..............................................................................................
NA JOHN BANDA, DODOMA
Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
yanayotarajiwa kufanyika tarehe 8 Machi, 2024 wanawake kutoka Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma wameshiriki kwa pamoja kutoa Misaada
mbalimbali kwenye Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo
Hospitalini hapo leo tarehe 6 Machi, 2024 Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi
ya Taifa ya Mashtaka Bi. Chivanenda Luwongo amesema wanawake kutoka Idara na
Vitengo mbalimbali vya Ofisi ya taifa ya Mashtaka, wamechangishana fedha ambazo
wamezitumia kununulia mahitaji mbalimbali kwa ajili ya kuwapa msaada wagonjwa
waliolazwa kwenye hospitali hiyo ya Rufaa.
Bi. Luwongo amesema kuwa wametoa matibabu kwa
wagonjwa wanaume 3 na wanawake 2 waliolazwa kwa muda mrefu ambapo watagharimia
matibabu yao kwa muda wa siku 7 kwa kuwapa Dawa, Gharama za mtoto mmoja
anayefanyiwa upasuaji pamoja na dawa za siku tatu pamoja na wagonjwa wenye
mahitaji maalumu.

Ametaja misaada mingine kuwa ni pamoja na
Sabuni za kufulia na kuogea, mafuta ya kupaka, Asali kwa ajili ya wagonjwa
wenye majeraha na Maziwa kwa ajili ya watoto wadogo wanaotibiwa na kuhudumiwa
hospitalini hapo bila kuwa na wazazi.
Kwa upande wake Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Bw. Stanley Mahundo ameishukuru Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka kwa kuchagua Hospitali hiyo kwa ajili ya kutoa misaada mbalimbali kwa
lengo la kuwasaidia wanawake na watoto wanaougua maradhi mbalimbali huku
akiahidi misaada hiyo kuwafikia walengwa kama ilivyokusudiwa.

“Baadhi ya wanawake na watoto hawana ndugu wa
kuwahudumia ambao wanapata matibabu hapa hivyo kwa wanawake wa Ofisi ya Taifa
ya Mashtaka kutoa misaada hii mmefanya jambo la muhimu kwani misaada hii
itawasadia kwa kiwango kikubwa." Amebainisha hayo Muuguzi Mfawidhi.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatafanyika
Kitaifa tarehe 8 Machi, 2024 katika Wilaya ya Chamwino, Makao Makuu
Jijini Dodoma.



