JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba limeagizwa kuwasaka
na kuhakikisha wahusika wote wa matukio ya kuhujumu vipando wanakamatwa
na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa huo ,Omar Khamis
Othman baada ya kuendelea kutokea kwa vitendo vya hujuma katika
mashamba ya baadhi ya wananchi katika Mkoa huo.
Amesema vitendo hivyo ambavyo vinafanywa na watu
wasiojulikana vinachangia umaskini kwa wamiliki wa mashamba jambo ambalo
halikubaliki na kwamba serikali ya Mkoa imelaani vikali kwani
vinakwenda kinyume na Haki za binadamu.
Akizungumza baada ya kukagua mashamba ya mihogo na migomba
yaliyohujumiwa huko Tumbe Wilaya ya Micheweni , ambako mashamba matano
yenye ukubwa wa eka tano likiwemo la Sheha wa Shehia ya Tumbe Magharibi
wamehujumiwa na watu wasiojulikana.
“Vitendo hivi haviwezi kuvumiliwa , hakikisheni kwamba
wahusika wanasakwa na wanakamatwa na kisha kufikishwa katika vyombo vya
sheria ”alisema .
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Michewenia Abeid Juma Ali amesema
hujuma hizo ni za makusudi na zimepangwa na watu waliondaliwa kuhujumu
mali za watu wengine , ambapo amewataka wananchi kutochukua sheria
mikononi mwao.
Amesema pamoja na kwamba hujuma hizo zinaathiri sana juhudi
zoa za kujikomboa na umaskini , ni vyema wananchi kuwasilisha
malalamiko sehemu husika na sio kujichukulia sheria mikononi .
“Hivi ni vitendo ambavyo vinanyesha kama ni vya kupangwa ,
hivyo nawaomba sana wananchi kutochukua sheria mikononi mwao bali
wafikishe malalamiko yao Serikali ili yafanyiwe kazi kwa mujibu wa
sheria ”alisisitiza.
Naye sheha wa Shehia ya Tumbe Magharibi Massoud
Khamis Kirendo amesema kuwa amesikitishwa sana na vitendo hivyo ambavyo
vimefanywa na watu hao wasio julikana.
Tags
HABARI KITAIFA