PICHA ZOTE NA ELIPHACE MARWA -MAELEZO
……………………………………………………………………………………………………………
Na Ally Daud- Maelezo.
MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA)
imebakiza Tsh. Trilioni 2.363 ili kufikia lengo waliojiwekea la
kukusanya mapato ya trilioni 12.363 katika mwaka wa fedha 2015/16,
ambapo hadi sasa imekusanya kiasi cha Tsh. Trilioni 10.
Akizungumza katika hafla ya
uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa mafunzo kwa wafanyakazi waliopo
kwenye fursa ya ajira za taasisi hiyo Kamishina Mkuu wa TRA Bw. Alphayo
Kidata alisema taasisi yake imefanikiwa kukusanya kiasi cha sh
trilioni 10 katika muda waliojiwekea na kuahidi kumalizia kiasi cha
shilingi trilioni 2.363 kabla ya mwaka mpya wa fedha wa Serikali
unaoanza mwezi Julai mwaka huu.
“Tumejiwekea malengo ya kukusanya
kiasi cha fedha cha shilingi trilioni 12.363 kwa mwaka huu wa fedha na
tumefanikiwa kukusanya shilingi trilioni 10 mpaka mda huu ila
tunaendelea na kutimiza lengo letu hadi kufikia July mwaka huu na
tutajipanga upya mwaka ujao wa fedha kufikia malengo mapema” alisema Bw.
Kidata.
Aidha Bw. Kidata amesema kuwa kwa
mpango huo wa mafunzo ulioanzishwa kwa kushirikiana na Chuo cha
Usimamizi wa Kodi (ITA) ni mafunzo ya mwaka mmoja yanayoendana na usaili
mpya kwa wahitimu ili kufanya Mamlaka hiyo kuwa na wafanyakazi
waadilifu na wachapa kazi ili kupaisha uchumi nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha
cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo alisema kuwa wameamua
kuanzisha mpango huo kwa kushirikiana na Mamlaka ya mapato ili
kufundisha wafanyakazi wa TRA maadili na nyenzo za utendaji kazini
pamoja na kuendesha mafunzo ya dini ili kuwafanya wafanyakazi wawe
wacha mungu katika kazi zao.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Rasilimali
Watu na Utawala wa TRA Bw. Victor Kimaro aliwataka wafanyakazi wote
wanatakiwa wafanye kazi kwa maadili hususani upande wa ukusanyaji kodi
na Chuo hicho kimewafundisha wafanyakazi hao kufanya kazi kwa ushindani
katika maeneo ya kazi ili kuliletea taifa maendeleo yaliyokusudiwa.
Tags
HABARI KITAIFA