Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ilikutana mwishoni mwa wiki na kupitia kesi, mashauri
mbalimbali kuhusiana na usajili na mikataba ya wachezaji na viongozi
mbalimbali chini ya Makamu Mwenyekiti Wakili Mandi.
1. CHANGANYIKENI DHIDI YA POLISI DODOMA
Mchezaji Said Hamis Athumani
Kamati
ilibaini kweli mchezaji Said Athumani Hamis alikuwa mchezaji wa
Changanyikeni na taratibu za maongezi baina ya timu ya Polisi Dodoma na
Changanyikeni kazikukamilika, hivyo kuwataka wakubaliane kuhusiana na
fidia ya mchezaji kuhama kutoka Changanyikeni na baada ya maongezi
Polisi Dodoma waliridhia kuwalipa Changanyikeni kiasi cha Shilingi
400,000/= kiasi ambacho kilikubaliwa pia na timu ya Changanyikeni.
Kamati
imeitaka Sekretarieti kuandika barua Bodi ya Ligi kuifahamisha wawakate
fedha kiasi cha shilingi 400,000/= (laki nne tu) timu ya Polisi Dodoma
kwenye fedha watakazopewa na mdhamini.
2. PANONE DHIDI YA POLISI TABORA
Mchezaji Michael Chinedu
i.
Kwa kesi ya tuhuma za mchezaji Mohamed Jingo kuwa sio raia wa Tanzania
kamati imeona haina mamlaka ya kuthibitisha au kuamua uraia wa Mohamed
ii.
Pia imeamua kujiridhisha kama ni kweli timu ya Polisi Jingo, TFF
itaiandikia barua uhamiaji ili kupata uthibitisho wa uraia wa mchezaji
husika haraka. Kamati imeamua kujiridhisha kama timu ya Polisi Tabora
ilipata kibali cha Rais wa TFF kumtumia mchezaji Michael Chinidu bila ya
kumlipia dola 2,000 kama kanuni zinavyoeleza.
3. MAWENZI MARKET FC DHIDI YA BURKINAFASO
Mchezaji Victor Mswaki
Baada
ya kupitia kesi hii kamati ilijiridhisha kwamba klabu ya Burkinafaso Fc
ilimsajili mchezaji bila ya kuwasiliana na klabu yake ya Mawenzi Market
na yakwamba kanuni zinataka klabu inayotaka kumsajili mchezaji wa timu
nyingine iwasiliane na timu inayommiliki mchezaji husika na kufikia
makubaliano.
Kamati
imeona timu ya Mawenzi Market wanayo haki ya juu ya mchezaji Victor
Mswaki na hivyo kwa kuwa Burkinafaso FC iliongea kinyemela na mchezaji
inatakiwa iilipe klabu ya Mawenzi Market na wamekubaliana kulipana kiasi
cha Tsh 370,000/=.
4. KMC DHIDI YA AFRICAN LYON
Mchezaji Hamad Juma
Kamati
imeona na imejiridhisha ya kuwa Hamad Juma Hamad ni mchezji halali wa
African Lyon alisajiliwa kwa wakati na kwa kuwa usajili wake ulikubali
kwenye mtandao wa mawasiliano hivyo hakukuwa na ulazima wa jina lake
kuwekwa kwenye majina yanayohitaji pingamizi, hivyo kamati imejiridhisha
kwamba
mchezaji Hamad Juma Hamad ni mchezaji halali wa African Lyon na
imetupilia mbali malalamiko ya timu ya KMC na imetengua barua ya
kumsimamisha kucheza aliyoandikiwa na TFF baada ya KMC kuleta malalamiko
dhidi ya mchezaji huyo.
5. POLISI MOROGORO DHIDI YA BURKINAFASO
Mchezaji Victor Mswaki
Baada
ya kupitia kesi hii kamati ilijiridhisha kwamba klabu ya Burkinafaso Fc
ilimsajili mchezaji bila ya kuwasiliana na klabu yake ya Mawenzi Market
na yakwamba kanuni zinataka klabu inayotaka kumsajili mchezaji wa timu
nyingine iwasiliane na timu inayommiliki mchezaji husika na kufikia
makubaliano.
Mswaki
alisajiliwa na Burkinafaso ingawa TFF haikupewa taarifa sahihi vilevile
halikuwekwa pingamizi lolote wakati wa usajili. Hivyo kwa mujibu wa
kanuni 42(13) ya kanuni za Ligi daraja la kwanza kukitokea kasoro ya
namna hiyo ya usajili klabu husika itatozwa faini ya Ths 500,000/= na
matokeo ya uwanjani hayawezi kubadilishwa, kamati imeamua ya kwamba kwa
kuwa shauri hili linafanana na shauri jingine na mchezaji husika ni
yuleyule Victor Mswaki, hivyo klabu ya Burkinafaso haitaadhibiwa kwa
kosa lile lile la mara mbili, na kamati imeonelea mchezaji aendelee
kuichezea klabu yake ya Burkinafaso.
