BANDA MEDIA BLOG

No title

 HECHE: MSIGWA ASITEGEMEE KUREJEA CHADEMA KWANI AMESAHAU NINI?



Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, John Heche, amesema kuwa chama hicho hakina nafasi wala sababu ya kumpokea tena aliyekuwa kada wake, Msigwa, akidai kuwa tayari alishiriki katika harakati zilizoisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupata ushindi katika uchaguzi uliopita.


Heche alitoa kauli hiyo leo, Mei 25, 2026, alipokuwa akizungumza na maelfu ya wanachama na wafuasi wa CHADEMA katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Dodoma.


Akizungumza kwa msisitizo mbele ya umati huo, Heche alisema CHADEMA haiwezi kupokea viongozi au wanachama waliokisaliti chama hicho kwa kushiriki kuisaidia CCM, huku akimtaja Msigwa kuwa miongoni mwa watu waliopoteza sifa ya kurejea ndani ya chama hicho.


“Aliyempa kadi ya uanachama Msigwa atarudi kwenye chama chake lakini sio CHADEMA. Hatuwezi kuchukua wachezaji wa sabu kutoka CCM wakati kikosi kimetimia,” alisema Heche huku akishangiliwa na umati wa wanachama waliohudhuria mkutano huo.


Katika kauli yake, Heche alidai kuwa Msigwa alishiriki katika uchaguzi uliopita kwa namna ambayo iliinufaisha CCM, hivyo haoni sababu ya yeye kurejea tena CHADEMA baada ya matokeo ya kisiasa kubadilika.


“Tunasema wazi kabisa, akale ubwabwa CHAUMMA maana CHADEMA hakuna tunachoweza kumpa. Mtu ameshiriki uchaguzi na umeipa ushindi CCM, leo unarudi CHADEMA umesahau nini?” alihoji Heche.


Kauli hiyo imeibua mjadala mkubwa wa kisiasa miongoni mwa wadau na wanachama wa vyama mbalimbali, huku baadhi wakitafsiri tamko hilo kuwa ni ishara ya msimamo mkali wa CHADEMA dhidi ya viongozi wanaohama vyama na baadaye kutaka kurejea.


Mkutano huo wa hadhara ulikuwa sehemu ya ziara ya viongozi wa juu wa CHADEMA inayolenga kuimarisha chama na kuhamasisha wanachama wake kuelekea shughuli za kisiasa zijazo nchini.


#arushatvonline

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG