Mjasiriamali kijana Mercy Kitomari akiwa ofisini kwake wakati wa mahojiano.
Modewjiblog ilipata
bahati ya kuzungumza ana kwa ana na Mercy Kitomari mmoja wa
wajasiriamali wanawake vijana ambaye anafikiria kuwa na kiwanda kikubwa
cha ashkrimu (ice cream) ifikapo mwaka 2020 akizisafirisha na kuziuza
Tanzania nzima na Afrika Mashariki. Wapi alipotokea, yuko wapi kwa sasa,
ni machungu gani aliyokumbana nayo na anaishauri nini serikali na
wajasiriamali wenzake. Haya yote utayajua katika mahojiano haya .Soma…
MODEWJI BLOG: Role model wako nani?
MERCY:
Magufuli. You know why?(unajua kwanini?) ametuweka wazi kabisa kwamba
maisha ni changamoto na tusikubali kushindwa ni lazima kupambana na
kufanyakazi kwa bidii na maarifa kuondoa vigingi vyote
vinavyotukwamisha. Amenifanya nifanye kazi kwa bidii. Nataka kuwa
mwanamke anayefanya mabadiliko. Hakuna kitu kinachokuja kirahisi. Nataka
kuwa mwanamke yule ambaye anaonesha tofauti nataka kuifanya nchi yangu
iniringie.
Sijisikii
vibaya kwa kuwa niko mpweke, kitu cha kwanza ni kazi, nataka kuifanya
mwenyewe ili wanawake wenzangu watambue kwamba tunaweza kufanya wenyewe,
bila msaada wa mwanaume. Ndio unahitaji mume lakini si katika hili
suala la ujasiriamali, mwanamke peke yako unaweza kuleta mabadiliko.
Nataka kuwa mwanamke ambaye Afrika itaniringia na taifa langu litanichekelea kwamba mimi ni binti yao.
MODEWJI
BLOG: Turejee katika masuala ya kodi. Kodi ni muhimu sana kwa mapato ya
serikali. Je Kodi zinazowatoza zinawasaidia au zinawavunja moyo?
MERCY:
To be honest (kusema ukweli) zinatuvunja moyo. Nyingi ya hizi kodi
hazitusaidii sisi watu wa hali ya chini kunyanyuka, zinatukwamisha.Kodi
zimewekwa bila kujali madaraja. Anayeanza na aliyemo, mwenye kipato
kidogo na kikubwa. Na yote hayo yanafanyika bila kuzingatia kwamba
kuwapo kwa wajasiriamali wengi ndio kuchangamka kwa soko la wakulima na
pia ajira viwandani.
Mimi
ninayetengeneza ashkrimu natengeneza ajira; ninatengeneza soko kwa yule
anayeleta matunda sokoni kwani naenda kununua matunda kwa ajili ya
ashkrimu. Kodi nyingi zinakandamiza, haziangalii ukubwa na udogo wa
biashara. Mtu anabiashara inayoingiza mamilioni kwa siku anawekwa kundi
moja na anayeingiza laki moja.
Muonekano
wa nje wa duka la Ice Cream la Nelwa’s Gelato la Mercy Kitomari
lililopo ndani ya Petrol Station ya SOPCO barabara ya Morogoro-Magomeni
Mwembechai karibu na kwa Sheikh Yahya.
MODEWJI BLOG: Ukikutakana na role model wako utamuomba nini?
MERCY:
Nikikutana na Magufuli? Kwanza naomba nikutane naye! Nikikutana naye
nitamwambia ofisi zote za huduma kwa wananchi ziwe katika mtandao
(online) watu tuweze kufanya kila kitu katika mtandao. Na Serikali za
mitaa lazima zirejeshe faida kwa wananchi kwa kodi zao.
Wanatakiwa
watufundishe vitu vingi. Watufundishe kuwa wajasiriamali namna ya
kufunga na kuuza bidhaa zetu wasifanye tu shughuli za kukusanya ushuru
na kodi, watuambie namna ya kuendelea mbele ili waendelee kukusanya
ushuru na kodi au hawatakusanya kitu tukikwama.
Ni lazima wawekeze kwa wajasiriamali ili kuwepo na hali bora zaidi.
Ukitazama
soka katika televisheni unaona matangazo mengi ya krisp hapa kwetu wapo
wadada wanaotembeza za ndizi au viazi hawa wakifundishwa namna nzuri ya
kuweka chakula chao ni dhahiri tutakuwa na wajasiriamali wengi.
Wanatakiwa watuelekeze mambo mengi bidhaa za kwenye ‘super market’
zinakuaje na kadhalika wasibaki kudai na kuvuna hela tu watusaidie
tuweze kuwapatia fedha zaidi. Lakini nambieni lini nitakutana na role
model wangu huyu…….ha ha ha ha….kicheko….!
MODEWJI
BLOG: Wasaidizi wake wakisoma makala haya watajua nini unahitaji na
pasi shaka watakukutanisha naye.Ni watu wema hawa, hawawezi kukosa
kukupangia muda wa kumuona Role Model wako umweleze mambo ya kukusaidia
wewe na wengine wa aina yako.
MERCY:
Nakudai hilo kwani natamani sana atukutanishe wanawake vijana
wajasiriamali ili azungumze nasi. Najua ameshazungumza na
wafanyabiashara wakubwa, lakini akituona na sisi atatambua uwezo wetu na
namna ambavyo angetusaidia tungeibuka wengi na kuweka ndoto ya Tanzania
ya viwanda katika ukweli.
You
know (unajua) nilikutana na wanawake wenzetu wajasiriamali kutoka
Uganda na Rwanda naona wameendelea kwelikweli na siri ni serikali zao
kuhakikisha kwamba wanaendelea.
Wapo
wanawake waliokata tamaa hapa, nimekutana nao nikasema tusichoke hata
kidogo serikali ya sasa inataka viwanda ni lazima kuisaidia kujua
tunawezaje kufikia ndoto hiyo, kuna vizingiti hapa wakiviondoa tutaweza.
Hatupaswi kukata tama hasa kutokana na serikali ya sasa kutaka kuwapo na viwanda.
Tags
HABARI KITAIFA