6. RHINO RANGERS DHIDI YA
Mchezaji Mohamed Jingo
Kamati
haina mamlaka ya kuthibitisha au kutengua uraia wa mchezaji husika,
hivyo Kamati imeitaka TFF iwaandikie barua uhamiaji kwa ajili ya
kuchunguza uraia wa mchezaji Mohamed Jingo na mara kamati itakapopata
uraia wa mchezaji husika itakaa kuliangalia suala hilo na kutoa maamuzi
ya kesi husika.
7. LIPULI FC DHIDI YA KIMONDO FC KWA
Mchezaji George Mpole
Kamati
ilijidhihirisha kwenye kikao chake cha mwisho cha tarehe 23 Desemba
ilitoa zuio la mchezaji George Enock Mpole kuichezea Kimondo FC baada ya
kupata barua ya pingamizi kutoka kwa Kurugenzi FC ikidai ni mchezaji
wao halali na kwamba pamoja na taarifa za usajili kutolewa kwa njia
mbalimbali ikiwa ni pamoja na press release namba 228 ambayo ilitolewa
kwa vilabu vyote na vyama vya soka vya mikoa na kwenye vyombo vyote vya
habari tarehe 24 Desemba bado klabu ya Kimondo pamoja na kupata taarifa
za kutomchezesha mchezaji husika ilikaidi amri ya Kamati na kumchezesha
mchezaji husika katika mchezo wao na Lipuli FC.
Aidha
kamati ilipata pingamizi kipindi cha pingamizi baada ya usajili
kufungwa tarehe 15 Desemba 2015, wiki ya tarehe 16-22 Desemba. Kwamba
kamati imeona usajili ulifungwa tarehe 15 Desemba 2015, na kwamba tarehe
16 hadi 22 Desemba 2015 ni muda uliowekwa kwa ajili ya kuweka
pingamizi. Katika muda huo klabu ya Kurugenzi ilileta pingamizi dhidi ya
mchezaji George E. Mpole. Na kwamba kamati hii ilikaa tarehe 23/12/2015
pamoja na maamuzi mengine kamati iliamua kwamba klabu ya Kimondo FC
isimchezeshe mchezaji husika yaani George Enock Mpole hadi
watakapoelewana na Kurugenzi ya Mafinga na kwamba watakapokubaliana
watatoa taarifa TFF ili TFF imruhusu mchezaji huyo aendele kucheza.
Na
kwamba barua iliyowasilishwa na Kimondo mbele ya kamati hii kwamba
walikubaliana tarehe 17/12/2015 haiwezi kuwa ushahidi mzuri kwa kuwa
malalamiko yalikuwepo na kamati ilikaa tarehe 23/12/2015 na endapo
kungekuwa na makubaliano katika hali ya kawaida kungekuwa na taarifa
ambayo haikuwepo. Na kwamba hata baada ya taarifa rasmi kutolewa na TFF
ya kwamba mchezaji amewekewa pingamizi na hatakiwi kucheza hivyo
wasimtumie mpaka wakikubaliana na klabu yake yaani Kurugenzi FC,
hawakuwahi kutoa taarifa yoyote hivyo basi klabu ya Kimondo S.C
imemchezesha mchezaji ambaye amesimamishwa na TFF.
Kanuni ya 42 (9) inasema kama ifuatavyo
“Timu
yoyote ambayo itamchezesha mchezaji aliyechini ya adhabu ya kufungiwa
/kusimamishwa au ambaye ametakiwa kulipa faini kwa maelekezo maalumu na
hajalipakwa mujibu wa kanuni hii itapoteza mchezo huo na timu pinzani
itapewa ushindi” Kwa mujibu wa kanuni hii kamati inatoa adhabu dhidi ya
timu ya Kimondo SC katika mchezo uliochezwa tarehe 26/012/2015 dhidi ya
Lipuli FC. Na kwamba timu ya Lipuli ndiyo itakuwa mshindi wa mchezo huu,
hivyo itapewa pointi tatu (3) na magoli matatu (3).
Mchezaji
huyo ataendelea kusimamishwa mpaka TFF itakapojiridhisha ya kwamba
taratibu za usajili zimekamilika. Kurugenzi ndio itakayotoa taarifa ya
utekelezaji wa maagizo ya kamati.
