Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akiongea jambo na Balozi wa Jamhuri
ya Watu wa China, Dkt. Lu Youqing (wa pili kushoto) wakati
alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni
Afisa Ubalozi wa China.
Balozi wa wa Jamhuri ya Watu wa
China, Dkt. Lu Youqing (katikati) akimweleza jambo Afisa Ubalozi wa
China nchini, wakati wa kikao chake na Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo (kulia).
Afisa Ubalozi wa China nchini (wa
kwanza kushoto) akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini Profesa
Sospeter Muhongo wakati wa kikao chake na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa
China nchini, Dkt. Lu Youqing (katikati).
Balozi wa Jamhuri ya Watu wa
China nchini, Dkt. Lu Youqing (wa tatu kushoto), akimweleza jambo Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Wa kwanza kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Utumishi Wizara ya Nishati na Madini,
Lusias Mwenda. Wengine ni ujumbe ulioambatana na Balozi wa China.
………………………………………………………………………………………………………………
Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam,
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China imeitaja nchi ya Tanzania kuwa na nafasi kubwa ya kunufaika na
fedha kiasi cha Dola Bilioni 60 kupitia uwekezaji sekta ya nishati,
fedha zilizoahidiwa kutolewa na nchi hiyo wakati wa Mkutano wa Sita wa
Jukwaa la Ushirikiano baina ya China na Afrika, uliofanyika nchini
Afrika Kusini mwezi Desemba,2015.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar
es Salaam na Balozi wa China nchini, Dkt. Lu Youqing na ujumbe wake
alipokutana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa, China ina imani
kubwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Magufuli kwa namna anavyosimamia masuala mbalimbali nchini, pia Profesa
Sospeter Muhongo kutokana na namna anavyoisimamia sekta ya Nishati na
Madini.
Miongoni mwa Sekta zinazopewa
kipaumbele katika fedha hizo ni pamoja na pamoja na miundombinu, afya,
biashara, uwekezaji na kupunguza umaskini, barani Afrika.
Kutokana na mahusiano mazuri
ambayo yamekuwepo kwa miongo kadhaa baina ya nchi hizo mbili, Balozi
Youqing amemwakikishia Waziri Muhongo kuwa, China itaendeleza
ushirikiano huo kwa kuhakikisha inazishawishi kampuni kubwa na
zilizobobea kitaalamu na kiteknolojia za China, ili ziweze kushirikiana
na Tanzania katika sekta ya nishati, na zaidi katika uzalishaji umeme
kwa kutumia Makaa ya Mawe kutokana na namna ambavyo Wizara inavyokipa
kipaumbele chanzo hicho kuzalisha umeme nchini.
Wakati huo huo, China imesema
itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi Watanzania kusoma
masuala ya mafuta na gesi katika vyuo mbalimbali nchini humo kutokana na
umuhimu wa sekta hiyo na kwamba, China inapenda Tanzania ifanikiwe
katika kuzalisha wataalam wa kutosha katika fani hizo na kuongeza kuwa,
anatambua juhudi zinazofanywa na Waziri Muhongo kuhakikisha wanafunzi
wengi wa kitanzania wanapata fursa ya kusoma masuala ya mafuta na gesi
maeneo mbalimbali Duniani, ikiwemo China.
Aidha, leo tarehe 26 Februari,
2016, Wizara ya Nishati imetangaza nafasi za Masomo kwa wanafunzi wa
Kitanzania kuomba kusoma katika Vyuo vya China katika fani za Mafuta na
Kazi katika ngazi za Shahada ya Uzamili (Masters) na Uzamivu (Phd).
Maelezo zaidi ya kuomba nafasi hizo yanapatikana kupitia tovuti ya
wizara www.mem.go.tz
Tags
HABARI KITAIFA