CHUO KIKUU CHA DODOMA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA CHUO KIKUU CHA UUGUZI RUTGERS CHA NCHINI MAREKANI
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof.
Lughano Kusiluka, leo amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka
Chuo Kikuu cha uuguzi Rutgers cha nchini Marekani, ambao ni wadau muhimu
wa maendeleo wa chuo hicho kupitia Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii.
Akikaribisha ujumbe huo, Prof. Kusiluka ameelezea shukrani zake kwa ushirikiano
na ufadhili unaotolewa na Chuo Kikuu cha Rutgers kwa Shule Kuu ya Uuguzi
na Afya ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Dodoma, amesisisitiza matarajio makubwa
ya UDOM katika kuendeleza kuanzisha miradi mingi zaidi ya kujifunza na
ufundishaji, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kozi mpya za uuguzi na Afya ya
Jamii. "
Kwa kuzingatia ongezeko la matumizi ya teknolojia nchini na uwekezaji mkubwa ulioufanya katika miundombinu ya TEHAMA, sioni sababu ya kutokufundisha baadhi ya programu kwa njia ya masafa kwa kushirikiana na wataalamu wenzetu waliopo Rutgers" alisema Prof. Kusiluka.
Aidha, aliwataka viongozi wa Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii, kutumia
fursa
zilizopo katika kuanzisha kozi ambazo zitakuwa na manufaa kwa taifa na
zinazoweza kufundishwa kupitia mtandao.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Rutgers, Dkt. Emilia
Iwk, alieleza kuwa kupitia ushirikiano uliopo kati ya vyuo hivyo viwili,
wamepanga kuongeza maeneo ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo
ya muda mfupi kwa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dodoma ili kuongeza ujuzi na
kupanua wigo wa
mafunzo kwa wanachuo.
Kwa sasa, Chuo Kikuu cha Dodoma kina
ushirikiano na Chuo Kikuu cha Rutgers katika maeneo ya uandishi wa miradi
ya pamoja ya utafiti, ufundishaji, ubunifu, na kubuni mitaala mipya ya
masomo.
Ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Rutgers uliongozwa na Dkt. Emilia Iwk, akifuatana
na viongozi wengine Dkt. Antony Fillipelli na Bi. Catie Filippeli Apn,
pamoja na wanafunzi 12 wanaosoma katika chuo hicho ambao wamekuja
kujifunza na kubadilishana uzoefu na wanafunzi wenzao katika Shule Kuu ya
Uuguzi na Tiba ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mkuu wa Idara ya “Clinical Nursing”
ya Chuo Kikuu cha Dodoma Bi. Angelina Alphonce Joho, ameeleza ujumbe huo
utakuwepo nchini kwa majuma kadhaa, ambapo mbali na kufundisha, pia
wamepanga kufanya tathmini ya maeneo ya ushirikiano pamoja na kuainisha
maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo kuangalia uwezekano wa kupata vifaa tiba
vya kisasa kwa ajili ya kufundishia pamoja na fursa za mafunzo wa wakufunzi
ili kuendelea kuwajengea uwezo.