8. BURKINAFASO FC DHIDI YA KIMONDO FC
Mchezaji Innocent Baru
Madai
ya kwamba Burkinafaso Fc wanalalamikia kuwa mchezaji Innocent Boru
Namwandu siyo mchezaji halali wa Kimondo SC na kwamba wanapinga matokeo
ya mchezo yaliyotokea kwenye mchezo uliochezwa 2/01/2016 kati ya Kimondo
SC na Burkinafaso na kwamba mfumo wa usajili wa TFF unaonyesha kuwa
mchezaji huyo Innocent Boru Namwanda amesajiliwa na Kimondo SC na timu
ya Kurugenzi FC haijawahi kuwasilisha barua wala kuleta pingamizi lolote
TFF.
Kwa
hiyo kamati inaona kuwa shauri hili au lalamiko hili halina ushahidi
unaoweza kuthibitisha kuwa mchezaji huyo siyo mchezaji halali wa Kimondo
SC. Na kamati imetoa uamuzi huo ikizingatia kwamba TFF ilitoa muda wa
kuweka pingamizi lakini timu ya Kurugenzi FC inayosemekana ni mchezaji
wao hawakuwahi kuleta pingamizi lolote mpaka sasa.
Kwa hiyo ushahidi uliopo kwa sasa ni kwamba Mchezaji husika ni mchezaji wa Kimondo SC ambaye usajili wake ulipitishwa na TFF.
9. MKAMBA RANGERS DHIDI YA WENDA FC
Mchezaji Vicent Costa
Kesi
hii haikuwa na uwakilishi lakini kamati imeamua timu ya Wenda FC
iwalipe mara moja Mkamba Rangers kiasi cha shilingi laki tatu
(300,000/=) kama fidia ya kumpoteza mchezaji huyo.
Mchezaji anasimamishwa na timu za Wenda na Mkamba zitaandikiwa barua kufahamishwa kuhusiana na maamuzi ya kamati.
10. POLSII TABORA DHIDI YA AFRICAN SPORTS
Mchezaji Karim Humud
Klabu
ya African Sports wameridhia kuilipa klabu ya Polisi Tabora kiasi cha
Tsh 1,000,000/= toka kwenye vyanzo vyao vya mapato TFF/Bodi ya Ligi
hivyo mchezaji Karim Humud Juma ameruhusiwa kuitumikia klabu yake ya
African Sports kuanzia tarehe 15.01.2016.
11. AFRICA LYON dhidi ya Wachezaji
i. Morris Kaniki-Mwadui
ii. Miraji Athuman-Toto Africans na
iii. Emmanuel Simwanda-Mwadui
Kamati
ya Sheria na hadhi za wachezaji imeamua klabu husika ziandikiwe barua
ya kumalizana na African Lyon na wapewe wiki mbili toka tarehe
15.01.2016 hadi tarehe 30.01.2016 kama watashindwa kumalizana
watasimamishwa kuzichezea klabu hizo. Wakimalizana wapewe barua na
African Lyon ndiyo itakayotuma barua TFF kuwaruhusu waendelee
kucheza.
12. KESI MBALIMBALI ZA MADAI YA WACHEZAJI NA WALIMU
i.
Kesi namba moja kati ya Fadhil Msemi anayewawakilisha wachezaji 28 wa
KMC wanaodai malipo ya mishahara yao kwa mwajiri wao KMC
Kamati
imeamua mwakilishi wa wachezaji ndugu Fadhil Msemi akae na viongozi wa
KMC, katibu wao na mratibu wa timu wajadili na kupitia utaratibu wa
malipo namna viwango vya malipo kwa wachezaji hao vinavyopaswa kuwa na
iwasilishwe TFF Jumatatu.
ii.
Kesi namba mbili ilikuwa kati ya Stand United dhidi ya wachezaji na
wataalamu wake wanaoidai. Stand United iliwakilishwa na Ernest Brown kwa
barua kwa hiyo maamuzi yote ya Kikao yatakuwa halali.
Kesi zilizojadiliwa zilikuwa ni kama ifuatavyo.
a.
Kesi ya madai ya Mchezaji Peter Mutabuzi aliyeichezea Stand United
dhidi ya klabu yake, Mutabuzi aliwakilishwa na kiongozi wa klabu yake ya
sasa Frank Mchaki wa KMC.
Mchezaji
huyu alikuwa anaidai klabu ya Stand United kiasi cha Tsh 3,400,000/=
lakini kikao kilikubaliana alipwe kiasi cha Tsh 2,000,000/= ndani ya
mechi nane za ligi toka tarehe ya kikao 15.01.2015.
b.
Kesi kati ya Ndikumana Hamad dhidi ya Stand United, mwenyewe alikuwepo
na pia aliwakilishwa na Fadhil Hussein. Ndikiumana anaidai klabu ya
Stand malimbikizo ya mshahara, malazi na chakula kiasi cha shilingi
11,025,000/=. Wamekubaliana mchezaji anarudishwa kwenye klabu yake ya
Stand United kuitumikia na pia madai yake watamalizana huko Stand na pia
Stand imlipie gharama alizokuwa anaishi akiwa Dar es Salaam hotelini
maana mchezaji sio raia wa Tanzania.
c.
