Mvua iliyonyesha kwa zaidi ya saa kumi, imeleta uharibifu wa mali, miundombinu pamoja na baadhi kupoteza maisha. Picha/TRT Afrika
Watu kadhaa wanaripotiwa kupoteza maisha jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania baada ya mvua kubwa kunyesha nchini humo kwa zaidi ya saa kumi. Hayo ni kwa mujibu wa mwandishi Wetu
Maeneo yanayoripotiwa kuathirika zaidi ni katika viunga
vya mji huo kama vile Mbezi, Tegeta, ambapo nyumba kadhaa zimefunikwa na maji,
huku baadhi ya vitu kama magari, matawi ya miti pamoja ambapo mali kadhaa zikisombwa
na mafuriko.
Mvua hizo pia, zinaripotiwa kuharibu miundombinu muhimu
ya barabara ikiwemo kuvunja Daraja la Mtongani ambalo ndilo kiunganishi kikubwa
cha mji wa Dar es Salaam mji wa kihistoria wa Bagamoyo uliopo Mkoa wa Pwani.
Baadhi ya wakazi wa mji huo wa
kibiashara, ambao unaongoza kuwa na idadi kubwa ya wakazi zaidi ya milioni tano,
wanakiri kwamba shughuli zao za kila siku zimekwama kutokana na uharibifu wa
mali uliosababishwa na mvua hizo.
Maafa hayo yanatokea ikiwa imepita mwezi mmoja na wiki kadhaa tangu kutokea maporomoko ya udongo huko katika Wilaya ya Hanang, Kaskazini mwa Tanzania ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 80, huku mamia wakiachwa bila makazi.
Awali, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini humo ilitoa tahadhari
ya kuwepo kwa mvua kubwa, maarufu El Nino na kutaka watu hasa wale wanaoishi
karibu na mabonde kuchukua tahadhari. Wataalamu wametabiri eneo la Afrika
Mashariki kukumbwa na mvua hizi, ambazo kwa kawaida huwa ni nyingi kupitiliza
na huleta madhara kwa wananchi kutokana na mafuriko, pamoja na maporomoko.

