Kumekuwa na taarifa za upotoshaji
zinasombazwa kwenye mitandao ya kijamii juu ya kutolewa kwa ajira mpya
ya walimu kwa shule za sekondari na msingi kwa mwaka 2015/2016.
Taarifa hizo zinazosambazwa
zinaeleza kwamba walimu wapatao 17,928 wa cheti (Daraja IIIA) , 5,416 wa
Stashahada kwa sekondari na 12,677 kwa shule za mazoezi za vyuo vya
ualimu Tanzania Bara wamepangwa kwa ajili ya kuanza kazi.
Katika taarifa hiyo inawataka
walimu hao waliopangwa kuripoti kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kwa ajili
ya kupangiwa vituo vya kazi na kuanza kazi tarehe 01/04/2016.
Taarifa hizo pia zinaeleza kuwa
walimu ambao hawataripoti ifikapo tarehe 10/04/2016 hawatapokelewa tena
na watakuwa wamepoteza ajira zao.
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inapenda kuchukua nafasi hii kukanusha
taarifa hizo kuwa ni za upotoshaji. Wananchi wanapaswa kuzipuuzia kwani
mpaka sasa bado Serikali haijatoa ajira za walimu kwa mwaka 2015/2016.
Ajira mpya za ualimu zitakapokuwa
tayari zitatangazwa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari na katika
tovuti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambayo ni www.tamisemi.go.tz.
Imetolewa na :
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
11/03/2016
Tags
ELIMU