Kovu langu, alama yangu
Kupitia taasisi yake, Seitebogo amesaidia kurudisha tabasamu za watu wengine wenye kuishi na hali hiyo. Picha: SeitebogoTaasisi ya Seitebogo Peta inajikita katika kusaidia watoto waliozaliwa na mdomo sungura. Picha: Seitebogo
Na
Pauline Odhiambo
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Tasisi iliyoanzishwa na binti mdogo aliyezaliwa na ‘mdomo
sungura’ yapania kuondoa unyanyapaa kwa watu wenye hali hiyo huku ikiazimia
kuonesha umuhimu wa kuchangia matibabu yake.
Sehemu ya alama iliyosalia kwenye sehemu ya juu ya kinywa
chake, sio aibu kwa Seitebogo Peta.
Kimsingi, anajisikia fahari sana kubaki na alama hiyo
mwilini wake.
Ingawa upasuaji wa mwisho kwenye kinywa chake ungeweza
kuondoa kumbukumbu za mateso aliyopitia utotoni, Seitebogo anaona bora kuwa na
tabasumu lake lenye kubeba kasoro, kile anachoelezea kuwa ni ‘sehemu muhimu ya
maisha yake.’ Akiwa amezaliwa na ‘mdomo sungura,’ hali ya kuwa na uwazi ama
nafasi katika mdomo wa juu jirani na pua, Seitebogo amekwishafanyiwa upasuaji
kadhaa kurejesha tabasamu usoni mwake.
Ilimlazimu binti huyo mwenye umri wa miaka 32 kupambana
na namna jamii na dunia kwa ujumla invyowachukulia watu wenye midomo sungura.
Hilo bado halikumrudisha nyuma Seitebogo katika harakati
za kuwapambania wenzake. Kupitia Taasisi ya Seitebogo Peta, aliyoianzisha mwaka
2017, binti huyo amejitahidi kurejesha tabasamu nyingi kwa watu wenye hali kama
aliyokuwa nayo.
“Niliangazia makundi yote mara tu baada ya kuanzisha
taasisi hii,” anasema Seitebogo katika mahojiano maalumu na TRT Afrika.
“Nilionekana kuguswa zaidi na watoto, mara baada ya kushika mimba.”
Seitebogo anakiri wazi kuwa huenda binti yake angerithi
hali hiyo kutokana na sababu za kijenetiki, sababu kuu inayotajwa pia na
Shirika la Afya Duniani (WHO).
"Baada ya binti yangu kuzaliwa mwaka 2019, kitu cha
kwanza kuangalia ilikuwa ni kinywa chake,” anaelezea. "Nilifarijika sana
kuona kuwa hakuwa na hali hiyo ingawa nilijaribu kuvaa viatu vya wazazi wenye
watoto wenye midomo sungura.”
Uhusiano
wa kimafamilia
Kwa mujibu wa WHO, hakuna mahusiano ya moja kwa moja ya
jenetiki yanayosababisha hali hii. Hata hivyo, WHO inadai kuwa kuna wakati yapo
na wakati mwengine hakuna.
Kati ya sababu za kimazingira, kwa mujibu wa Shirika
hilo, ni kwa kina mama wajawazito kutumia dawa maalumu, kabla ya kujifungua,
uvutaji wa sigara, unywaji pombe na mkao wa mtoto ndani ya tumbo la uzazi.
Hata hivyo, kwa mshangao wa wengi, kuna uwezekano kwa
watoto walipangiliwa, na kuzaliwa wakiwa na siha njema kupata ‘midomo ya
sungura’.
“Baadhi ya watu hapa Afrika ya Kusini, wanahusisha hali
hiyo na ushirikina au adhabu ya Mungu kutokana na makosa ya wazazi,” anaelezea
Seitebogo.
“Baadhi ya watu hapa Afrika ya Kusini, wanahusisha hali
hiyo na ushirikina au adhabu ya Mungu kutokana na makosa ya wazazi,” anaelezea
Seitebogo.
Makovu yenye hisia
Kulingana na wataalamu wa afya, mtoto mchanga anaweza
kuzaliwa na mpasuko kwenye mdomo wa juu na kuathiri upande mmoja wa uso ama
pande zote.
Lakini kwa hali kama iliyomtokea Seitebogo, yote
yanawezekana.
Kufuatia hali hiyo, ilimlazimu binti huyo kufanyiwa
upasuaji kadhaa kurekebisha sura yake ya utotoni.
Dhihaka
Shuleni
Kwa hakika, ilimuwia vigumu Seitibogo kuishi na ‘mdomo
sungura,’ hasa akiwa shuleni kutokana na dhihaka alizopata kutoka kwa wanafunzi
wenzake.
"Nilikuwa ni mwanafunzi mwenye kujiamini sana,
nakumbuka nikiwa shule ya msingi, nilipishana hoja na mwanafunzi mmoja
aliyejaribu kunifananisha na mbwa kwenye moja ya vipindi vya televisheni,”
anaeleza.
Dhihaka na utani wa mara kwa mara shuleni ulimuondolea
hofu Seitebogo, na kimsingi kumfanya kudiriki kuitetea hali yake, kwa namna
yoyote ile.
"Baada ya binti yangu kuzaliwa, nilianza kuhofia
namna atakavyoishi na kupambana na utani na dhihaka,” anaeleza.
Mzigo mkubwa
Pamoja na unyanyapaa aliokumbana nao, Seitebogo safari za
mara kwa mara hospitali, zilikuwa ni sehemu ya maisha ya binti huyo.
“Inamlazimu binadamu yoyote aliyezaliwa na mdomo sungura
kuwa karibu na wataalamu wa afya kwa wakati wote,” anasema. "Mara uko na
mtaalamu huyu mara yule, hakika ni pilipapilika yenye kuchosha."
Hata hivyo, bado Seitebogo anajiona mwenye bahati sana
kwani wazazi wake waliweza kugharamia matibabu yake.
"Ni ngumu sana kwa raia wengi wa hapa Afrika ya
Kusini kugharimia matibabu hayo," anasema. Changamoto hiyo ilimsukuma
Seitebogo kuongeza wigo wa shughuli za taasisi ikiwemo kusaidia familia zenye
kipato cha chini kupata huduma za afya wanazohitaji zaidi.
"Mara nyingi, najihusisha na wazazi waliokata tamaa
na matibabu ya midomo sungura kwa watoto wao," Seitebogo anasema. “Baadhi,
wamediriki hata kuwatelekeza watoto waishio na hali hiyo kutokana changamoto za
kifedha.”
Seitobogo amepitia upasuaji mara kadhaa akiwa mtoto katika hali ya kutafuta tabasamu lililokamilika. Picha: Seitebogo
Tabasamu linalovutia
Hadi sasa, Seitebogo, kupitia taasisi yake ameweza
kuwafikia zaidi ya watu 50 kupata huduma za urekebishwaji, wengi wakiwa ni
watoto. "Baadhi wamekuwa wakitokea sehemu za mbali, kama vile Eastern
Cape, Kwazulu Natal na Northwest. Pia niliweza kumsaidia mwanamke mwenye miaka
25, na nilifarijika kuona akirejea kwenye hali yake ya kawaida,” anasema.
"Kitu muhimu kwangu, ni kurejesha tabasamu kwa
wagonjwa waliokwisha kata tamaa.”
Ni matumaini ya kupanua wigo wa shughuli za taasisi yake, kujumuisha pia urekebishwaji wa sura kwa makundi yote, na kutoa huduma za afya zifaazo, wakati wote.