Ben Kalama ambaye alikuwa kocha wa makipa wa Stand United alikuwa
anadai malimbikizo ya mshahara wake kiasi cha Tsh usd 1,350
aliwakilishwa na Fadhili Hussein yeye walikubaliana kuwa anarudishwa
kwenye timu na watalipana huko huko madai yake. Kuhusu madai yake kiasi
cha dola 1,350 kamati iliamua kwa kuwa ni madai halali na mwakilishi
amekiri hilo basi wakatwe kwenye vyao vya mapato na TFF.
d.
Mathias Lule dhidi ya Stand ya madai ya mishahara, posho na medical
insurance kiasi cha Tsh 48,300,000/= aliwakilishwa na Fadhil Hussein.
Ilikubaliwa ya kwamba alipwe kiasi cha usd 4,300.00 ambacho
kimethibitishwa na kukubaliwa tayari na juu ya madai mengine watakaa na
muajiri wake wa zamani na kuyajadili kuona namna ya kulimaliza suala
hili. Fedha hiyo itakatwa kwenye vyanzo vyao vya mapato.
e.
JAKI FOOTBALL ACADEMY dhidi ya Stand United kiasi cha shilingi
7,600,000. Jaki waliwakilishwa na Fadhil Hussein ambaye alisema deni
wanaloidai Stand United ni kiasi cha Tsh 4,200,000/= na deni hili
limekubaliwa na litalipwa na Stand United kwenye vyanzo vyao vya mapato
toka TFF.
f.
Muhibu Kanu dhidi ya Stand United anayeidai mishahara, na posho klabu
ya Stand United kiasi cha Tsh 16,600,000/=. Makubaliano yamefikiwa kweli
Muhibu anaidai Stand kiasi hicho na ameshaanza kulipwa kupitia Bodi ya
ligi kiasi cha Tsh 2,600,000/= hivyo kiasi kilichobakia cha Tsh
14,000,000/= anaenda kujadiliana na muajiri wake kwa kuwa amerudishwa
kazini.
g.
Kesi kati ya aliyekuwa kocha msaidizi wa Stand United Emmanuel R.
Massawe dhidi ya Stand United anayeidai Klabu ya Stand United kiasi cha
Sh 12,100,000/= imehairishwa kwa kuwa muhusika hakuwepo wala hakutuma
muwakilishi.
3.
Kesi namba tatu ilikuwa ni kati ya Ndanda Fc dhidi ya wachezaji wake
wanaoidai timu hiyo. Kesi hii ilishindwa kusikilizwa kwa kuwa wachezaji
na wawakilishi wa wachezaji walikuwepo lakini klabu ya Ndanda FC
haikutuma mwakilishi pamoja na kuletewa mwaliko siku ya tarehe
12/1/2016.
Hivyo kamati iliamua yafuatayo
a.
Ndanda FC ikatwe kwenye vyanzo vyao vya mapato kiasi cha madai
yaliyothibitishwa na mwakilishi wao katibu mkuu kwenye kikao kilichopita
ambayo yalikuwa ya wachezaji wawili Rehani Kibingu kiasi cha tsh
2,000,000/= na Meshack Wilfredy Meshack aliyekuwa pia anadai kiasi cha
Tsh 2,000,000/=.
b.
Pamoja na katibu kuahidi kuleta ufafanuzi wa madai ya baadhi ya
wachezaji tarehe 28.12.2015 kwa barua TFF mpaka kikao cha tarehe
15.01.2016 hakuwa ameleta barua yoyote na timu haikuleta mwakilishi
kwenye kikao hicho hivyo basi kamati inaiagiza sekretarieti ya TFF
kuwaandikia barua kutaka kujua ufafanuzi wa madeni ya wachezaji
i.Said Mketo anayedai Tsh 2,720,000/=
ii.Salehe Malande anayedai Tsh 2,000,000/=
iii.Rajab
Isihaka anayedai kisai cha 3,720,000/= na pia kamati inataka kujua ni
namna gani klabu ya Ndanda FC itawalipa wachezaji hao wanaoidai.
c.
Kamati pia ilihakikishiwa na muwakilishi wa wachezaji ya kwamba
wachezaji Mohamed Upatu na Amir S. Msumi waliokuwa wanaidai klabu hiyo
kiasi cha Tsh 2,600,000/= kila mmoja hawaidai tena klabu hiyo na
walishamalizana nao.
Tags
MICHEZO KITAIFA