RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imedhamiria kwa makusudi kuitilia
mkazo na kuiimarisha sekta ya uwekezaji ambayo matunda yake yatawasaidia
wananchi wote wa Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo leo
alipofanya mahojiano na waaandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali
mara baada ya kumaliza ziara yake ya kuitembelea miradi ya Kampuni ya
Bakhresa ikiwemo ujenzi wa nyumba huko Fumba pamoja na ujenzi wa hoteli
ya kisasa huko Mtoni mjini Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa mradi
mkubwa wa ujenzi wa nyumba za kisasa huko Fumba utasaidia kwa kiasi
kikubwa kutokana na Serikali kuweza kupata pato sambamba na wananchi wa
Fumba na maeneo jirani kuweza kupata ajira.
“Fumba ilikuwa imefumba lakini
hivi sasa itafumbuka kwani kukamilika kwa mradi huu Fumba itakuwa ni
sehemu ya pekee katika kukuza uchumi wetu pamoja na kuwasaidia wananchi
wote kutokana na pato litakalopatikana katika maradi huo”,alisema Dk.
Shein.
Alisema kuwa matarajio ya ujenzi
huo ambao kwa maelezo ya uongozi wa Kampuni hiyo, eneo hilo litakuwa ni
Dubai ya Zanzibar linatoa matumaini makubwa katika kuuimarisha uchumi wa
Zanzibar, ambapo mradi huo utajulikana kwa jina la ‘Uptown Living’.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa
nchi nyingi duniani ziliazia na miradi kama hiyo ambazo zilikuwa ni
masikini kuliko Zanzibar lakini hivi sasa zimeweza kupiga hatua kubwa na
kuwa nchi tajiri kutokana na kuwepo miradi kama hiyo na kueleza kuwa
kinachofanywa na serikali katika suala zima la uwekezaji ni tija kwa
wananchi wote,
Kutokana na juhudi hizo Dk. Shein
alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kuheshimu na kufuata taratibu zote
zilizowekwa na Serikali juu ya suala zima la matumizi ya ardhi.
Katika maelezo yake Dk. Shein
alisikitishwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuvunja sheria na taratibu
zilizowekwa juu ya umili wa ardhi huku wakitambua kuwa ardhi ni mali ya
serikali hivyo kila mmoja ana jukumu la kuilinda na kuitunza ardhi
iliopo.
Kwa upande changamoto ya ajira
kwa vijana wa Zanzibar hasa katika sekta ya utalii, Dk. Shein alieleza
kuwa jambo muhimu ambalo litawapa vijana wa Zanzibar kuajiriwa kwa
haraka katika sekta hiyo ni kuwa na elimu ya fani hiyo.
Alisema kuwa suala la elimu ni
muhimu sana na kutoa wito kwa vijana wa Zanzibar kujikita zaidi katika
kujitafuatia elimu na ndio maana Serikali anayoiongoza imeweza kutilia
mkazo suala hilo kwa kukiimarisha Chuo chake cha Huduma za Watalii
kiliopo Maruhubi kwa kutoa mafunzo ya Cheti, Diploma huku kukiwa na
mchakato wa kukiingiza kuwa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar (SUZA).
Dk. Shein alisisitiza kuwa iwapo
vijana watakuwa na elimu ya kutosha suala la upendeleo halitochukua
nafasi huku akitoa inzari umuhimu wa elimu kwa hi sasa kwa vijana hao
hasa katika ushindani wa ajira katika soko la Afrika Mashariki.
Mapema Dk. Shein alipata nafasi
kutembelea mradi ya nyumba za kisasa zinazojengwa na Kampuni ya Bakhresa
huko Fumba akiwa na mwenyeji wake Said Salim Bakhresa na kupata maelezo
juu ya uendelezaji wa mradi huo utakaojenwga nyumba 600 ambapo awamu ya
kwanza ni wa nyumba 92 za kisasa zinazoendelea kujengwa ambazo zitakuwa
kwa ajili ya wananchi wenye kipato cha juu na kipato cha kati.
Mradi huo ambao mbali ya nyumba
utakuwa na eneo maalum la bustani kwa ajili ya wananchi, bandari ambayo
itawasafirisha wakaazi wa eneo hilo kutoka eneo hilo hadi Dar-es-Salaa
kwa boti maalum zitakazokuwepo eneo hilo huku uongozi huo ukieleza hatua
zitakazochukuliwa katika kuhakikisha suala ziama la ulinzi na usalama
linaimarishwa.
Pia, Dk. Shein alipata fursa ya
kuangalia mtambo wa kisasa wa kupikia lami unaomilikiwa na Kampuni hiyo
ya Bakhresa na baadae kukagua barabara itakayotoka eneo hilo hadi uwanja
wa ndege.
Ziara ya Dk. Shein ilimalizia
huko Mtoni nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambapo alijionea ujenzi wa
hoteli hiyo itakayokuwa na sifa ya kimazingira ‘Eco Friend’ ambayo
inajengwa kwa umiliki wa Kampuni hiyo ambayo inatarajiwa itakuwa ni ya
pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mkuu wa
ujenzi wa mradi huo Salim Aziz, alisema kuwa hoteli hiyo itajitosheleza
kwa huduma za maji na umeme na kupunguza gharama katika matumizi hayo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein
alitembela eneo la bahari kuona shughuli za ufukiaji bahari ‘Land
Reclamation’ lenye ukubwa wa heka 4 ambalo ni eneo la hoteli hiyo
linalotarajiwa kuwa na maegesho ya meli ndogo na meli kubwa, huduma za
bustani ya maji ambayo inajumuisha michezo ya kila aina itakayochezwa na
wananchi pamoja na watalii.
Akimalizia Ziara yake, Dk. Shein
alitembelea Gofu la Mtoni ‘Mtoni Palace Ruins’ na kupata maelezo ya
kihistoria na hatimae alipata mapumziko yalioambatana na burudani
mwanana kutoka kikundi cha Rahatul-zaman na kutumbuizwa kwa nyimbo
zilizoibwa na Kitukuu cha Siti Bint Saada pamoja na mpiga Ganon maarufu
Zanzibar Nasor Mohamed hapo katika mkahawa wa hoteli hiyo.
Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein alifuatana na viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Tags
HABARI KITAIFA