………………………………………………………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
SERIKALI imetangaza utaratibu
mpya utakaofuatwa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
kuanzia Juni 16 hadi 23, 2016 ambapo imewaagiza Watendaji Wakuu katika
Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali kutenga
siku moja ya kukutana na watumishi katika sehemu zao za kazi kwa lengo
la kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, imewaagiza watendaji hao
kutenga siku nyingine moja kwa ajili ya kukutana na wananchi, kusikiliza
na kuzitafutia ufumbuzi kero zao zinazohusiana na huduma zinazotolewa
na Taasisi zao.
Akitangaza utaratibu huo leo
jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma Mhe. Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali imeamua
kubadili mfumo wa maadhimisho hayo kwa lengo la kuongeza ushiriki wa
wananchi na watumishi wa umma katika maadhimisho hayo.
Ameongeza kuwa wakati wa
maadhimisho hayo Watendaji hao watatakiwa kukutana wananchi na
kusikiliza kero zinazohusiana na huduma zinazotolewa na taasisi zao pia
kukutana na watumishi wa umma katika sehemu zao za kazi kusikiliza kwa
lengo la kusikiliza kero zinazowakabili zikiwemo za upandishwaji wa
vyeo, madai mbalimbali na taratibu mbalimbali kuhusu utumishi wa umma.
Amesema kuwa baada ya maadhimisho
hayo kila Wizara, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi ya Umma
itapaswa kuandaa taarifa jinsi ilivyotekeleza maagizo yaliyotolewa kwa
kuiwasilisha Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma kabla ya Juni 30, 2016.
Ameeleza kuwa Tanzania inaungana
na mataifa mengine ya Bara la Afrika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa
Umma Barani Afrika chini ya Kaulimbiu isemayo Uongozi wa Umma kwa
Ukuaji Jumuishi:kuelekea katika Afrika tunayoitaka.
Mhe. Angellah amebainisha kuwa
maadhimisho ya mwaka huu yatajikita katika kuangalia mchango wa Utumishi
wa Umma katika ukuaji wa uchumi Barani Afrika, mchango wa Utumishi wa
Umma katika kuiwezesha Ajenda ya Afrika ya 20163 ambayo inaweka mkazo
katika maendeleo ya Afrika na Haki za Wanawake.
Amesisitiza kuwa malengo na
mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ni kufikia uchumi wa viwanda
uliofungamanishwa na maendeleo ya watu, Tanzania ikiwa imejiwekea
malengo ya kupiga hatua katika ukuaji wa uchumi kupitia maendeleo ya
viwanda.
Amesema ili kufikia azma hiyo
Serikali kupitia Utumishi wa Umma ina wajibu wa kuwawezesha wananchi
kushiriki katika shughuli za uzalishaji ili kukuza uchumi huku watumishi
wa umma wakitakiwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi, kutoa
huduma kwa wananchi wote kwa wakati pasipo urasimu wala ukiritimba pia
kuepuka vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao
Tags
HABARI KITAIFA