Mkoa wa Dodoma umeanza rasmi
kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli lililotaka kufanyika kwa usafi wa mazingira katika maeneo
mbalimbali ya nchi siku ya tarehe 9 Disemba, 2015 kama mojawapo ya maadhimisho
ya siku ya uhuru na kuwataka viongozi na wataalamu kusimamia utekelezaji wa
agizo hilo.
Tayari Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Mhe. Chiku Gallawa ameshakutana na viongozi mbalimbali wa Mkoa na Taasisi zilizopo
Mkoani Dodoma kujadili na kupanga
mikakati ya utekelezaji wa agizo hilo. Vilevile Mhe. Chiku Gallawa amekutana na
maafisa watendaji wa kata na maafisa maendeleo ya jamii, Afya, Usafi na
Mazingira na Waratibu elimu kata na kupanga namna bora ya utekelezaji wa agizo
hilo na namna ya kuwaelimisha na kuwashirikisha wananchi kwenye maeneo yote.
Katika maamuzi yaliyofikiwa,
Uongozi wa Mkoa umepanga zoezi la ufanyaji usafi lianze mapema kabla ya tarehe
9 Disemba na kuwa litakuwa endelevu ambapo mazoezi ya kufanya usafi kwenye Mkoa
wa Dodoma yatakuwa ya aina mbili yakianzia saa 1:00 hadi saa 3:00 asubuhi.
Zoezi la kwanza litakua la
usafi wa kila siku ambapo wananchi watakua wanafanya usafi kwenye maeneo yao ya
makazi na shughuli mbalimbali chini ya usimamizi wa viongozi na wataalamu
waliopo kwenye ngazi za Kata na baadae taarifa za kila siku juu ya nini
kilichofanyika kwenye zoezi la usafi zitakuwa zinatumwa kwa wakurugenzi wa
Halmashauri za Wilaya na Manispaa.
Zoezi la pili litakuwa usafi wa
kila siku za Jumamosi ambapo taasisi zilizopo Mkoani Dodoma zitakuwa zinakwenda
kushiriki kufanya usafi pamoja na wananchi kwenye maeneo ambayo wananchi
watakuwa wameyapendekeza kufanyiwa usafi wa pamoja na hususani yale
yanayohitaji nguvu ya pamoja kama vile maeneo ya huduma za jamii na yale ambayo yamekithiri kwa uchafu. Utaratibu
utakaotumika utakuwa kuzigawanya taasisi kwenda kwenye mitaa tofauti kufanya
usafi na wananchi wa maeneo hayo.
Mhe. Chiku Gallawa ametaja kuwa
mazoezi hayo yanaaanza mara moja na kuwa siku ya tarehe 9 Disemba itakuwa siku
ya kutathimini kazi ya usafi inayoendelea na pia utafanyika usafi kwenye maeneo
ya huduma za jamii. Kwa kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma jumamosi ya
Novemba 28, 2015, watumishi na viongozi wake wote watajumuika pamoja kufanya
usafi wa mazingira kwenye jengo la zamani la ofisi ya Mkuu wa Mkoa lililoko
kwenye makutano ya barabara ya Mtaa wa Nyerere na barabara ya Mpwapwa.
Mkuu wa Mkoa amebainisha kuwa
maagizo yaliyotolewa kwa mamlaka za serikali za mitaa katika ukaguzi na
usimamizi wa zoezi la usafi kwenye
maeneo ya makazi na shughuli mbalimbali ni pamoja na ukaguzi wa vyoo, usafi
wa mazingira ya makazi, maeneo ya huduma za jamii, maeneo ya utupaji taka.
Maelekezo mengine ni pamoja na matumizi ya sheria ndogo kama kutoa ILANI,
Makatazo na adhabu za Faini kwa makosa ya uchafuzi wa mazingira.
Uongozi wa Mkoa wa Dodoma
umeelezea kuwa zoezi hili la kufanya usafi wa mazingira kila siku na usafi wa
pamoja wa kila siku za jumamosi utasaidia kupunguza magonjwa mengi yatokanayo na
uchafu wa mazingira kama vile kipindupindu, kuhara na magonjwa mengine ya
milipuko.
Tags
HABARI KITAIFA