BANDA MEDIA BLOG

TOP 10 YA MATUKIO YA KUKUMBUKWA MAPINDUZI CUP 2016

Wachezaji wa URA FC wakishangilia ubingwa wao
Wachezaji wa URA FC wakishangilia ubingwa wao
Baada ya michuano ya Mapinduzi Cup kumalizika  January 13, 2016 na kushuhudia timu ya URA kutoka Uganda ikitwaa taji hilo, mtandao huu umekuja na ‘count down’ ya matukio 10 ambayo yatakumbukwa na wapenzi wa soka kutokana na matukio hayo kuwa gumzo kwenye michuano hiyo ya mwaka huu.

  1. Waandishi wa habari kulipa viingilio
Ni tukio ambalo liliwashangaza waandishi wengi wa habari hasa wale waliotoka Tanzania bara ambao walifika visiwani Zanzibar wakiwa na vitambulisho vilivyotolewa na shirikisho la soka Tanzania (TFF). Lakini katika hali isiyo ya kawaida, viongozi wa mashindano waligoma kuvitambua vitambulisho hivyo na kusisitiza vitumike vitambulisho maalumu vilivyotengenezwa kwa ajili ya mashindano.
Kibaya zaidi ni pale baadhi ya waandishi walipozuiwa kufanya kazi wakati wakisubiri vitambulisho vyao vitengenezwe, hivyo kuna waandishi walilazimika kulipa viingilio lakini wakati huo wakiwa na vitambulisho vyao shingoni vilivyotolewa na TFF.
  1. Naibu waziri wa michezo Zanzibar azuiliwa kuingia uwanja wa Amaan akidaiwa kitambulisho
Katika hali ambayo iliwashangaza watu wengi ni pale ambapo naibu waziri wa michezo visiwani Zanzibar alipopojikuta akikaziwa kuingia uwanjani na walinzi wa mlangoni ambao wanakagua ticket na vitambulisho vya watu wote wanaoingia uwanjani kupitia mlango wa VIP.
Mlinzi mmoja alisikika akisema “hakuna kujuana hapa, kama hauna kipande (kitambulisho) shingoni huwezi kuingia la sivyo kalipie ticket”.
Ilibidi viongozi wa kamati ya mashindano kutoa ufafanuzi wa kina kwa mlinzi huyo ndipo Naibu Waziri wa michezo akaruhusiwa kuingia uwanjani.
  1. Mechi ya Yanga vs Azam yageuka ulingo wa masumbwi
Mechi kati ya Yanga dhidi ya Azam FC hatua ya makundi iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana goli 1-1 ilijaa ubabe mwingi kiasi cha kuharibu burudani iliyotarajiwa na wapenzi wengi wa soka wa Zanzibar.
Wachezaji wote wa timu mbili walianza kuchezeana rafu mbaya ambazo zilipelekea kushikana mashati. Hiyo haikuishia kwa wachezaji tu, bali hata makocha wa timu hizo Hans van Pluijm na Stewart Hall almanusura wazitwange kavukavu wakati timu hizo zikielekea vyumbani wakati wa mapumziko. Makocha hao walianza kutupiana maneno ndipo wakavaana kutaka kuzichapa lakini waliamuliwa na wachezaji wao kabla mambo hayajawa mabaya.
  1. Kocha wa Azam FC Stewart Hall awatolea lugha chafu na kuwakimbia waandishi wa habari
Baada ya timu yake kutupwa nje ya michuano ya Mapinzuzi Cup, kocha wa Azam FC Stewart Hall aligoma kuongea na waandishi nwa habari, badala yake alikuwa akitembea kwa hatua za haraka kuelekea vilipo vyumba vya kubadilishia nguo. Waandishi wa habari bado wakaendelea kumfukuzia wakitaka atoe neno  lakini badala yake kocha huyo uzalendo ulimshinda na kuanza kuporomosha matusi kwa waandishi waliokuwa wakitaka kusikia neno lake baada ya Azam kuyaanga mashindano.
6.Mwamuzi wa pembeni kulikataa goli halali la Mtibwa Sugar
Mwamuzi wa pembeni Dalila Jaffar Mtwana alilikataa goli halali la Mtibwa Sugar lililofungwa na Chiza Kichuya ambalo kama lisingekataliwa lingeipa ushindi Mtibwa Sugar wa magoli 2-1 dhidi ya Azam FC.
Licha ya mwamuzi huyo kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa michuano hiyo, lakini tayari alishaathiri matokeo ya Mtibwa Sugar. Pengine goli hilo lisingekataliwa Mtibwa ingefanikiwa kuongoza kundi lake kuelekea mchezo wa nusu fainali.
