Mbunge wa Simanjiro (CCM), mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, amefichua kile kilichojificha nyuma ya pazia kuhusu kushambuliwa na risasi akisema siku moja kabla ya tukio hilo alifanya mazungumzo na viongozi wa juu, kuhusu hatma ya ardhi ya wafugaji inayotakiwa kubadilishwa kuwa maeneo ya hifadhi.
Ole Sendeka akiwa safarini alishambuliwa kwa risasi Machi 29 mwaka huu majira ya saa 12:45 jioni katika Kijiji cha Ngabolo, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Simanjiro, Ole Sendeka, amesema Alhamisi ya Machi 28 mwaka huu alikaa na viongozi kujadili suala la kupandishwa hadhi kwa mapori ya wafugaji.
“Niwape na siri nyingine. Ijumaa ndiyo nimeshambuliwa (Machi 29), Alhamisi (Machi 28), nilikaa na viongozi kujadili kupandishwa hadhi kwa mapori haya ya wafugaji. Tena viongozi wa ngazi za juu kabisa. Na tukaelewana, kila mmoja anasema hatutakubali ardhi yetu ibadilishwe kuwa ardhi ya wanyama. wamesema wenyewe.
“Lakini hii hainifanyi nisiende bungeni kusema. Ngojeni niwaambie, hotuba yangu ya kwanza bungeni haitakuwa kueleza kupigwa kwangu risasi.
…Itakuwa ni kueleza kwamba ardhi ya wafugaji wa Simanjiro, ardhi ya wafugaji wa Monduli, ardhi ya wafugaji wa Ngorongoro, ardhi ya wafugaji wa Longido, ardhi ya wafugaji wa Kiteto, ardhi ya wafugaji wa Same na Mwanga; wamependekeza nazo ziwe hifadhi katika ardhi wanazoishi wamasai.”
Katika mkutano huo, Ole Sendeka, amesema atakwenda kueleza kwamba serikali ikichukua hata kilomita moja katika eneo hilo, kwa ajili ya kisingizio cha uhifadhi ni kuweka rehani maisha ya wafugaji walioko hapo, kwa sababu wafugaji watakuwa hawana maisha tena.

