AFISA Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki (COSOTA) Bi.Doreen Anthony Sinare akifafanua jambo wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari - MAELEZO jijini Dodoma.


AFISA Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki (COSOTA) Bi.Doreen Anthony Sinare,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan leo Machi 21, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
- yatoa vyeti 7,670 vya uthibitisho na umiliki haki miliki-
NA JOHN BANDA, DODOMA
AFISA Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki (COSOTA) Bi.Doreen Sinare leo Machi 21,2025 mbele ya waandishi wa habari amebainisha kuwa taasisi hiyo imepokea migogoro 136 na kuitatua 118, huku akijivunia kutoa jumla ya vyeti 7,670 vya uthibitisho wa umiliki wa hakimiliki kwa ubunifu kwa waliosajili kazi zao
Afisa Mtendaji huyo, amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Bi.Sinare amesema kuwa usajili wa kazi zinazolindwa na Sheria ya hakimiliki na hakishiriki umeongezeka kwa asilimia 70 Ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kuanzia mwaka 2021 mpaka Februari 2025,
“COSOTA imesajili kazi za Sanaa na uandishi 11,519 na Wabunifu 3,436. Idadi hiyo ya wabunifu pamoja na kazi zao imetokana na zoezi la utoaji wa elimu na mafunzo mbalimbali ya hakimiliki na usajili kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina lakini pia kushiriki matukio mbalimbali ya wadau”amesema Bi.Sinare
Aidha Bi.Sinare amesema kuwa COSOTA ilipata fursa ya kuelimisha wadau kuhusiana na hakimiliki na uhamasishaji wa usajili wa kazi za hakimiliki.
Amesema katika kipindi hicho kamati maalumu ya Usajili ndani ya COSOTA inayojihusisha na masuala ya usajili, imefanikiwa kutoa mafunzo na ufafanuzi kuhusiana na hakimiliki kwenye kazi zilizopokelewa katika kipindi hicho kwa idadi ya wabunifu 167.
Hata hivyo amesema katika kipindi cha Miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan COSOTA imefanikiwa kupokea jumla ya migogoro 136.
Amesema Kati ya Migogoro hiyo Migogoro 118 imetatuliwa, migogoro 10 haijafanyiwa kazi bado na Migogoro 8 bado inafanyiwa kazi, huku akiweka wazi kuwa tasinia za Muziki na Filamu ndizo zinazoongoza kwa migogoro hiyo
