Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mhe. George Masaju amewataka Mawakili wa Serikali kuwa makini na kutoa
ushauri kwa uadilifu na uweledi wa hali ya juu pindi wanapotoa ushauri
wa kisheria kuhusu mikataba mbalimbali.
Mhe. Masaju ameitoa kauli hiyo
alipokuwa akiongea na Mawakili wa Serikali wakati wa ufunguzi wa
mafunzo yanayohusu uhakiki wa mikataba ya ununuzi wa umma leo Mjini
Dodoma.
Alisema ni vyema wakatekeleza
jukumu hilo kwa makini kwani ushauri unaotolewa na Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali kupitia mawakili hao ndio msimamo wa Serikali.
“Ninapenda kuwakumbusha kwamba
ninyi ni watumishi wa umma na mnaongozwa na Sheria ya Utumishi wa Umma
ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2003” alisema Mhe. Masaju
na kuongeza kuwa:
“Kama walivyo watumishi wengine wa umma na kwa msingi huu, ninyi ni sehemu ya Serikali na nafasi yenu katika Serikali ni kubwa”.
Pia aliwataka wanasheria wa
Serikali kujengewa uwezo kuhusu uhakiki wa mikataba na iwapo watashindwa
kutekeleza wajibu huo ipasavyo watawajibishwa kwa kuchukuliwa hatua
stahiki za kinidhamu.
Alisema kuwa kutokana na
kuongezeka kwa thamani ya mikataba inayohakikiwa na wanasheria wa
taasisi ya manunuzi ni wazi kwamba kuna umuhimu wa Maafisa Sheria
kupatiwa mafunzo hayo.
“Wanasheria wa Serikali
wanaohakiki mikataba hii wanawajibika kuzingatia sheria zinazohusiana na
mikataba husika pamoja na maadili ya Wanasheria wa Serikali katika
Utumishi wa Umma kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 27 cha Sheria ya
Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya
mwaka 2005”,alisema Mhe. Masaju.
Mhe. Masaju alishauri utaratibu
wa mikataba yote kuhakikiwa Dar es Salaam ubadilike kwani unasababisha
ongezeko la gharama kwa taasisi za Serikali na kuchelewesha miradi.
Alifafanua kuwa Divisheni ya
Mikataba iko Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pekee
hivyo, mikataba yote ya mikoani ni lazima ipelekwe Dar es Salaam kwa
ajili ya kuhakikiwa.
“Hii inasababisha wadau hasa wa
kwenye Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa, Jiji na wengine walioko
mikoani kusafiri na kupeleka mikataba Dar es Salaam kwa ajili ya
uhakiki” alisema Mhe. Masaju.
Hivyo alisema Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeona umuhimu wa kuwajengea uwezo Mawakili
wa Serikali wa Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali zilizoko Mikoani
ili hatimaye baadhi ya Mikataba kutoka kwa wadau walioko wilayani na
mikoani iwe inapelekwa katika Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali
zilizoko mikoani.
Tags
Bunge