WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano Tanzania wameaswa kutumia mifumo ya ufuatiliaji wa fedha za
umma ili kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika
katika malengo yaliyokusudiwa.
Wito huo umetolewa leo mjini
hapa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Colman Titus
Msoka wakati wa semina ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC).
Dkt. Msoka alisema wajibu na
nafasi ya Mbunge katika chombo hicho cha kisheria ni pamoja na suala
zima la kuisimamia Serikali, hivyo aliwataka Wabunge kuhakikisha
wanafuatila matumizi ya fedha za umma kila zinapotengwa na jinsi
zinavyotumika.
“Wekeni mifumo ya ufuatiliaji
wa matumizi ya fedha za umma kwenye majimbo yenu, kaeni pamoja na
wataalamu wawafundishe watu wenu na muombe ufafanuzi wa matumizi hayo
kwa wahusikia ili kuepukana na ubadhirifu wa fedha” alisema Dkt. Msoka.
Kwa upande wake Mtafiti
Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umasikini nchini
(REPOA), Bw. Solomon Baregu alisema ili kuwepo na ufanisi katika
ufuatiliaji na usimamizi wa bajeti ya fedha zinazotengwa na Serikali
kunahitaji kuwepo na sera kabambe zinazoanisha mikakati ya uondoaji wa
umaskini kwa wananchi.
Aliongeza kuwa ufuatiliaji na
usimamizi kupitia sera kutaifanya bajeti kuwa nyenzo ya utengaji wa
rasilimali zitakazosaidia kutimiza malengo yaliyokusudiwa katika
Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) na Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/17- 2020/21 sambamba na Dira ya
Maendeleoya Taifa ya 2025.
Naye Mbunge wa Viti Maalum
(CCM) Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Jacquiline Ngonyani alisema semina hizo
hazina budi kufanyika kabla ya kukamilika kwa bajeti ili kuwapa nafasi
wabunge kuweza kuchangia wakiwa na uelewa wa kutosha.
“Kamati zinapaswa kutembelea
sehemu miradi inapotekelezwa badala ya kusubiri kulalamika wakati miradi
hiyo imeshatekelezwa na kubaini upungufu,” alisema Ngonyani.
Mbunge wa Kasulu (CCM), Daniel
Nsanzugwanko alisema ni wajibu wa wabunge kufuatilia matumizi ya fedha
za umma katika miradi ya serikali ili miradi hiyo iweze kuleta tija mwa
wananchi na taifa kwa ujumla.
Tags
Bunge