Waziri wa Kilimo nchini
Tanzania amesema serikali imechukua hatua kadhaa kuhakikisha uhaba wa tatizo la
uhaba wa sukari nchini linaondoka. Waziri Bashe amesema, miongoni mwa hatua
hizo, ni pamoja na kutoa vibali vya kuruhusu uingizaji wa sukari takriban tani
laki moja kutoka nje.
Kauli hii ya serikali, inakuja baada ya bidhaa hiyo
muhimu kupanda bei kutoka shilingi elfu mbili hadi elfu nne na katika baadhi ya
maeneo kuadimika kabisa. Hali ambayo imeibuwa wasiwasi kwa wananchi kutokana na
umuhimu wa bidhaa hiyo ambayo mahitaji yake kwa siku ni takriban lakini 1500
kwa siku.
"Hatua ya kwanza tuliyochukua kama serikali,
ni kuruhusu uagizaji wa sukari wastani wa tani laki moja ambao tumewapa viwanda
ili waweze kuingiza hiyo sukari, maamuzi ya kuwapa viwanda sio ya bahati mbaya,
kama mnavyofahamu, ni lazima tulinde viwanda vyetu vya ndani, na hatulindi kwa
gharama ya mlaji, bei ya sukari kabla ya tatizo hili, viwandani ilikuwa bei
2240 mpaka 2270 na bei ya reja reja ilikuwa inatembea kati ya 2700 mpaka 3000,
leo imepanda baadhi ya maeneo mpaka kufika 4000. serikali tumewaagiza viwanda
kusimamia kuhakikisha kwamba wanasimamia usambazaji wao kama kawaida bila
kumuumiza mlaji. Lakini hatua ya pili tuliyochukua kama serikali, tumetoa
idhini ya uagizaji wa sukari zaidi ya tani laki moja, tunaamini hii ikiingia
katika mfumo wetu wa ugavi, hali ya usambazaji wa sukari itakuwa katika hali
nzuri," amesema Bashe.
Tanzania ina jumla ya viwanda saba vya sukari,
ambapo kwa mujibu wa serikali, kutokana na mvua kubwa zinazoendelea katika
maeneo mbalimbali nchini humo, uzalishaji umepungua kwa takriban tani elfu moja
kwa siku.
Waziri huo amefafanua kuwa, katika kipindi cha
mvua, mbali na uvunaji na uchakataji wa sukari unavyokuwa mgumu, lakini kiwango
pia cha sukari katika miwa kinapungua kwa zaidi ya asilimia 25.
