|
|
|
Wanajeshi wa Afrika Kusini. |
.
Mwezi Februari, serikali ya
Afrika Kusini ilipeleka wanajeshi 3,000 kujiunga na wengine 1,000 ambao tayari
walikuwa katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
linalokumbwa na vita.
Wakati huo, Pretoria ilisema
kupelekwa kwa wanajeshi hao ilikuwa sehemu ya dhamira yake ya kulinda amani
barani Afrika, na kuisadia DRC kukabiliana na mashambulizi ya waasi.
Lakini sasa, wanajeshi hao
wanasema hawana vifaa vya msingi, na kuwaweka katika hatari kubwa.
Afrika Kusini inakabiliwa na
changamoto kadhaa za kiuchumi.
Waziri wa ulinzi, Thandi
Modose, aliwambia waandishi wa habari hivi karibuni mjini Pretoria kwamba
helikopta tano tu za usafiri kati ya 39 ndizo zinafanya kazi, na kwamba ni
helikopta tatu tu kati ya 11 za kufanya mashambulizi ndizo zinaweza kuruka.
Wizara yake inakiri kuwa
ilishindwa kusaini kandarasi mpya na kampuni ya kutunza na kukarabati ndege
hizo.
Wanajeshi nchini DRC wanasema
pia kwamba hawapati huduma za madaktari na waaguzi, na wakati mwingine hulala
njaa baada ya kukosa chakula.
Kiongozi wa chama cha jeshi
la taifa Pikkie Greeff, anasema serikali ilipeleka wanajeshi wake katika moja
ya maeneo hatari zaidi ya vita duniani bila vifaa, ufadhili na mafunzo muhimu.
“Wanajeshi wa Afrika Kusini
wanalazimika kuweka kambi mpya, wakiwa pia na fikra ya kushambulia sio
kujilinda. Hiyo ni njia mpya ya kujifunza kwa jeshi kwa sababu hatujafanya
mazoezi hayo.
Usipofanya mazoezi mara kwa
mara, hautatekeleza vizuri. Kando na hayo, kuna changamoto za kifedha mbali na
uwezo wa wanajeshi hawa. Hakuna ndege ya kubeba vifaa muhimu ambavyo wanajeshi
wanahitaji walipopelekwa ili kuwasaidia kikamilifu,” alisema.
Tangu mwezi Februari, waasi
wa M23 wameua wanajeshi kadhaa wa Afrika Kusini wanaopigania ardhini, na
kujeruhi wengine kadhaa katika shambulio la kombora.
Greeff anasema anazungumza na
wanajeshi walioko DRC kila siku, na ari yao iko chini. Anasema wengine wanahisi
kwamba wako katika “operesheni ya kujiua.”
“Watu hawa wako katika hatari
kubwa. Kupelekwa kwao kuliamualiwa kwa haraka sana. Kama kulikuwa mpango,
mpango huo haukujadiliwa kwa uwazi kwa sababu kwa hakika wanajeshi walio
uwanjani wanaachwa katika hali ngumu kwa sababu ya uhaba huu wa vifaa na mambo
mengine. Hali ni tete sana,” aliongeza.
Akizungumza bungeni hivi
karibuni, Rais Cyril Ramaphosa alikanusha kuwa utawala wake ulipeleka wanajeshi
nchini DRC “ kwa maslahi” na bila msaada unaohitajika.
Alisisitiza kuwa wanajeshi
wake wako “tayari kupigana na wana uwezo wa kutosha.”
Lakini Greeff anasema
wanajeshi zaidi wa Afrika Kusini watajeruhiwa na kuuawa nchini DRC, iwapo
hawatapata uwezo wanaohitaji.
Wachambuzi wa masuala ya
kijeshi na ulinzi wanasema nia ya serikali ya Afrika Kusini ya kulinda amani
hailingani na fedha zinazohitajika ili kuhakikisha mafanikio yao.
