Na Baraka Mbolembole
KUNA mipambano minne ya ‘Kukata na Shoka’ katika muendelezo wa michezo ya ligi kuu Tanzania Bara wikendi hii.
Kwa kuanza nitawachambulia pambano ambalo linamrudisha kocha Mecky Mexime ambaye kwa mara ya kwanza katika historia yake ya mpira atakuwa ‘mpinzani’ dhidi ya ‘timu ya maisha yake.’
Mtibwa Sugar klabu pekee ambayo Mexime alitumia kucheza soka kwa zaidi ya miaka 15 na kushinda mataji mawili ya VPL (1996 na 2000), itampokea ‘mpinzani wanayefahamiana sana’ na shujaa aliyepita wa klabu yao, si mwingine ni Mexime ambaye safari hii anakinoa kikosi cha Kagera Sugar FC.
“Nia yetu ni kushinda game na si kutoruhusu goli. Kama tukipata magoli mawili na wao (Mtibwa) wakipata goli moja siyo mbaya. Lengo letu ni kupata pointi 3 lakini tutajitahidi kuendeleza rekodi yetu ya kutoruhusu goli.” anasema naodha wa Kagera Sugar, George Kavila nilipofanya mahojiano naye Alhamis hii.
Kagera haijaruhusu goli lolote katika michezo yao minne ya mwanzo na watakwenda Manungu Complex, siku ya Jumamosi wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa 1-0 Oktoba, 2015. Said Bahanunzi ndiye aliyeizamisha Kagera wakati huo ikiwa chini ya Mbwana Makatta.
Safari hii, Mecky ameimarisha ukuta wake akiwapanga wachezaji watano mbele ya golikipa, Hussein Shariff.
Mwaita Salehe amechukua nafasi iliyoachwa na Salum Kanoni katika beki mbili, Juma Jabu ameshikilia upande wa beki 3, huku vijana Ramadhani Shemvuni, Erick Kyaruz na nahodha-mzuoefu, George Kavila wakikamilisha ukuta wa kati (namba 4, 5 na 6).
Kocha wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga hafurahishwi na namna safu yake ya ulinzi inavyocheza. Mayanga hakupoteza mchezo wowote kati ya 15 katika uwanja wa nyumbani msimu uliopita alipokuwa kocha wa Tanzania Prisons lakini msimu huu tayari amepoteza mchezo katika uwanja wake wa nyumbani huku safu yake ya ulinzi ikiruhusu magoli matano katika michezo minne.
Rashid Mandawa amekwisha funga magoli mawili na atawavaa Kagera timu ambayo ilimtambulisha vyema kiuchezaji msimu wa 2014/15. Haroun Chanongo, Ally Yusuph na kijana mwingine, Stamili Mbonde wataungana na Ibrahim Juma ‘Jeba’ kujaribu kumshinda Mecky na safu yake ngumu ya ulinzi.
Kitendo cha safu ya ushambuliaji kufunga magoli manne hadi sasa ni ishara kwamba katika idara hiyo Mayanga amekuwa na matumaini huku kiungo kikiongozwa vyema na nahodha, Shaaban Nditti.
Mechi hii si tu kwamba inazikutanisha timu zinazojuana, ama makocha wanaofahamiana, bali hadi wachezaji wanajuana vizuri kiuchezaji. Licha ya kwamba Kagera wapo juu ya Mtibwa katika msimamo, safu yao ya ushambuliaji imefunga goli moja tu katika ligi.
Kwa maana hiyo, Mecky anakabiliwa na tatizo kubwa sana-ufungaji na hilo ndilo linaweza kumuangusha kuifunga timu yake ya zamani. Mtibwa wanafunga lakini wanaruhusu magoli kwa wingi, Kagera hawafungi lakini ni wagumu kufungika.
Tags
MICHEZO KITAIFA