
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri wameongoza mapokezi ya viongozi
walioteuliwa na kuapishwa ili kuitumikia Sekta ya Maji hapa nchini, wakiwa
pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Maji na watumishi wa wizara hiyo katika Mji
wa Serikali Mtumba.
Viongozi waliopokelewa katika ofisi za Wizara, Mji wa
Serikali Mtumba jijini Dodoma ni Naibu Waziri wa Maji Mhe. Kundo Methew (Mb) na
Naibu Katibu Mkuu Bi. Agness Meena.
Mara baada ya kupokelewa viongozi hao wameahidi
ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha Wizara ya Maji inapiga hatua katika
kufikia lengo la Serikali kufikisha huduma ya maji kwa kila Mtanzania, wa mjini
na vijijini.

Wamesema wanatambua mahitaji ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha upatikanaji wa
huduma ya maji unafika asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka
2025.
“Nimeziona nyuso za furaha kwa watumishi wa wizara.
Nina uhakika nitakuwa na furaha katika kazi yangu. Umoja wetu ndio nguzo yetu
ambayo itaweza kutufikisha kwenye malengo”. Mhe. Kundo amesema huku Naibu
Katibu Mkuu Bi. Meena, akiongeza kuwa wamekuja kufanya kazi baada ya kuaminiwa
hawataweza kumuangusha Mhe. Rais Samia katika kufanya kazi. Amesema kuwa
anategemea kujifunza mengi kutoka kwa watumishi wa Wizara na yupo tayari
kujifunza.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso pamoja na Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo Mhandisi Mwajuma Waziri kwa pamoja wamewahakikishia ushirikiano
na kwamba Wizara ya Maji ina watumishi wenye morali ya kufanya kazi.
Waziri Aweso ameongeza kuwa yapo mafanikio ambayo
yamefanyika ndani ya wizara hiyo ikiwemo kuwa kinara kwa miaka miwili mfululizo
Duniani katika utekelezaji wa miradi ya maji kupitia program ya Lipa kutokana
na matokeo (P for R) na kwamba mafanikio hayo yametokana na utayari wa
watumishi wa wizara.
Mhe. Aweso amesisitiza kazi ifanyike zaidi kwa
kutumia mifumo ya kisasa ya kidigital ili kurahisisha huduma kwa wadau wote wa
Sekta ya Maji. Pamoja na hilo ameainisha kuwa mafanikio yanapatikana kwa
kufanya kazi kwa moyo wa ushirikishwaji na kupendana miongoni mwa watumishi na
viongozi.