Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Yusuf Manji, leo October 21 amekutana na waandishi wa habari kuzungumza mambo kadhaa kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa dharura unaotarajiwa kufanyika Jumapili October 23 kwenye uwanja wa Kaunda yalipo makao makuu ya klabu hiyo.
Manji amesema, wanachama hai wote wajitokeze kwenye mkutano huo na kutoa hoja zao kuelekea mabadiliko ya uendeshaji ya klabu hiyo bila kujali kama wanaunga mkono au hawaungi mkono kwa sababu mwisho wa yote zitapigwa kura ili kujua hatima ya klabu hiyo kama itakodishwa au la.
“Napeleka ujumbe kwa wana Yanga, tulieni kikao chenu kitafanyika Jumapili taratibu zote zimefatwa, maandalizi ni ya kutosha. Wale wenye mawazo mbadala wasiogope kufika kwenye kikao, Yanga si ya mtu mmoja Yanga ni ya watu wote maamuzi tutakayofanya Jumapili yatakuwa ni ya wote. Hakuna mtu atakayeshambuliwa, ulinzi utakuwa ni wa kutosha hakuna mtu atakayeshambuliwa kwa hiyo hakuna haja ya kuogopa,” amesema Manji ambaye anataka kutodishwa klabu ya Yanga pamoja na nembo kwa kipindi cha miaka 10.
“Mwenye fikra tofauti na yale yatakayofanyika aje na hoja zake kutakuwa na uhuru wa kuongea, kama mawazo yake yatakuwa bora atatusaidia. Kutakuwa na nafasi ya kupiga kura kuunga mkono au kutounga mkono wote watapiga kura ili kujua hatima ya Yanga yetu ni nini.”
“Sio vizuri watu kwenda maelezo kuongea na kushawishi wakati wanao uhuru wa kuja kwenye vikao vya wanachama kuelezana na kushauriana hata kama kuna tofauti mwisho wa siku tutapiga kura. Tukijenga hoja kupitia vyombo vya habari haisaidii.”
“Yanga ilikuwepo kabla yangu na itakuwepo baada ya mimi, ni klabu maarufu sana inaheshima ndani ya jamii. Sio heshima kwa watu walioijenga kuogopa kikao, kikao ni haki ya kila mwana Yanga.”
“Jumapili nitaamua baada ya kusikia maamuzi ya wanachama wa Yanga. Mimi sifukuzi mtu ambaye hastahili kufukuzwa utaratibu wa Yanga ni Mwenyekiti anayo mamlaka ya kusimamisha na kupeleka kwenye kamati ya maadili kikao cha wanachama ndiyo chenye mamlaka ya kumfukuza mtu.”
Tags
MICHEZO KITAIFA