Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Wanawake Wajasiriamali wenye mahitaji Maalum wakiwemo
Wenye uoni hafifu, wasioweza kutembea kutoka Mikoa ya Pwani na
Dodoma wanaoshiriki katika maonesho mbalimbali ya
ujasiriamali kuelekea Siku ya Wanawake duniani katika
Viwanja vya Mashujaa wameishukuru Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya
Afya kwa Umma kwa kuweka kipaumbele zaidi katika utoaji wa Elimu ya Afya pamoja
na ugawaji wa vielelezo ikiwa ni pamoja na Vizibao (Reflectors) katika maonesho
hayo.
Wakizungumza mara baada ya kupatiwa
vizibao(Reflectors) hivyo, baadhi ya Wanawake Wajasiriamali hao
wamesema vizibao hivyo vitasaidia katika kuepusha na ajali hasa
kipindi giza linapoingia hasa wanapotoka kazini kwani
waendedha wa vyombo vya usafiri ikiwemo magari na pikipiki watakuwa wanaona
kiurahisi na kuweza kuchukua tahadhari .
“ Tunashukuru sana Wizara ya Afya kwa kutupa hivi
vimeremeta vitatusaidia kututambulisha, tunapotaka kuvuka barabara watumiaji
wengine wa barabara itakuwa rahisi sisi kutuona na kutuepusha na ajali na pia
katika reflector hizi kuna ujumbe mahsusi namna ya kutambua afya zetu hasa afya
ya Uzazi”anasimulia Regina Mbaji Mkazi wa Kibaha Mkoani Pwani.
Naye Hapiness Mataji mwenye ulemavu wa kuona kutoka
mkoani Pwani anasema Wizara ya Afya imetoa mchango kwao .
“Nafurahi sana Wizara ya Afya imetupa kama
kitambulisho tunapovuka barabarani wadereva wanatutambua
haraka kwani ukivaa mavazi haya unaonekana haraka hata ukiwa
mbali”amesema Hapiness.
Habiba Mohammed Issa yeye anasimulia kuwa pindi
huduma za afya zitakapoanza kutolewa ikiwemo uchunguzi wa awali wa Saratani ya
Mlango wa Kizazi zitakapoanza kutolewa katika mabanda ya Wizara ya Afya yupo
tayari kwenda kupima afya huku akizungumzia namna vizibao vitakavyosaidia
kuepusha ajali kwani ataonekana haraka na watumiaji wengine wa barabara pindi
awapo barabarani.
Grace Msemwa ni Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya
amesema upokeaji wa Vizibao umekuwa na mwitikio mkubwa huku akitoa
wito kwa wananchi kupata fursa ya kutembelea mabanda ya Wizara ya Afya kuanzia
Machi 7-11, 2024.
MWISHO.


