Mawaziri wa Fedha wa Kenya, Tanzania na Uganda wakionyesha bajeti za mwaka wa fedha 2024/2025.
Raia wa Afrika Mashariki, hasa kutoka Tanzania,
Kenya, Uganda na Sudan Kusini, kwa mara nyengine, wanategea sikio leo hii
ambapo nchi zao zinawasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa ajili ya mwaka wa
fedha 2024/25.
Waziri wa Fedha nchini Tanzania Mwigulu Nchemba, kwa
niaba ya serikali ya nchi hiyo, atawasilisha bajeti ya shilingi trilioni 49.34,
ambayo ni sawa na ongezeko la asimilia 11.2 ya bajeti ya mwaka 2023/2024 ambayo
ilikuwa shilingi trilioni 44.3.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha, asilimia 70.1 ya
Bajeti Kuu inatarajiwa kutoka katika mapato ya ndani."Sehemu kubwa ya
bajeti asilimia 70.1 itagharamiwa na mapato ya ndani ambayo yanatarajiwa
kuongezeka kwa asilimia 10.0 mwaka 2024/25," alisema Nchemba.
Akinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini
Tanzania,
Mwanadiplomasia na mchambuzi wa siasa, Hamduni
Maliseli, amesema iwapo bajeti hiyo itatekelezwa kama ilivyokusudiwa, basi
inaweza kuleta mapinduzi katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, elimu na
uwekezaji.
atika Bajeti hiyo, serikali pia imeainisha vipaombele
vyake, ambapo imejikita zaidi katika mahitaji muhimu ikiwemo upatikanaji wa
huduma muhimu kwa wananchi kama vile maji, umeme na miundombinu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha ya Tanzania, shilingi
trilioni 15.78 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Hata hivyo, Bajeti ya mwaka huu inasomwa wakati
ambapo wananchi kutoka mataifa haya ya Afrika Mashariki, wamekuwa wakilalamikia
ugumu wa maisha unaosababishwa na kupanda kwa gharama za bidhaa muhimu ikiwemo
chakula.
Ni kutokana na hilo, ndio maana wananchi wa kada
mbalimbali ikiwemo wanafanyabiashara wadogo na wakubwa, wamejawa na shauku
kubwa ya kutaka kujua, iwapo mapendekezo ya bajeti ya mwaka huu yataleta afueni
yoyote katika maisha yao ya kila siku.
Waziri wa fedha wa Kenya Profesa Njuguna Ndung'u akifika bungeni ytayari kusoma bajeti ya mwaka wa 2024/25 / Picha kutoka Bunge la Kenya
Bajeti ya Kenya
Kwa upande wake, bajeti ya Kenya ya mwaka huu ni dola
za kimarekani bilioni 36.7, ambapo katika mwaka wa fedha uliuopita, ilikuwa
dola za kimarekani bilioni 28.5.
Serikali ya nchi hiyo inatarajia kukusanya dola
bilioni 16.9 kutoka mapato ya ndani.
Hata hivyo, nchini Kenya, kumeshuhudiwa mjadala mkali
kutoka kwa wananchi, ambao wamekuwa wakijaribu kutumia ushawishi wa mitandao ya
kijamii kuwahimiza viongozi wao kupiga kura dhidi ya mswada wa fedha ambao ni
sehemu ya bajeti kuu.
Miongoni mwa vipengele vya mswada huo ni pamoja na
kuongezeka kwa kodi katika bidhaa kadhaa muhimu ikiwemo mafuta ya kupikia,
mkate, na mawasiliano
“Katika hatua hii, kila anayeifanyia kampeni ni adui
wa umma, asiyeipinga ni adui wa umma, yeyote atakayeipigia kura ni adui wa
umma, yeyote atakayejizuia kupiga kura ni adui wa umma….tutawaangalia, msidhani
kwamba mtakapo kaa kando bila kupiga kura mtakuwa mmesalimika,” amesema Fanya
Mambo Kinuthia, mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya.
Katika hali ya kushangaza nchini Kenya, raia mmoja
ameonekana akijaribu kuunyakua mkoba wa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo ambao
ulikuwa na Bajeti Kuu ya nchi. Hata hivyo, mwananchi huyo ameishia kutiwa
mbaroni na vikosi vya ulinzi na usalama.
Waziri wa fedha Uganda Matia Kasaija anasoma bajeti yenye lengo la zaidi ya dola bilioni 19.3 kwa mwaka wa 2024/2025/ picha kutoka Bunge ya Uganda
Bajeti Uganda
Uganda nayo inasoma bajeti yenye lengo la zaidiya
dola bilioni 19.3. Hii ni ongezeko kutoka kwa dola bilioni 14.1 ambayo bajeti
ya mwaka wa 2023/2024 ilitangaza.
Nchi hiyo imelenga kupata zaidi ya dola bilioni 8.6
kutoka kwa mapato ya ndani ya nchi .


