milioni 500.
..................................................................
Fedha hizo zilipatikana zilipatikana kutokana na wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwa ni ppamoja na wizara na taasisi za Serikali, taasisi za kifedha, mashirika ya hifadhi za jamii, wafanyabiashara na wasanii pamoja na njia ya mnada ambapo jezi zenye majina ya wachezaji wa timu ya Taifa iliyoshiriki AFCON miaka ya 1980 ziliuzwa na jezi iliyouzwa na gharama kuwa ilikuwa ya golikipa Juma Pondamali iliyonunuliwa kwa shilingi milioni 25.
Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia ametoa mchango huo jana usiku Jumatano, Januari 10, 2024 wakati
alipompigia simu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa ajili ya kuzungumza na wadau
mbalimbali wa michezo walijitokeza katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kuzichangia timu za Taifa.
“Wito wangu na
ombi langu kwenu Watanzania wenzangu tuchangie timu zetu ili ziende kuwakilisha
vizuri jina la Tanzania. Serikali imejitahidi na imehamasisha na timu zetu
zinasonga mbele, michezo ni gharama ndugu zangu. Mimi na marafiki zangu kwa
kuanzia tutachangia shilingi milioni 500.”
Waziri Mkuu ambaye
aliongoza harambee hiyo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alisema lengo
la kukusanya fedha hizo ni kuziwezesha timu za Taifa zinazoshiriki katika
michuano mbalimbali ya kimataifa kusonga mbele. “Serikali ya awamu ya sita
chini ya uongozi thabiti wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeshuhudia mageuzi makubwa sana katika
sekta ya michezo.”
Waziri Mkuu
alisema mageuzi hayo yametokana na jitihada na uwekezaji mkubwa unaofanywa na
Serikali pamoja na wadau mbalimbali yakiwemo makampuni pamoja na watu binafsi,
ambapo utashi mkubwa wa kisiasa katika sekta ya michezo umeleta msukumo chanya
unaoongeza ari na morali kwa wadau wa sekta ya kuunga mkono na kuzienzi
jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uwekezaji na mabadiliko
makubwa katika sekta ya michezo.
Alisema kwa upande wa
mpira wa miguu, Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanaume “Taifa Stars”
imefuzu kucheza mashindano ya AFCON yanayofanyika nchini Ivory Coast mwezi huu
Januari 2024. “Ninayo furaha kuwataarifu kuwa hivi sasa timu yetu ipo kambini
nchini Misri na tayari Mheshimiwa Rais amekwisha kutoa fedha za kusaidia Timu
ya Taifa kushiriki mashindano haya.”
Vilevile, Waziri
Mkuu alisema timu ya Taifa ya wanawake ya Mpira wa miguu “Twiga Stars” imefuzu
kucheza mashindano ya WAFCON ambayo yatafanyika mwaka huu nchini Morocco, timu
hiyo nayo imepewa bonasi ya Mheshimiwa Rais ya shilingi milioni 200 ilipofuzu
mashindano hayo.
Awali, Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya
kuchangia timu za Taifa, Bw. Theobaid Sabi alisema kamati yao ina majukumu
makuu matatu ambapo la kwanza ni kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia timu za
Taifa zinazotarajia kushiriki mashindano ya kimataifa, kuuelimisha umma kuhusu
uwepo na umuhimu wa timu za Taifa na kuuhamasisha kuziunga mkono na kuzichangia
timu hizo.
Bw. Sabi ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC alisema lengo ni kukusanya shilingi bilioni
10, hivyo amewaomba wadau wajitokeze kwa hali na mali kuchangia timu hizo.
Alisema Benki ya NBC itaanza kuchangia shilingi milioni 100.
(mwisho)
