Na Baraka Mbolembole
“Sasa mimi sijui nitazungumzia nini, sababu siwezi tena kuendelea na soka. Naenda shule. Majeraha yamezidi kupitiliza.” Baada ya kuzungumza na Salum Telela, Desemba 25, 2012 alijibu hivyo kufuatia kumuuliza kuhusu hatima yake ya kucheza soka kufuatia kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara katika misimu yake miwili ya mwanzo klabuni Yanga ( 2010-2012).
Wakati aliposajiliwa Moro United kama mchezaji wa mkopo mwanzoni mwa msimu wa 2011/12 baada ya kocha Mganda, Sam Timbe kukubali hilo, Telela alipiga mpira wa uhakika katika timu hiyo iliyopata kutamba mwanzoni mwa miaka ya 2000 na haikushangaza aliporudishwa kundini Yanga siku chache baada ya klabu hiyo kumtimua Timbe na kumrejesha Mserbia, Kostadin Papic.
Papic ambaye alipendekeza usajili wa Telela, Omega Seme wakiwa makinda wa timu ya Taifa ya Vijana mwaka 2010. Alijitahidi kuwapa nafasi vijana hao katika kikosi cha kwanza msimu wa 2010/11 lakini majeraha yakaanza kuwaandama kiasi cha kutumia muda mwingi kujiuguza kuliko kuitumikia klabu hiyo. Baada ya Papic kutimuliwa na Timbe kupewa nafasi yake, Telela hakuwa fiti kwa maana alikuwa na majeraha.
Pengine hilo lilimfanya Timbe asimfikirie kwa umakini mchezaji huyo hasa ukizingatia alikuwa na nahodha wa timu, Shadrack Nsajigwa katika nafasi ya beki wa kulia. Kimsingi ndiyo nafasi ambayo Telela ilimtambulisha na kumpa nafasi Serengeti Boys na kusajiliwa Yanga.
Telela ni mchezaji ambaye alisisitiza sana kuhusu ‘kufanya kazi kwa ajili ya Watanzani’ inapotokea majukumu ya kitaifa kwa wachezaji. Kauli zake thabiti za kuhamasisha na kuwakumbusha majukumu yao wachezaji wenzake pengine ndiyo yalikuwa sababu ya kuvaa beji ya unahodha wa timu za Taifa za Vijana.
“Najihisi nimebarikiwa, kwa sababu kipindi kirefu nimekaa nje ya uwanja kutokana na majeraha, lakini nimeaminiwa na kuvumiliwa. Nawashukuru Yanga kwa kunivumilia katika kipindi kigumu nilichopitia.”
Wakati kauli yake ya kuachana na soka na kurejea darasani aliponiambia mwaka 2012 nilijaribu kutafakari mwenyewe na kugundua kwamba ‘ alikuwa amekata kabisa tamaa ya kucheza soka la ushindani.’Nakumbuka nilimtia moyo na kumwambia anapaswa kuachana na uamuzi huo kwasababu alikuwa na kipaji kikubwa ambacho kilifichwa na majeraha.
Nilimsisitiza anapaswa kupambana na kuyashinda majeraha kwa maana kuna wachezaji wengi walio/wanaotamba duniani baada ya kushinda vita ya majeraha. Aalan Shearer ni kati ya nyota hao.
Mei 12, 2015 nilifarijika sana Telela alipozungumza kwa furaha, pia nilimuona ni makini baada ya kuwashukuru mashabiki, wanachama, viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wenzake. ‘Nawashukuru Yanga kwa kunivumilia katika kipindi kigumu.’ Niliipenda sana kauli hii hasa nikikumbuka namna mchezaji huo alivyokuwa katika nyakati ngumu za majeraha ya mara kwa mara.
MISIMU 6 MATAJI ‘LUKUKI’ YANGA, IMETOSHA, LAKINI…
Telela hajapewa heshima inayostahili! “Nimecheza kwa misimu 6 katika timu hii na nimepata mafanikio makubwa ikiwemo ushindi wa mataji ya ligi kuu (2010/11, 2012/13, 2014/15, 2015/16,) nimeshinda Kagame Cup 2011 na 2012, Ngao ya Jamii 2013, 2014, 2015, pia taji moja la FA.”
Telela alitaka tena kuichezea Yanga hata kwa mwaka mmoja zaidi lakini imekuwa ni rahisi sana kwa Mbuyu Twite raia wa Rwanda kupewa nafasi ya kuichezea Yanga kwa msimu wa tano na si Telela kupata mkataba hata wa mwaka mmoja na kuichezea Yanga kwa msimu wa 7.
Nilifarijika sana Hans Van der Pluijm alipopendekeza Mbuyu apewe mkataba mpya na niliamini angefanya hivyo pia kwa mchezaji aliyecheza game zaidi ya 20 katika kikosi kilichoshinda VPL na kufika hatua ya makundi katika michuano ya Shirikisho Afrika mwaka huu.
Msimu wa 2013/14 ambao aliufungua kwa goli la mkwaju wa mbali dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii haukuwa mzuri sana kwa kuwa kutokana na kuandamwa na majeraha. Chini ya Mbrazil, Marcio Maximo (2014/15) alianza kupata nafuu na kupata nafasi ya kucheza katika beki namba 2 lakini akaumia tena.
Hans alivyopewa timu hiyo baada ya Yanga kumtimua Maximo mwishoni mwa mwezi Desemba, 2014 , Telela akageuka kiungo maridadi sana na ushirikiano wake na Haruna Niyonzima katikati ya uwanja ukaifanya Yanga ionekane ikicheza mpira wa kupasiana sana tena wakipanga mashambulizi ya uhakika.
Wakati Hans alipoiongoza Yanga kushinda game kumi mfululizo, Telela alikuwa ni kati ya wachezaji muhimu sana. Ila katika game ambayo Yanga walipoteza ugenini dhidi ya BDF XI ya Botswana katika michuano ya Shirikisho, kisha ule uliofuata dhidi ya Simba katika VPL, kijana Said Juma Makapu ndiye alianza katika nafasi ya Telela na game zote Yanga hawakupata matokeo.
“Mimi siumwi ila mwalimu ameniambia ninashambulia sana. Ameniambia nimtazame yule Makagu anavyocheza. Nimemuomba anipe muda. Ninalazimika kufuata maagizo yake.” alinijibu siku moja nilipomuuliza ni kwanini ameondolewa kikosi cha kwanza ghafla wakati alichangia ushindi wa timu katika game kumi mfululizo.
Siwezi kumuondoa Telela Yanga bila shukrani, kwasababu kushukuru ni jambo la thamani siku zote.
Telela hajafanya makubwa sana akiwa Yanga ila katika game zake mbili za CAF, na 15 za VPL msimu wa 2014/15 nimebaki na magoli yake mawili bora zaidi, Yanga v Coastal Union na Yanga v Platnum FC, halafu kuna lile dhidi ya Azam katika Ngao ya Jamii.
Telela alitaka sana kuendelea kuichezea Yanga na mchango wake msimu uliopita ulikuwa mkubwa sawa na wachezaji wengine, ila SHIKAMOO Hans, unampa mkataba Mbuyu na kumnyima Telela. Sehemu ya moyo wangu inasononeka ila kuna maisha nje ya Yanga na naamini Telela atabaki kuwa mchezaji bora.
Tafadhali, Abo Master Telela usiache soka. Mtaalamu wa pasi na magoli ya video, mtu mwenye nidhamu wewe.
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.
Tags
MICHEZO KITAIFA