Mwezi wa Juni kila mwaka unashuhudia kusomwa kwa bajeti za nchi kadhaa za Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mwezi Juni kila mwaka unashuhudia kusomwa kwa bajeti
kuu za nchi kadhaa za Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani EAC kwa ajili ya mwaka
mpya wa fedha.
Lakini utamaduni huu wa nchi kusoma bajeti kwa wakati
mmoja ulianzia wapi na kwa nini?
Rwanda, Uganda, Kenya, na Tanzania zimekuwa zikifanya
hivi kulingana na maelekezo ya mwaka 2010 ya Baraza la Mawaziri la EAC.
Wanafanya hivyo ili kuoainisha sera zao za kifedha
ili kuendana na matakwa ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na hatimaye Sarafu
moja.
Sababu nyengine ni kuepusha uwezekano wa nchi moja
kujinufaisha kwa kushusha au kupandisha kodi kwa faida yake dhidi ya nchi
nyingine.
Kwa mfano, Kenya ingesoma bajeti yake na kupanga bei
ya mkate kuwa shilingi 60, Tanzania ingefuata mfano huo wiki au miezi kadhaa
baadaye na kuweka bei yake kuwa shilingi 50 na wiki chache baadaye Rwanda
pengine ingefuata mkondo huo na kupanga bei ya mkate huo huo kuwa shillingi 45
halafu Uganda nayo ikaweka shillingi 40.
Hii itakua na athari katika soko la kanda la Afrika
mashariki.
Mwaka huu ni Tanzania, Kenya, Uganda na Sudan Kusini
zitakazosoma bajeti zao kwa wakati mmoja.
Hii ni kutokana na kwamba, Rwanda imeshasoma bajeti
yake mwezi wa 5 mwaka huu kwa sababu inaelekea kufanya mchaguzi mkuu mwezi
Julai, 2024.
Kwa upande mwengine, Somalia na DRC hazitosoma bajeti
zao siku hiyo hiyo, kwani bado hazijaainisha sera zao za kifedha na jumuiya ya
EAC. Hata hivyo, bajeti za mwaka huu wa fedha kutoka nchi za Afrika Mashariki,
zimejikita katika vipao mbele kadhaa, ikiwemo miradi ya kimkakati pamoja na
uwekezaji katika miundombinu muhimu.
Wakati huo huo, wananchi wanategea macho kuona ni kwa
kiasi gani bajeti ya mwaka huu itaathiri maisha yao ya kila siku, hasa
ikizingatiwa kwamba, kumekuwa na mapendekezo ya kuongeza kodi katika bidhaa
muhimu kama vile mafuta ya kupikia.
