Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa
Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kushoto) akipokewa na
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo
alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es
salaam.
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa
Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (katikati) akiwasili Ofisi za
Wakala ya Serikali Mtandao kwa ziara ya kikazi leo jijini Dar es
salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi
ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kushoto)
kuhusu utendaji wa Wakala hiyo leo wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe.
Angella Kairuki katika Ofisi za Wakala hiyo leo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Uratibu wa
Miundombinu ya TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao Bw. Benjamin Dotto
akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mhe. Angella Kairuki (kulia) kuhusu kituo cha ufuatiliaji mifumo ya
mawasiliano Serikalini leo jijini Dar es salaam.
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa
Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kulia) akitembelea maeneo
mbalimbali ya Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao leo. Kushoto ni
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo
alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es
salaam.
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa
Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki akizungumza na Watendaji na
baadhi ya Wafanyakazi wa Wakala ya Serikali Mtandao leo alipofanya ziara
ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam.
…………………………………………………………………………………………….
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Serikali imepiga marufuku
matumizi ya Barua pepe za kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au
kupokea taarifa za Serikali na kuwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa
wanatumia mfumo rasmi wa Mawasiliano ya Barua Pepe Serikalini (GMS)
ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha mawasiliano kwa njia
ya Mtandao.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Mhe.Angella Kairuki alipokuwa akizungumza na Watendaji na
Watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao ( e Government Agency) wakati wa
ziara yake ya kukagua utendaji na ufanisi wa matumizi ya TEHAMA
Serikalini.
“Sasa kuna watumishi 7000
wanaotumia anwani za Barua pepe za Serikali ,idadi hii ni ndogo lazima
iongezeke, hatuwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa taarifa za Serikali
kwa kutumia Barua Pepe nje ya mfumo huu” Amesisitiza na kuongeza kuwa
Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye
mawasiliano binafsi.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa
uimarishaji wa mawasiliano ya TEHAMA Serikalini na kuongezeka kwa
matumizi ya TEHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia mitandao
mbalimbali ipo haja ya kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia
Barua Pepe za Serikali.
Mhe. Kairuki amewataka watendaji
wa Wakala hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia uratibu wa zoezi hilo ili
kuhakikisha kuwa Wizara, Idara na Taasisi zote za umma zinaunganishwa
na mfumo rasmi wa Serikali ili kuwa na mfumo mmoja wa Mawasiliano.
“Katika hili ninatoa siku 60
muhakikishe kuwa mnakamilisha kwa Taasisi zilizobaki ili kwa wale
watakaopuuzia hatua zianze kuchukuliwa” Ameeleza Mhe. Angella.
Aidha, ametoa wito kwa watendaji
wa Wakala hiyo kuweka mpango wa kuwawezesha na kuwajengea uwezo wa
kitaaluma watumishi waliopo kazini kwa kujenga utaratibu wa
kuwarithisha uzoefu watumishi ili kuendelea kuimarisha ufanisi na
utendaji wa Wakala hiyo.
Mhe. Kairuki amewataka kuwa
wabunifu katika kuanzisha mifumo mipya ya TEHAMA ili kuimarisha dhana
ya Serikali mtandao ili kupunguza gharama hadi kufikia asilimia 5 ya
fedha zinazotumika kuendeshea masuala mbalimbali ambayo yangefanywa
kupitia matumizi ya TEHAMA.
Akizungumzia kuhusu ununuzi wa
vifaa vya TEHAMA serikalini ameitaka Wakala hiyo kutoa ushauri ili
kudhibiti mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha katika
kununulia vifaa hivyo kwa gharama kubwa wakati vinaweza kupatikana kwa
bei ya kawaida.
“katika hili Serikali itachukua
hatua kwa yeyote atakayebainika katika upotevu wa mapato muhakikise
mnazisaidia Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika masuala ya
ununuzi wa mifumo na vifaa vya TEHAMA ili mifumo inayonunuliwa iwe na
manufaa kwa wananchi na thamani halisi ya fedha”
Amesema Serikali itaendelea
kuboresha utoaji wa huduma kupitia mtandao ili wananchi waweze kupata
huduma hizo mahali walipo kwa gharama nafuu na kutoa wito kwa watumishi
wa Wakala ya Serikali mtandao (e-Gov) kuwa wabunifu katika kutengeneza
programu mbalimbali na mifumo salama itakayowasaidia wananchi kupata
huduma.
Aidha, katika hatua nyingine
ameitaka e-Gov kuendelelea kujenga uwezo katika kudhibiti dharura na
majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza katika matumizi ya TEHAMA na
kuitaka Wakala hiyo iendelee kulifanyia kazi suala la kuwezesha mifumo
ya Serikali kuzungumza kati ya taasisi moja hadi nyingine ili huduma
zote ziweze kupatikana katika eneo moja na kuondoa urudufu wa mifumo
iliyopo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa
Wakala ya Serikali Mtandao (e-Gov) Dkt. Jabiri Bakari akitoa taarifa ya
utendaji wa Wakala hiyo amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto
mbalimbali toka kuanzishwa kwake Julai 11, 2012 imeendelea kupata
ufanisi katika uimarishaji wa Serikali Mtandao.
Amesema kuwa Wakala hiyo
inaendelea kuhakikisha kuwa huduma za Serikali zinawafikia wananchi
kupitia mtandao mahali walipo na kuhakikisha kuwa inafanikisha lengo la
huduma zote za Serikali kupatikana chini ya dirisha moja.
Aidha amesema kuwa Wakala ya
Serikali Mtandao itaendelea kuhakikisha kuwa usimamizi wa viwango vya
matumizi ya TEHAMA katika Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali
vinazingatiwa.
Tags
HABARI KITAIFA