Picha na Ally Daud-Maelezo.
——————————————
—
Na Ally Daud-Maelezo
Ugonjwa unaosababishwa na Sumukavu
kwenye Mahindi ya chakula umegundilika katika Wilaya za Chemba na
Kondoa Mkoani Dodoma baada ya kupeleka jopo la Wataalam waliofanya
utafiti na kugundua kuwepo kwa ugonjwa huo.
Akizungumza hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Bi. Ummy Mwalimu amesema kwamba matokeo ya awali ya watafiti
hao imeonyesha kwamba ugonjwa huo umesababishwa na ulaji wa chakula
kilichokuwa na sumukuvu na kuleta madhara.
“Hayo ni matokeo ya awali ya
watafiti wa wizara yangu hivyo basi nasubiri matokeo ya vipimo vya damu
na haja ndogo vilivyopelekwa kwa uchunguzi zaidi katika Maabara ya CDC,
Atlanta iliyopo nchini Marekani na matarajio yetu ni kupata majibu hayo
katika kipindi kisichozidi wiki moja” aliongeza Bi Mwalimu.
Aidha Bi. Mwalimu amesema kwamba
mpaka kufikia tarehe 24 Juni 2016, idadi ya wagonjwa imefikia 32, na
idadi ya vifo imebakia 7. Hii ni baada ya kuongezeka kwa wagonjwa 11
katika kipindi cha wiki moja.
“Hadi jana kulikuwa na jumla ya
wagonjwa 9 ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Dodoma, na 14
wako katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa. Wagonjwa watatu waliolazwa
Hospitali ya Mkoa Dodoma, na wawili waliolazwa Kondoa, bado hali zao ni
tete” aliongeza Bi. Mwalimu.
Pamoja na hayo Bi. Mwalimu alisema
kwamba Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kupunguza
uchafuzi wa sumukuvu katika vyakula, ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo
wa kupima vimelea hivyo katika damu na mkojo miongoni mwa taasisi za
ndani ya nchi.
“ Tutaendelea kutoa matibabu kwa
wananchi walioathirika na Ugonjwa huo, kwenye Hospitali ya Mkoa wa
Dodoma na Hospitali ya Wilaya ya Kondoa ili kudhibiti na kurudisha afya
za wananchi katika kiwango kinachohitajika” aliongeza Bi. Mwalimu
Aidha Bi. Mwalimu ametoa rai kwa
wananchi na wakazi wa Dodoma kwamba wanapaswa kuchambua nafaka
zilizoharibika (zilizooza, kuvunjika, zilizobadilika rangi), kukoboa
mahindi kabla ya kusaga au kuacha kutumia nafaka zitakazoonekana
kuharibika sana ili kuepukana na kiasi kilichozidi sumukavu kwenye
nafaka.
Tags
AFYA