……………………………………………………………………………………………………
Na Grace Michael
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jaffo amewataka
wakurugenzi wa Halmashauri na Waganga wa Wilaya kuhakikisha wanatoa
elimu ya umuhimu na matumizi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa
watumishi wengine ili waweze kunufaika na huduma hizo.
Mbali na hilo, ameupongeza Mfuko
huo kwa jitihada ambazo umekuwa ukifanya katika kushughulikia changamoto
mbalimbali hususan za huduma za matibabu katika maeneo yote
wanapokutana nazo.
Hayo ameyasema wilayani Kisarawe
wakati akipokea msaada wa magodoro 60 kutoka NHIF ambao ambao
umekabidhiwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo kwa lengo la kusambazwa
katika vituo vya afya ambavyo vina uhitaji mkubwa.
“Katika hili NHIF mmefanya vizuri
sana ….na sio hapa tu, nimekuwa nikipita katika maeneo mbalimbali na
taarifa zenu nakutana nazo kuwa mmekuwa wepesi sana katika kushughulikia
matatizo hasa ya uboreshaji wa huduma za afya pale mnapokutana nayo,”
“Mmeboresha sana huduma zenu kwa
wanachama wenu hasa kwa kupanua wigo wa vituo vya kutolea huduma hatua
inayowawezesha wanachama kupata huduma mahali popote wanapotaka wao…sasa
naomba viongozi wa halmashauri hakikisheni mnawapa elimu watumishi na
wananchi kwa ujumla juu ya huduma hizi za Mfuko,” alisisitiza Naibu
Waziri Jaffo.
Akitoa maelekezo ya mgao wa
magodoro hayo, alimtaka Mganga Mkuu kutoa kipaumbele katika Vituo vya
Afya vya Mwanerumango, Masaki na Mzenga kwa kuwa vina uhitaji mkubwa wa
vifaa hivyo.
Kwa upande wa NHIF, akikabidhi
magodoro hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti Rehani Athumani
alisema kuwa Mfuko ulibaini changamoto ya ukosefu wa magodoro wilayani
humo wakati ilipopita kwa ajili ya ugawaji mashuka hivyo Mfuko
ulidhamiria kuondoa tatizo hilo.
“Tulipita katika vituo mbalimbali
wilayani hapa wakati tunagawa mashuka siku ya sherehe za Uhuru ambapo
Mfuko pia ulishiriki katika kufanya usafi katika vituo hivyo…baada ya
kuona tatizo hilo Uongozi wa Mfuko uliona kuna haja kubwa ya kubana
matumizi katika maeneo mengine kwa lengo la kuwasaidia wananchi,”
alisema Bw. Rehani.
Alisema kuwa jitihada za kubana
matumizi zimeuwezesha Mfuko kutoa misaada ya Magodoro 60 wilayani
Kisarawe, mabati 400 katika zahanati ya Mpingi, Songea Vijijini, Vitanda
20 na magodoro 20 katika kituo cha afya cha Mjimwema mkoani Ruvuma
pamoja na saruji tani tatu katika Shule ya Sekondari ya Kilangalanga.
“Mfuko huu ni wa Watanzania wote
sisi tumepewa dhamana ya kuusimamia hivyo ni lazima twende na kasi
ambayo Rais wetu anaitaka kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania na niseme
tu kwamba Huduma bora za Afya Tanzania inawezekana.
Tags
AFYA