"Afichaye dhambi zake
hatafanikiwa, Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema"Mithali
28:13-14.
Nukuu hii ya maneno haya
kutoka katika Biblia takatifu yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma
Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Theopista Mallya wakati akitoa
salamu za sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania
Dayosisi ya Dodoma Jimbo la Makao Makuu ushirika wa Arusha road.
Kamanda Mallya amesema
kupitia sikukuu hii waumini wa dini kikristo walikuwa katika kipindi cha
mfungo, kufanya toba na matendo ya huruma, endeleeni kumcha mungu na
kuacha dhambi".
Aidha, Kamanda Mallya
amewataka waumini wa dini hiyo kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kufanya
vitendo vya kikatili kwa binadamu mwenzie hususani matukio ya mauaji na
kukatisha uhai wa mtu jambo ambalo ni kinyume na sheria.
"Mwenye mamlaka ya
kukatisha uhai wa mtu ni Mungu peke yake, hivyo kupitia maungamo na sala
mlizofanya katika kipindi cha mfungo Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma hatutegemei
kuwepo kwa matukio ya mauaji pamoja na uhalifu mwingine."amesema Kamanda
Mallya.
Jeshi la polisi mkoa wa
Dodoma limeshiriki ibada ya pamoja March 31, 2024 na waumini wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Dodoma pamoja na kushiriki harambee.
Toka Dawati la Habari Dodoma.




