Na Rose Jacob,BUNDA.
ZAIDI ya watu wawili hufariki dunia kila mwezi ,wilayani Bunda mkoani Mara, kutokana na ajali mbalimbali, wakati wananchi wakifanya safari ama shughuli za kiuchumi ndani ya ziwa Victoria.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Vicent Naano wakati akipokea msaada wa vifaa okozi hususani majaketi 20 kutoka Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), kufuatia ajali ya mtumbwi iliyotokea Septemba 15, 2024 katika Kijiji cha Igundu na kusababisha vifo vya watu sita.
Dk. Naano amesema asilimia kubwa ya wakazi wa wilaya hiyo, uchumi wao unategemea ziwa Victoria,hivyo suala la usafiri au shughuli zao ndani ya ziwa hilo ni jambo la kawaida,ambalo linakabiliwa na adha ya ajali za mara kwa mara,ambazo hupelekea vifo vya watu wilayani humo.
"Ajali zinatokea wananchi wakiwa wanasafiri au wanafanya shughuli zao,tumekuwa tukipoteza watu wengi, kila mwezi lazima kunatokea vifo, tayari tumebaini kuwa vifo vingine vinatokana na watu kutozingatia sheria za usafiri salama majini,
kutokana na hali hiyo tayari tumeishaanza kampeni maalum ya kuelimisha jamii kuzingatia suala zima la usalama wawapo majini,"amesema Naano.
Amesema kampeni hiyo mbali na kushirikisha wataalamu kutoka ofisi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), inahusisha maofisa kutoka halmashauri mbili za wilaya hiyo kutoa elimu kwa wananchi,wana boti maalum kwaajili ya ukusanyaji wa mapato yatokanayo na ziwa hilo,imeanza kutumika kutoa elimu kwa wananchi,hivyo jitihada zote hizi zitasaidia kupunguza ajali zitokeazo ndani ya ziwa Victoria.
Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria,Masinde Bwire, amesema ofisi yake imeamua kutoa msaada wa vifaa okozi,kufuatia ajali iliyotajwa hapo juu ambayo mtumbwi uliyokuwa umebeba abiria wakitokea arusini ambapo watu sita walifariki na wengine 14 kunusurika kwakile kilichodaiwa mtumbwi huo ulizidiwa na uzito mkubwa na haukuwa maalumu kwa kusafirisha abiria.
Amesema ipo haja ya Mamlaka husika kuchukua hatua za haraka za kudhibiti ajali ambazo zimekuwa zikitokea ndani ya ziwa hilo na kupelekea vifo ya watu wengi kila mwaka katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda,hivyo Kamisheni hiyo tayari wameanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya uokozi katika nchi zote tatu, huku kituo kikuuu kikijengwa mkoani Mwanza na vituo hivyo vitakapokamilika pamoja na mambo mengine vitasaidia kupatikana taarifa kwa haraka za ajali na uokoaji kufanyka mpema.
"Hili ziwa halitakiwi kuwa lango la kaburi,halitakiwi kuwa chanzo cha watu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupoteza maisha,bali linatakiwa kuwa chanzo cha uchumi wa watu wa Jumuiya, hatutaki tuwe tunakuja hapa kila mwaka kwasababu ya vifo bali tuwe tunkuja hapa kwaajili ya miradi mikubwa ya kimaendeleo na kiuchumi, " amesema
Aidha amesema miaka miwili iliyopita matukio yaliyotokea katika Kata ya Igundu na kusababisha vifo vya watu 20,wakiwepo wanafunzi 13 wa Shule ya Msingi Bulomba yanaskitisha hivyo ipo haja ya kuhakikaiha matukio hayo hayatokeo tena.
Wakizungumza baada ya kupokea msaada wa maboya okozi kutoka Kamisheni hiyo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Igundu wilayani humo, walisema ajali nyingi zinazotokea zinasabaishwa na wamiliki wa mitumbwi kutokufuata sheria na taratibu.
Nyanjiga Mafuru,amesema "ili kukomesha ajali hizo hatua kali zichukuliwe dhidi ya watu, hususani wamiliki wa mitumbwi ya uvuvi wanaotumia mitumbwi hiyo kusafirisha abiria,wakati wakijua leseni zao siyo za usafirishaji bali ni za uvuvi na uwezo wa kubeba watu wanne au watano,lakini unabadilishiwa matumizi na kubeba watu zaidi ya 20 hii ni hatari tunaomba hatua zichukuliwe.
Tags
HABARI
