Umoja wa Afrika yazitaka Ethiopia na Somalia kupunguza mvutano
Mwenyekiti ya tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameoambia Ethiopi na Somalia waache mvutano / Photo: Reuters.................................................................................
Mwenyekiti ya Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat
anatoa wito wa utulivu na kuheshimiana ili kupunguza mvutano unaoendelea kati
ya Serikali za Ethiopia na Somalia.
Somalia imekataa makubaliano baina ya Ethiopia na eneo
lake lililojitenga la Somaliland kuiruhusu kutumia bandari kubwa yenye ufikiaji
wa Bahari Nyekundu, ikisema makubaliano hayo hayana nguvu za kisheria.
Iwapo makubaliano hayo
yatafanya kazi, yatairuhusu Ethiopia,
kukodisha kilomita 20 kuzunguka bandari ya Berbera, ambayo iko kwenye Ghuba ya
Aden na ufikiaji wa Bahari Nyekundu, kwa miaka 50 kwa jeshi lake la majini na
malengo ya kibiashara.
Somalia, ambayo inaiona Somaliland kama sehemu ya ardhi
yake, pia ilimuita balozi wake nchini Ethiopia kwa ajili ya kujadiliana kuhusu
makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na
kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi siku ya Jumatatu.
Umoja wa Afrika unaitambua Somalia na sio Somaliland kama
mwanachama wake.
Mwenyekiti wa Tume ya AU, Faki anasema amekuwa
akifuatilia kwa karibu mvutano uliotokana na kusainiwa kwa mkataba kati ya
Ethiopia na Somaliland.
Katika taarifa yake, "Anazitaka nchi hizo mbili
kujiepusha na kitendo chochote ambacho bila kukusudia kinaweza kusababisha
kuzorota kwa uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili jirani za Afrika
Mashariki."
Kwa upande wake, kiongozi wa Somaliland alisema Ethiopia
inaitambua Somaliland kama taifa huru, na kuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo.
Hata hivyo, Somalia ilitaja makubaliano hayo kama
"uchokozi" na kuapa kutetea eneo lake.
Faki ameongezea kuwa "Anasisitiza umuhimu wa
kuheshimu umoja, uadilifu wa eneo na mamlaka kamili ya nchi zote wanachama wa
Umoja wa Afrika mkiwemo Ethiopia na Somalia."
Ameomba nchi hizo mbili kuzingatia kanuni za ujirani
mwema ili kukuza na kuimarisha amani, usalama na utulivu katika eneo la Pembe
ya Afrika.
Wakati huo huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya
Marekani Matthew Miller amesema, "Marekani inatambua uhuru na uadilifu wa
eneo la Somalia ndani ya mipaka yake ya 1960."
