Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Theresia Mmbando
…………………………………………………………………………
Na. Abushehe Nondo & Frank Shija
MAELEZO Dar es Salaam.
JUMLA ya kaya 26,248 zimenufaika
na mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III) kwa kupatiwa jumla ya
shilingi Bilioni 6.6 katika mkoa wa Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa na Katibu
Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Theresia Mmbando wakati akiongea na
waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
Mmbando amesema kuwa utambuzi wa
kaya maskini ulianza mwezi Januari 2015 kwa kushirikisha wilaya za
Kinondoni, Temeke na Ilala ambapo jumla ya kaya 26,248 zilizoandikishwa
na kupokea ruzuku kila baada ya miezi miwili kwa kuzingatia mzunguko wa
malipo.
Aliongeza kuwa wanufaika wa mpango
huo wamepatikana kutokana na ushirikishwaji wa jamii husika ambapo
jamii yenyewe ilibainisha majina ya walengwa katika maeneo yao.
Aidha Mmbando amesema kuwa pamoja
na mafanikio hayo kuna baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika
kutekeleza mpango huo ikiwemo baadhi ya kaya zilizokidhi vigezo kukataa
kuandikishwa, kuandikishwa kwa kaya zisizokuwa na sifa, pamoja na
kupokea ruzuku pungufu.
Katika kukabiliana na changamoto
hizo, Mmbando amesema mpaka sasa jumla ya kaya 609 zimeondolewa katika
kwenye mpango huo ikiwemo kaya 141 (Ilala), kaya 296 (Kinondoni) na kaya
172 (Temeke).
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF
Mkoa wa Dar es Salaam, Esterine Sephania amesema kuwa suala la
udanganyifu wa kuandikishwa kwa walengwa wasiokuwa na sifa linaanzia
katika ngazi ya serikali za mitaa ambapo huko ndiko wanaleta majina.
Aliongeza kuwa kutokana na
udanganyifu uliojitokeza katika zoezi hilo takribani shilingi milioni
2.2 zimepotea kupitia udanganyifu uliotokana na uandikishwaji kwa watu
wasiokuwa na vigezo.
Tags
HABARI KITAIFA