Na Baraka Mbolembole
“Napenda sana kufunga mabao, kuwapita mabeki wote hata kipa. Si sababu ya umahiri wangu, ila hii ndiyo tabia yangu.” aliwahi kusema mshambuliaji nyota wa zamani wa Brazil, Ronaldo De Lima.
Hakika kila mshambuliaji anapenda kufunga magoli. Katika soka mafanikio ya timu ni muhimu zaidi kuliko mafanikio binafsi ya mchezaji.
Siku zote nitaamini kati ya makosa makubwa yaliyofanywa na klabu ya Simba SC ni kumuacha ‘kimajungu’ mshambulizi raia wa Uganda, Hamis Kiiza na kutumia kitita kikubwa cha pesa kumsaini, Mrundi, Mavugo.
Kuna wakati niliandika kwamba, mpango wa kumsaini, Shiza Kichuya ulipaswa kuhakikisha, Kizza anabaki kikosini na wawili hao (Kiiza na Kichuya) walipaswa kucheza pamoja kijana Ibrahim Ajibu katika safu ya mashambulizi.
Uwezo wa Kiiza tayari ulikuwa machoni mwetu. Achana na magoli yake 19 aliyoifungia Simba katika ligi kuu msimu uliopita na mengine manne aliyofunga katika michuano ya FA, Mganda huyo ni ‘mmaliziaji wa hatari’ huku njaa yake ya kufunga ikichangia makali yake.
Nilishangaa sana alipoachwa kwa sababu zisizo za kimpira na kusainiwa Mavugo ambaye ni mchezaji wa kawaida sana na amepitwa mbali kiuwezo na Kiiza.
Simba haitashinda ubingwa msimu huu na kitakachowaangusha ni safu yao mashambulizi. Mavugo alifunga goli katika mchezo wake wa kwanza wa VPL vs Ndanda SC, akafunga tena vs Ruvu Shooting kisha Mtibwa Sugar.
Baada ya hapo hajafanikiwa tena kufunga. Alicheza kwa kiwango chini vs Majimaji FC kisha Yanga SC. Uchezaji wake wa kibinafsi umechangia kwa kiasi kikubwa mchezaji huyo kushindwa kupata magoli ya kutosha.
Kitendo cha kuwekwa benchi katika mchezo wa Jumatano vs Mbeya City FC ni dalili zinazoashiria kuanza kupoteza imani kwa benchi la ufundi.
Mara kadhaa wakufunzi wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog na msaidizi wake, Mganda, Jackson Mayanja walikuwa wakisisitiza kuhusu ushirikiano wa wachezaji wote katika timu lakini zaidi walimtaka Mavugo kuachana na mchezo wake wa kibinafsi ambao wakati mwingine alikuwa ‘akishuti’ mpira katika mazingira ambayo alipaswa kutoa pasi kwa mchezaji mwenzake.
Ajibu pia alikuwa ‘mchoyo’ katika michezo ya mwanzo lakini haraka amebadilika. ‘Mavugo hatafikisha nusu ya magoli 19’ aliyofunga Kiiza msimu uliopita.
Bila ubishi, Mavugo ni mchezaji bora katika ligi ya Burundi, lakini katika ligi ya Bara mchezaji huyo ataendelea kuonekana wa kawaida sana na hilo litakuwa mtihani kwa wakufunzi wake kumtumia ili timu ipate matunda.
Simba wamefunga magoli 15 katika mechi 8, si haba lakini magoli mengi yamefungwa na mchezaji ambaye hakusajiliwa kutimiza hilo. Magoli 6 katika mechi 8 yaliyofungwa na Kichuya ndiyo yameibeba zaidi timu hiyo.
Sifikirii kama mshambuliaji huyo wa pembeni ataendelea kufunga katika kila mchezo. Mavugo alisajiliwa ili kuchukua nafasi ya Kiiza, na kama ataendelea kuonesha kiwango cha chini timu hiyo haitashinda ubingwa msimu huu. Naamini hivyo.
Jamal Mnyate amefunga magoli mawili, Ajibu amefanikiwa kufunga magoli manne, ukichanganya na yale tisa yalifungwa na Kichuya na Mavugo utagundua kwamba wanne hao wamefunga jumla ya magoli 15 na ndiyo idadi ya magoli yote ya Simba hadi sasa. Viungo hawafungi, na hilo ni tatizo.
Baada ya kuwekwa benchi vs City na kiwango chake cha chini katika michezo miwili ya mwisho aliyocheza, bila shaka presha itaanza kuwa kubwa kwa Mavungo. Simba ilimuhitaji zaidi Kiiza kuliko Mavugo, kama waliweka malengo ya kushinda taji msimu huu kwa kumtegemea Mrundi hilo wasahau.
Ajibu hatatosha, Mnyate si mfungaji wa mara kwa mara na Kichuya hatafunga katika kila mchezo, mbaya zaidi timu haina wafungaji wengine hadi sasa zaidi ya wanne hao.
Nadhani, Ame Ally atakuwa mfungaji mzuri zaidi ya Mavugo kama ataendelea kufanya jitihada na kupewa nafasi. Simba SC wanajidanganya kumtegemea Mavugo kushinda VPL…
Tags
MICHEZO KITAIFA