Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala Mwaluma Msofe akiongea na waandishi wa habari (hawapo
pichani) kuhusu mpango wakunusuru kaya masikini muda mfupi kabla ya
zoezi la ugawaji wa fedha hizo kuanza katika mitaa 74 ya Manispaa hiyo
leo tarehe 09/08/2016 Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wakazi wa mtaa wa
Kimanga- Darajani, Kata ya Kimanga Manispaa ya Ilala wakisubiri zoezi la
ugawaji wa fedha kwa kaya masikini kuanza leo tarehe 09/08/2016 Jijini
Dar es Salaam.
Mmoja wa wanufaika wa Mpango
wakunusuru kaya masikini, Ayubu Kabeta akiongea na waandishi wa habari
(hawapo pichani) muda mfupi baada ya kukabidhiwa fedha za kujikimu leo
tarehe 09/08/2016 Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa
Kimanga- Darajani, Kata ya Kimanga Manispaa ya Ilala, Chacha Mwenge
akiendelea na zoezi la kuhakiki majina ya wanufaika wa mpango wa TASAF
katika mtaa wake leo tarehe 09/08/2016 Jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………………………………………
Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO
Mpango wa kunusuru Kaya masikini
(TASAF) wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala umetoa jumla ya shilingi
milioni 292 kwa ajili ya kusaidia kaya masikini 6115 za wilaya hiyo.
Fedha hizo zimetolewa leo Jijini
Dar es Saalam na Mratibu wa TASAF wa Halmashauri hiyo, Mwaluma Msofe
ambaye amesema kuwa fedha hizo zitagawanywa kwenye mitaa 74 ya
Halmashauri hiyo kwa kuwa ndiyo walengwa wa mpango huo.
Msofe ameongeza kuwa mchakato wa
kuwapata wananchi wenye maisha magumu unafanywa na wananchi wenyewe
katika mtaa husika ambapo baada ya kuwatambua wanathibitishwa mbele ya
mkutano wa mtaa.
“Fedha tunazowapatia wananchi hawa
zimeanza kuonyesha mafanikio kwa kuwa zimesaidia kaya hizo kuanzisha
miradi midogo midogo inayowawezesha kuendeleza maisha yao pia fedha hizo
zimesaidia watoto kupata mahitaji muhimu ya shule hivyo kupelekea
mahudhurio kuongezeka”, alisema Msofe
Mratibu huyo amefafanua kuwa kuna
aina mbili za ruzuku ambazo ni ruzuku ya msingi ambayo kaya masikini
hupewa kwa mtu yeyote anayetambuliwa na mpango huo wakati ruzuku ya
masharti hutegemea na aina ya familia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Kimanga- Darajani, Chacha Mwenge amesema kuwa
anaendelea na kazi ya kusimamia na kuchambua majina ya wahusika kwa kuwa
kuna baadhi ya wananchi waliingizwa katika mpango huo bila kuwa na sifa
kutokana na wananchi hao kutoa taarifa za uongo wakati wa utambuzi.
“Tumegundua kuwa kuna baadhi ya kaya ambazo zimeingia kwenye mpango huu kimakosa kwahiyo tunaen
delea kuzitoa, hadi sasa jumla ya kaya 28 za mtaa wetu tumeshaziondoa kwa sababu ya kukosa sifa”, alisema Mwenge.
Naye mmoja wa wananchi
wanaonufaika na mpango huo, Ayubu Kabeta ameishukuru Serikali kwa
kuwapatia fedha za kujikimu pia ameiomba kuongeza kiwango cha fedha hizo
kwa kuwa kiasi ni kidogo bado hakikidhi huduma muhimu.
Tags
HABARI KITAIFA