BANDA MEDIA BLOG

MWAMKO WA ULIPAJI KODI KWA HIARI, CHACHU YA MWELEKEO WA KUJITEGEMEA KIBAJETI KWA ASILIMIA 74.2

 


NA: DK. REUBENI LUMBAGALA

Waasisi wa taifa letu walipambana na wakoloni ili kujinasua kutoka kwenye makucha ya kutawaliwa na kuamuliwa nini cha kufanya ili hali uwezo wa kufanya hivyo tulikuwa nao.

Disemba 09, 1961, tukapata uhuru kamili wa kisiasa lakini tukiwa hoi kiuchumi, hivyo kuwa na wajibu wa kujenga uchumi imara wa kutufanyia tuheshimike kwa wengine.

Wenye wajibu wa kujenga uchumi ni wananchi wenyewe wa nchi husika. Mathalani, kwa Tanzania, ni sisi Watanzania wenyewe ambao tunawajibika kuijenga nchi yetu kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Ni hivi: Hatuna mjomba wala shangazi wa kuja kuijenga Tanzania yetu. Ni sisi Watanzania wenyewe ndiyo wahusika wa kuijenga nchi yetu, kuhakikisha tunatatua changamoto zilizopo na kukuza ustawi wetu kwa maendeleo endelevu.

Kazi kubwa ya kujenga uchumi imara na uboreshaji wa huduma za kijamii, inategemea sana uwepo wa raslimali fedha za kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Swali linakuja, tunapata wapi fedha za kutekeleza miradi na mipango ya maendeleo? Majibu yanaweza kuwa mengi, lakini jibu la msingi ni kupitia ukusanyaji wa kodi kutoka kwa wananchi wenyewe.

UMUHIMU WA TRA KATIKA KUFANIKISHA MIPANGO YA MAENDELEO

Julai 1, 1996, serikali ikaanzisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo hadi kufikia Julai 1, 2026, Mamlaka hiyo imetimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake. 

Pamoja na majukumu mengi ya TRA, moja kubwa ni kukusanya kodi kutoka kwa wadau kama vile wafanyabiashara, wafanyakazi, wajasiriamali, wawekezaji na wananchi kwa ujumla wenye sifa za kulipa kodi.

Kwa hakika, mageuzi makubwa yaliyofanywa, imeiwezesha TRA kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 531 mwaka wa fedha 1996/1997 hadi trilioni 32 mwaka 2025/2026.

Maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuifanya Tanzania kujitegemea kwa asilimia kubwa badala ya kutegemea misaada na mikopo ya wahisani, ambayo wakati mwingine imejaa masharti magumu, kutunyima uhuru wetu na hata kutweza utu wetu.

Aidha, kutokana na maono hayo, mapema mwezi Aprili 2021, Rais Dk. Samia alitoa maelekezo mahsusi kwa TRA kuongeza makusanyo ya kodi lakini kodi hizo zisiwe za dhulma, uonevu, ubabe na mabavu.

Ukweli ni kuwa, Rais alikuwa tayari mapato ya nchi yashuke hata kwa miezi miwili au mitatu, lakini kujengwe misingi imara na rafiki katika ukusanyaji kodi bila kuwaumiza walipakodi na wananchi ambao ndiyo nyenzo ya ujenzi wa taifa.

Leo, TRA inapoadhimisha miaka 30 na taifa letu linaloelekea maadhimisho ya miaka 65 ya uhuru wake, tuna kila sababu ya kusema “Tumeupiga mwingi katika makusanyo ya kodi, lakini tusibweteke, tuna kazi kubwa ya kujenga taifa linalojitegemea”.

Nasema haya kwa sababu, bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, asilimia 74.2 ni mapato ya ndani. Ni matunda ya Watanzania kusema tunaweza tutajenga nchi kwa nguvu zetu, kama kusaidiwa basi tusaidiwe katikati ya safari ya ujenzi wa Taifa letu, tena tusaidiwe kwa heshima kwa kuzingatia Tanzania imeimarisha sana diplomasia hasa ya kiuchumi na mataifa mengi ulimwenguni.

Hivyo, niwapongeze walipakodi na wananchi ambao wameipa heshima nchi yetu kwa kuongeza makusanyo ya kodi kwa mafanikio makubwa. Mwelekeo wa kujitegemea kibajeti utafanikiwa zaidi ya tulivyo sasa endapo kila mwenye sifa ya kulipa kodi atatimiza wajibu wake wa kulipa kodi tena kwa hiari.

Julai 01, 2026, Rais Dk. Samia alihudhuria hafla ya Tuzo za Rais kwa Walipakodi katika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam. Katika hafla hiyo, Rais alikemea “Kodi ya dhulma na dhulma ya kodi”.

Alifafanua kuwa, kodi ya dhulma ni kumlipisha mlipakodi zaidi ya kiwango kinachopaswa kulipwa na dhulma ya kodi ni kulipa kiwango cha chini cha kile kinachopaswa kulipwa.

Kimsingi, msisitizo wa Rais ni kuwa, kila anayepaswa kulipa kodi alipe kiwango kinachopaswa kulipwa ili kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi kwa maendeleo endelevu ya kizazi cha sasa na kijacho.

Maoni: 0620 800 462.     

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG