...........................................................
Ni majira ya jioni, Dina Simbangui, mama wa watoto
watatu akiendelea na maandalizi ya chakula cha jioni. Moshi unafuka jikoni,
huku akiendelea kuukoleza kwa kutumia mikono yake ambayo haina vidole. Ni
athari zitokanazo na ugonjwa wa ukoma, baada ya kuuguwa kwa miongo kadhaa.
Dina, ni sehemu ya wakazi 62 wa kitongoji cha Samaria kilichopo Mkoani Dodoma nchini Tanzania.
Ni ugonjwa ambao, uliambatana na unyanyapaa kwa kiasi
kikubwa, huku wengi wakiuhusisha na ushirikina. Wataalamu wa afya wanakiri
kwamba, hii yote ilichangiwa na uelewa mdogo miongoni mwa jamii.
Hivi sasa, matumizi ya kijiji hicho yamebadilishwa,
na kufanywa makazi ya kudumu kwa waliosalia kuwa waathirika wa ugonjwa huo.
Hiki ndicho chanzo cha Dina Simbangui na mume wake
Saimon Mkoi kujikuta kijijini hapo. Wameishi miaka mingi lakini simulizi zao
zinatofautiana.
Saimon Mkoi, yeye alizaliwa mwaka 1942 wilayani
Kilosa Mkoani Morogoro, lakini maisha yake yalibadilika mwaka 1962 baada ya
kuugua ukoma.
Anakumbuka enzi za ujana wake kabla ya kuumwa, alipokuwa
mkulima wa mazao mbalimbali kama vile mahindi na maharagwe.
“Mimi nilikuwa kijana safi kabisa, lakini
nilipokaribia miaka 30 ndipo nilipoanza kuumwa. Nilikuwa Kilosa na nilikuwa
mkulima lakini sasa nashindwa kulima na mikono haina kazi,” anasimulia.
Katika kusaka matibabu, alifika katika hospitali
kadhaa ikiwemo Turiani, Sukamahela na ifakara, zote zipo mkoani Morogoro.
Harakati hizi hazikuzaa matunda. Kwa sababu mfa maji haishi kutapatapa,
hatimae, alijikuta katika kijiji cha Samaria.
“Kote nilitembea kwa sababu ya kupata matibabu,
lakini nilipofika Hospitali ya kilosa sikuwa na habari kama naumwa ukoma,
lakini nilieleweshwa kwamba tayari nilikuwa na ukoma,” amesma.
Nae Simbangui, mke wa Mkoi, yeye alizaliwa Wilayani
Mpwapwa Mkoani Dodoma na tangu alipofika kijijini hapo, anasema, katu
hajatembelewa na ndugu zake, walioamua kumtenga kabisa.
“Wataalamu walipogundua kuwa naumwa, na sina msaada
wowote kutoka kwa ndugu, ndipo nilipoamua kuja kukaa hapa kwa ajili ya kupata
matibabu ya karibu. Na huo ndio ulikuwa mwanzo wa mimi kuishi hapa. Mpaka sasa,
hakuna ndugu aliye kunitembelea” anasimulia.
Mbali na wahisani kuwajengea makazi ya kudumu, lakini
baadhi wameiambia TRT Afrika kwamba kwa sasa wanachokosa ni huduma za matibabu
ya bure, pamoja na mahitaji muhimu kama vile chakula na malazi.
“Ukienda Hospitali unakaribishwa vizuri lakini
wakishakutibu wanakudai malipo, wanasema hii Hospitali haipo kwa ajili yetu
pekee. Sisi ni walemavu tunaotegemea Serikali, lakini nayo imetutupa,” anasema.
Ingawa hivi sasa wamepona ugonjwa wa ukoma lakini
athari za ugonjwa huo bado zipo mwilini. Mara kwa mara wanapatwa na magonjwa
nyemelezi kama kutokwa na vidonda.
Kwa upande wake, Mary Manyono ambaye ni muangalizi
Mkuu wa wazee hao, alikiri kuwepo kwa chagamoto.
"Njaa ipo na wanahangaika sana, hakuna vyoo,
hakuna umeme, wala mashine za kusaga na kwenda kijijini kusaga ni mbali?
anasema Mary.
Serikali imesema kiwango cha ukoma kimeshuka kutoka
wagonjwa 2,297 mwaka 2015 hadi wagonjwa 1,309 mwaka 2023 sawa na punguzo la
57%.
Takwimu zinaonesha hadi kufikia mwaka 2023, Tanzania
ilikuwa na wagonjwa 3 kwa kila watu 100,000 hivyo kufikia kiwango cha awali cha
Shirika la Afya Duniani (WHO) kutokomeza ukoma.
Hata hivyo, Serikali imetoa wito kwa halmashauri 19
katika mikoa tisa ya nchi humo ukiwemo Dodoma, kuwaibua wagonjwa wa ukoma,kufuatilia
mwenendo wa ugonjwa, na kuweka takwimu sahihi. Dodoma ni miongoni mwa mikoa
ambayo haijafikia viwango vya kutokomeza ugonjwa huo.
“Bado kuna halmashauri 19 katika mikoa ya Morogoro,
Lindi, Dar es Salaam, Mtwara, Kigoma, Tanga, Dodoma, Geita, na Pwani ambayo
haijafikia viwango vya utokomezaji,” ilisema taarifa hiyo.
Pamoja na kutoweka kwa ukoma, imekuwa ni utamaduni wa
kila mwaka kuadhimisha siku ya Ukoma duniani, lengo ikiwa ni kufanya tathmini
na kuangalia baadhi ya changamoto zilizopo.



