Halmashauri ya Mji wa Kibaha
imeeleza kuwa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi
wa mji huo kwa sasa ni asilimia 56 kupitia miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Halmashauri hiyo.
Akiongea kwa njia ya simu Afisa
Habari wa Halmashauri hiyo Bw. Innocent Byarugaba amesema kuwa
Halmashauri ina jumla ya miradi 11 ya maji ambayo mitano imekamilika na
sita iliyobaki iko katika hatua za mwisho.
“Maji safi na salama yanapatikana
kwa asilimia 56 ikiwa ni juhudi za Halmashauri za kukabiliana na tatizo
la maji na mpaka sasa miradi mitano imekamilika ambayo hutoa huduma ya
maji kwa wananchi,” alisema Bw. Byarugaba.
Katika kuhakikisha huduma ya
upatikanaji wa maji unakuwa bora zaidi, Byarugaba amesema kuwa jitihada
za kukamilisha upatikanaji wa maji unafikia asilimia 100 ambapo
wanaendelea kukamilisha miradi mbalimbali inayofanywa na Halmashauri
hiyo.
Aliongeza kwa kutaja miradi
iliyokamilika kuwa ni pamoja na Mradi wa maji Mtaa wa kwa mfipa Galagaza
kata ya Msangani, Vikawe kata ya Pangani, Sagale kata ya Viziwaziwa,
Zojosa kata ya Misugusugu na Mwanalugali kata ya Tumbi.
Aidha alianisha miradi mingine ya
maji inayotegemewa kukamilika kwa mwaka wa fedha 2016/17 kuwa ni mtaa
wa Sofu kata ya Sofu, Muheza kata ya Mailimoja, Kibenge kata ya
Msangani, Kibugalo kata ya Visiga, Kalabaka kata ya Misugusugu na
Mikongeni kata ya Viziwaziwa.
Bw. Byarugaba alitoa wito kwa
kuwataka wananchi kuwafichua watu wanaokata mabomba ya maji na
kujiunganishia maji kinyemela kwani kwa kufanya hivyo kunapunguza kasi
ya maji na kusababisha watu wengine kukosa maji.
Tags
HABARI KITAIFA