Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifunga mkutano wa 14 wa siku mbili
wa Wahandisi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa
Wahandisi Tanzania (ERB) Profesa Ninatubu Lema akizungumza na wahandisi
katika mkutano wa 14 wa siku mbili uliowakutanisha wahandisi wa ndani na
nje ya nchi, jijini Dar es Salaam
Baadhi ya wahandisi wakila kiapo
mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani katika mkutano wa 14 wa Siku ya Wahandisi uliofanyika jijini
Dar es Salaam.
Moja ya washiriki wa maonesho ya
mkutano wa 14 wa Siku ya Wahandisi akipokea cheti kutoka kwa Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani wakati wa
kufunga mkutano huo, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (wa tatu kushoto), akiwa na viongozi
mbalimbali wa taasisi zilizo chini ya Sekta ya Ujenzi katika mkutano wa
14 wa Siku ya Wahandisi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wahandisi wakimsikiliza
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani
(hayupo pichani), katika mkutano wa 14 wa Siku ya Wahandisi uliofanyika
jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………..
Serikali imewataka Mameneja wa
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kutojenga na kuondoa matuta ambayo
yamekuwa kero kwa watumiaji wa usafiri wa vyombo vya moto katika
barabara zote kuu nchini.
Akifunga maadhimisho ya 14 ya
wahandisi nchini, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.
Edwin Ngonyani amesema hakuna sababu ya kuweka matuta endapo madereva
watatii sheria za usalama barabarani.
“Natambua kuwa mkutano huu
umeshirikisha wahandisi kutoka sehemu mbalimbali pamoja na wanataaluma
wengine hivyo zingatieni maelekezo ya kutojenga na kuondoa matuta katika
barabara kuu ili kurahisisha matumizi sahihi na ya kisasa ya barabara”,
amesema Eng. Ngonyani.
Aidha Eng. Ngonyani amewataka
Mameneja wa TANROADS kutumia njia mbadala ya kuweka alama za vivuko vya
waenda kwa miguu (Zebra), na alama za kupunguza mwendo katika barabara
kuu ili kuzuia ajali zinazoepukika.
Naibu Waziri huyo amewataka
Wahandisi wa Halmashauri kuwa mabalozi wa kutoruhusu kuanzishwa vituo
vya biashara katika maeneo ya barabarani na ambayo hayajapangwa na
Halmashauri husika, suala ambalo linahatarisha usalama wa wananchi na
uharibifu wa miundombinu.
“Hakikisheni wananchi hawafanyi
biashara karibu na miundombinu ya barabara kwani kufanya hivyo licha ya
kusababisha ajali pia huongeza msongamano”, amesisitiza Eng. Ngonyani.
Akizungumzia Siku ya Wahandisi
Eng. Ngonyani amewataka wahandisi hao kutumia fursa kuonesha uwezo wao
wa kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuanzisha viwanda na
kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
“Mkumbuke kutekeleza aliyoagiza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kwa
kujihusisha katika utekelezaji wa miradi mikubwa nchini ikiwemo miradi
ya gesi, bomba la mafuta na ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege”,
amefafanua Eng. Ngonyani.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili
wa Wahandisi Tanzania (ERB), Eng. Prof. Ninatubu Lema amemhakikishia
Naibu Waziri huyo kuwa watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuja na mpango mkakati wa
utekelezaji wake.
Zaidi ya Wahandisi 2500
wameshiriki katika maadhimisho ya 14 ya Siku ya wahandisi na kujadiliana
kwa kina namna bora ya utekelezaji wa kauli mbiu ya mwaka huu isemayo
‘Tanzania kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati na kuwa nchi ya viwanda:
Nini jukumu la wahandisi’.
Tags
HABARI KITAIFA