WANAWAKE WATAKIWA KWENDA KUGOMBEA MAJIMBONI
Na Selemani Msuya
JUKWAA la Wanawake Viongozi wa Jumuiya za Vyama vya Siasa
nchini (ULINGO), limeshauri wanawake waliopata nafasi ya viti maalum zaidi ya
mara moja, kuelekeza nguvu kwenye majimbo na kuachia vizazi vipya.
Aidha, vyama vya siasa nchini vimetakiwa kuweka kifungu
kwenye Katiba zao kinacholazimisha uwakilishi wa watu wenye ulemavu na sio
kuteuliwa kwa hisani.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Ulingo, Mama Anna
Abdallah wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo
jukwaa hilo lilikutana kwa siku moja kujadili miswaada ya sheria mitatu
iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, 2023.
Miswaada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani wa Mwaka 2023, Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Sheria ya
Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023.
Mama Anna alisema iwapo mwanasiasa mwanamke amepata nafasi ya
kuwa mbunge wa viti maalum kwa awamu zaidi ya moja ni vema kuachia vijana wapya
na yeye kushiriki kwenye majimbo, hali ambayo itawezesha jamii hasa vijana wa
kike kutamani kushiriki siasa.
“Sisi tunaamini kugombea ni haki ya kila Mtanzania ambaye ana
sifa za kugombea, na hivi viti maalum vilianzishwa ili kuwapa ujasiri wanawake
katika siasa, hilo limefanikiwa sasa tuna asilimia 30 ya wabunge wa viti
maalum, hivyo wanawake tuelekeze nguvu kwenye majimbo tukashindane na wanaume,”
alisema.
Alisema Ulingo inatamani kuona wanawake wengi wanagombea
kuanzia uenyekiti wa kitongoji, kijiji, mtaam, udiwani, ubunge na urais kwani
ushahidi umeonesha kuwa wanaweza.
Mwenyekiti huyo alisema Rais Samia Suluhu Hassan ni ushahidi
tosha kuwa wanawake wanaweza, hivyo ni jukumu la kila mmoja wapo kumsapoti
mwanamke anaingia kwenye siasa.
“Sisi tunakauli yetu kuwa rafiki wa mwanamke ni mwanamke na
jirani wa mwanaume ni mwanaume, tukienda na nguvu hii 2024 na 2025 tutafanya
viziru sana, tupendane. Lakini tunaamini miaka 10 ya viti maalum inatosha,
kwani hata upatikanaji wake kwa upande mwingine unatuzalilisha,” alisema.
Aidha, Mama Anna aliwaomba wapiga kura kutowachagua wabunge
wa majimbo na viti maalum ambao hawatekelezi majukumu yao kwani ni kikwazo cha
maendeleo.
Makamu Mwenyekiti wa Ulingo, Suzan Lyimo alisema suala la
viti maalumu anaungana na wote wanaotaka ushiriki wa misimu miwili, ili kuwapa
nafasi watu wapya.
“Nafasi ya viti maalum ni utaratibu wa kila nchi, ili kuwa na
usawa, ila tunataka kuona mabadiliko baada ya kupata nafasi, lakini pia Katiba
inatakiwa kusema wazi ni yapi majukumu ya mbunge wa viti maalum na hapa ndipo
ajenda ya Katiba Mpya inaibuka,” alisema
Alisema wao kama wawakilishi wa wanawake nchini Tanzania
wanasisitiza suala la jinsia katika nafasi mbalimbali ili dhana ya usawa iweze
kutekelezeka.
Lyimo alisema pamoja na kupendekeza sheria hizo kuangalia
eneo hilo la jinsia ni vema na Katiba za vyama vya siasa kuakisi ambacho wao
wanakipigania kwenye Katiba mama.
“Sisi Ulingo tunajipanga kutoa hamasa kwa wanawake viongozi
kuhamasisha wanawake wenzetu, ili washiriki uchaguzi kuanzia serikali za mitaa
kwa wingi, kwa sababu tunaamini mwanamke akiongozi, anaongoza kama mama ndani
ya familia, kwani anajua uchungu wa mtoto,” alisema.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema siasa ni kila kitu, hivyo
amewashauri wanaume kuondokana na dhana ya kuwa wanawake ni watu wa jikoni na
hawawezi.
“Tuna Rais Samia mwanamke, Spika Dk Tulia Ackson mwanamke na
tunaona wanafanya vizuri, hivyo tuwaunge mkono kwa sisi kushiriki chaguzi zote
na tukipata nafasi ya kutoa maoni tutoe,” alisema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Ulingo, Zanzibar Mgeni
Hassan Juma alisema jukwaa hilo ni muhimu kwao kama wanasiasa wanawake kukutana
na kuzungumza mambo yote ambayo yanawahusu.
Mgeni ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Wawakilishi
alisema wao kama wanawake wanataka tafsiri ya Katiba inayosema haki sawa kwa
wote iweze kuonekana katika utekelezaji na sio kuwepo kwenye maandishi pekee.
“Tumejipanga kuwasilisha maoni yetu bungeni, juu ya miswaada
hiyo ambayo imewasilishwa bungeni, mfano inahitajika kuwepo uwiano wa asilimia
fulani kuanzia ngazi ya chama na kwenye vyombo,” alisema.
Naibu Spika alisema uongozi wa Rais Samia umeonesha dunia
kuwa wanawake wanaweza, hivyo ni dhahiri kwamba wakipewa nafasi katika uongozi
wanaweza kusaidia nchi zao.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wanawake wenye Ulemavu Tanzania
(SWAUTA), Stella Jailos alisema pamoja na mvutano wa uwepo wa viti maalum, bado
kundi la watu wenye ulemavu halijapewa nguvu ya kisheria.
“Sisi watu wenye ulemavu hasa wanawake tunaomba vyama viweke
vifungu kwenye Katiba zao ambavyo vitaelekeza kuwa ni lazima ikitokea viti
maalum watu wenye ulemavu wawepo na sio hisani,
alisema.
Pia wanashauri mchakato wa kuwapata wanawake wenye ulemavu
katika upande wa Zanzibar ukamilike hukohuko na sio kuwashindanisha na wa
Tanzania Bara, huku akisisitiza kuwa iwapo mwakilishi huyo anafariki nafasi
hiyo izibwe na kundi hilohilo.
Mkurugenzi huyo alisema kinachofanyika kuhusu viti maalum
hakitafsiri dhana nzima ya maalum, hivyo ni nvema shria zikabadilika na kuakisi
hilo.