  1. Agrey Morris abaniwa kuingia uwanjani na kutakiwa kulipa kiingilio
Beki wa kutumainiwa wa Azam FC na timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ alijikuta kwenye wakati mgumu pale alipokumbana na walinzi wa mlangoni ambao waligoma kumtambua kama mchezaji wa  Azam wala timu ya taifa ya Zanzibar na kumzuia kuingia uwanjani bure wakimtaka alipe kiingilio.
Agrey ni majeruhi hivyo hakuwepo kwenye orodha ya wahezaji wanaounda kikosi cha Azam hivyo kulazimika kukaa jukwaani. Wakati akitaka kupita mlangoni kwenda jukwaa la VIP walinzi walimdai ticket inayomruhusu kwenda kukaa kwenye jukwaa hilo, ndipo akawajibu yeye ni mchezaji wa Azam na timu ya taifa ya Zanzibar lakini bado haikutosha kumfanya apite.
Walinzi hao walimkomalia Agrey hadi akaamua kwenda kulipia ticket na ndipo aliporuhusiwa kupita getini.
  1. ‘Changudoa’ wa Zanzibar awa mwiba kwa wapenda dezo
Unaweza ukashangazwa na jina hili hasa kwenye tasnia ya soka. Huyu ni jamaa ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kwenye mashindano ya Mapinduzi kutokana na uwezo wake wa kuweza kuwazuia watu wote ambao hawakuwa na vitambulisho vya kuwaruhusu kuingia uwanjani au wale ambao huwa wananyatia na kuingia bila tiketi.
Mtandao huu ulishindwa kulipata jina lake kamili mara moja lakini ‘Changudoa’ ni jina ambalo linamtambulisha zaidi visiwani Zanzibar. Jamaa hana masihara anapokuwa getini na kama huna ticket wala kitambulisho basi ujue hakuna namna unaweza kuingia uwanjani kwa kumshawishi.
Huyu ndiye aliyemzuia Naibu Waziri wa Michezo wa Zanzibar kuingia uwanjani kwasababu hakuwa na ticketi wala kitambulisho na pia Agrey Morris alijikuta akikwama kuingia uwanjani hadi alipotakiwa kuonesha tikezti yake.
3. Kiwango cha Ibrahim Jeba chawashika wengi
Kiungo huyo wa Mtibwa Sugar alicheza michuano ya Mapinduzi Cup 2016 kwa kiwango cha juu kiasi cha kuteka mashabiki wengi waliokuwa wakijitokeza kushuhudia michuano hiyo iliyochezwa visiwani Zanzibar.
Licha ya timu yake kushindwa kulichukua kombe la Mapinduzi, Jeba alipiga mpira mwingi na kuwafanya mashabiki wa soka kumjadili kwenye mitaa mbalimbali ya Zanziba. Jamaa mmoja aliandika bango na kulining’iniza kwenye nyumba yake likiwa na ujumbe uliosomeka “ Jeba mkali wa Mapinduzi, Nani kama Jeba?”
  1. Mapinduzi Cup yamponza Kerr
Michuano ya mwaka huu huenda ikawa imeacha kumbukumbu mbaya kwa aliyekuwa kocha mkuu wa Simba pamoja na kocha wa makipa wa timu hiyo Iddi Salim baada ya kufungashishiwa virago kufuatia kuondolewa kwenye michuano hiyo na Mtibwa Sugar kwenye hatua ya nusu fainali.
Baada ya kikosi chake kutupwa nje ya michuano hiyo, kocha huyo aliitwa jijini Dar es Salaam na uongozi wa timu yake na baadaye ikatoka taarifa ya kutimuliwa kwa kocha huyo pamoja na kocha wake wa magolikipa.
  1. Mtibwa yashindwa kutamba kwenye Mapinduzi Cup kwa mara nyingine tena
Mtibwa ilifungwa na URA kwenye mchezo wa fainali ya Mapinduzi Cup kwa magoli 3-1 na kupoteza fainali ya nne kati ya tano ambazo wamecheza kwenye michuano hiyo. Mwaka uliopita Mtibwa ilipoteza mchezo wake wa fainali dhidi ya Simba kwa mikwaju ya penati na kushuhudia kombe likienda Msimbazi.
Wakata miwa hao wa Morogoro wametwaa kombe la Mapinduzi mara moja tu kati ya mara tano walizofanikiwa kucheza fainali ya michuano hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG