Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.
Florence Temba akiwaeleza waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusu
utaratibu wa Serikali kutumia TEHAMA katika kufanya mikutano kwa kutumia
mfumo wa Mawasiliano ya (Video comference) ambapo kikao kimoja
kitawaunganisha pamoja washiriki kutoka Mikoa 8 ambapo mada
huwasilishwa na kutoa fursa ya kuwasiliana moja kwa moja (interactivity)
kwa maswali na ufafanuzi leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bi Zamaradi Kawawa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi Zamaradi Kawawa akifafanua jambo kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano kati ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na vyombo vya habari uliofanyika leo jijini Dar es asalam.Kulia kwake ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Florence Temba na Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Priscus Kiwango.
Baadhi ya waandishi wa habari
wakifuatilia mkutano wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi kuhusu
utaratibu wa Serikali kutumia TEHAMA katika kufanya mikutano ambapo
mfumo wa Mawasiliano ya (Video comference) utatumika ili kupunguza
gharama za mikutano kwa Taasisi za Serikali.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.
Florence Temba akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari kuhusu faida za
kutumia TEHAMA ikiwemo kuokoa fedha zilizokuwa zinatumika awali kuandaa
mikutano hiyo ambapo kwa sasa washiriki watashiriki mikutano hiyo wakiwa
katika vituo vyao vya kazi leo jijini Dar es salaam. Kulia ni
Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma Bw. Priscus Kiwango.
(Picha na Frank Mvungi-Maelezo)
..…………………………………………………………………………………………
Na Jovina Bujulu-MAELEZO
Uanzishaji wa matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Serikalini utaboresha na
kuongeza ufanisi wenye tija ambao utapunguza gharama za utendaji na
kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kupitia utaratibu huu wa vikao
kazi ambavyo vitaendeshwa kwa kutumia mfumo wa mawasiliano ya video
ambapo kikao kimoja kitaunganisha kwa pamoja washiriki kutoka mikoa nane
ambapo mada huwasilishwa na kutoa fursa ya kuwasiliana moja kwa moja
kwa maswali na ufafanuzi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma Bw. Florence Temba alipokuwa akiongea na waandishi wa habari
kuhusu matumizi ya TEHAMA katika kupunguza gharama za uendeshaji vikao
kazi.
Mfumo wa mawasiliano ya video ni
teknolojia inayowezesha mawasilano kutoka vituo mbalimbali kuwasiliana
kwa njia ya sauti na picha kwa njia ya kielekroniki bila kuhitaji
kukutana eneo moja.
“Teknolojia hii ya kutumia mfumo
wa mawasiliano ya video itapunguza gharama mbalimbali za uendeshaji
vikao Serikalini ambazo ni pamoja na kukodi kumbi za mikutano, usafiri
na muda ambao hutumika nje ya vituo vya kazi” alisema Temba.
Aidha, Bw. Temba alisema kuwa
utaratibu wa vikao ni rasmi kama ilivyo mikutano mingine ya kazi ambao
ni salama kwa kuwa miundo mbinu yake inaratibiwa na Serikali.
Bw. Temba aliendelea kusema kuwa
mwongozo wa mawasiliano kwa njia ya video umetolewa na unapatikana
katika tovuti ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
“Mwangozo huu unahusu wajibu wa Wizara, idara, Wakala za Serikali na
Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika kuboresha mawasiliano kwa njia ya
video” aliongeza Bw.Temba
Pia mwongozo huo unaainisha
mazingira na vifaa ya kuendesha mawasiliano kwa njia ya video kuzingatia
sifa na viwango vya chini na kuhakiki mfumo huo kabla ya matumizi.
Mfumo huo ulianzishwa na
Serikali mwaka 2013/2014 katika mikoa ya Kilimanjaro, Kagera, Morogoro
na Iringa kati ya utumishi na mamlaka za Serikali za mitaa ambapo kwa
sasa mawasiliano hayo yanapatikana nchi nzima isipokuwa mikoa mipya ya
Geita, Simiyu, Katavi na Njombe.
Tags
HABARI KITAIFA


