Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitaka maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo na Mizani,
Bibi Magdalena Chuwa (kulia) kuhusu sababu zilizomfanya azuie matumizi
ya flow Meter katika kuhakiki kiwango cha mafuta yanayoingia nchini
kupitia bandari ya Dar es salaam wakati alipofanya ziara kwenye badari
hiyo Februari 11, 2016. katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala,Raymound
Mushi. (picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………………………………………..
SERIKALI imeamua kuwasimamisha
kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia leo
ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la
kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka mitano.
Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja
Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye
anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.
Akitangaza uamuzi huo kwenye
kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo (Ijumaa, Februari 12, 2016)
ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm
Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.
“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie
barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki
hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika. Pia
utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.
Waziri Mkuu pia amesema ofisi
yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi ili wafuatilie suala
hilo mara moja na ikithibitika kuwa walihusika hatua rasmi
zitachukuliwa na itathibitika hawakuhusika basi watarudishwa.
Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja.
Jana (Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).
Pia Waziri Mkuu alitembelea
sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko
Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya
mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia
baina ya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.
Katika ziara hiyo ilibainika kuwa
Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye
bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu
kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi
mmoja.
“Jana niliagiza kuwa bomba hilo
ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili kurekebisha mfumo huo. Simamieni
vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.
Tags
HABARI KITAIFA