BANDA MEDIA BLOG

WAZAZI WASHAURIWA KUWA KARIBU NA WATOTO WAO NA KUZIENDELEZA NDOTO ZAO.

 



Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwandeti, John Massawe akizungumza  na wanafunzi pamoja na wazazi katika mahafali hayo shuleni hapo.

Afisa Maendeleo ya jamii Arusha DC, Stedvant Kileo akizungumza katika mahafali hayo mkoani Arusha
………
Happy Lazaro, Arusha .

Wazazi wameshauriwa  kuwa karibu na watoto wao ili waweze kuzitambua ndoto zao na  kuziendeleza  badala ya kuwakatisha tamaa kwa kile wanachotaka kufanya kwa maisha yao ya baadaye.

Hayo yamesemwa  mkoani Arusha na Afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya Arusha dc ,Stedvant Kileo wakati akizungumza katika mahafali ya 7 ya  kidato cha sita ambapo jumla ya wanafunzi   68 walihitimu masomo yao. 
Amesema kuwa,kumekuwepo na changamoto kubwa ya wanafunzi kukatishwa  ndoto zao na wazazi jambo ambalo  linawakatisha tamaa wanafunzi katika kuwa na mwamko wa kuendelea na masomo yao. 
“Wanafunzi wengi wamekuwa na ndoto za kuwa watu wakubwa katika maisha ya baadaye lakini wengi wao ndoto hizo hukatishwa na wazazi wao jambo ambalo halitakiwi  ni lazima wazazi watambue  wajibu wao katika kuwasaidia watoto wao.”amesema .
Mkuu wa shule hiyo ,John Massawe amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri mfululizo na hiyo ni kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa kati ya walimu na wazazi katika kushirikiana kwa pamoja. 
Aidha ametoa onyo  kwa wazazi wanaowashawishi watoto wao waseme uongo ili wasiende  shule au warudi nyumbani ,kuacha mara moja tabia hiyo kwani kwa kufanya hivyo inakuwa ngumu kwa watoto hao kuwa bize na masomo .
Makamu Mkuu wa shule hiyo ,Lekera Sekai amesema kuwa malengo waliyojiwekea kwa mwaka huu ni kuhakikisha wanafuta  kabisa daraja la nne  kwa kidato cha nne kwa kuhakikisha wanafunzi wanafaulu  wote na kuendelea kuwa shule ya mfano.
Amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kila mwaka katika matokeo ya kidato cha nne na sita na hiyo ni kutokana na ufundishaji mzuri uliopo shuleni hapo pamoja na walimu bora wanaohakikisha wanafunzi hao wanafikia malengo yao waliyojiwekea.
Aidha  Sakei amewaomba wazazi kuhakikisha wanawakumbusha watoto hao wajibu wao wa kujisomea pindi wanapokuwa likizo badala ya kuwaacha wakae  wakiangalia  tu vitu ambavyo havifai na vinawapotezea muda mwingi.
Naye Afisa elimu taaluma sekondari kutoka Arusha dc ,Prosper Kessy amesema kuwa,amekuwa akisimamia ipasavyo swala zima la elimu kwani katika halmashauri hiyo elimu ndio kipaumbele  na kwa kufanya hivyo imesaidia sana kuendelea kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi katika halmashauri hiyo.
Kessy amesema kuwa,halmashauri hiyo imekuwa ikifaulisha kwa asilimia 97.3 na hiyo ni kutokana na ushirikiano wa karibu uliopo katika ya wazazi na walimu kwani wamekuwa wakishirikiana kwa karibu sana katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao mashuleni .
“Nawaomba wazazi watoe ushirikiano wa kuchangia fedha kwa ajili ya uzio wa shule kwani shule wanapokuwa na uzio inasaidia sana kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na kuondokana na changamoto mbalimbali .”amesema Kessy.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG