Na Joseph Sabinus, Nottingham University
……………………………………….
JUZI niliandika makala kuonesha
kuwa kelele zinazoendelea kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari
ukizitazama kwa undani utakubaliana nami kuwa ni matokeo ya kada
isiyojiamini.
Tasnia ya habari hapo nchini
haijiamini na hili linaweza kuelezwa ama na miaka mingi ya kuhangaika
kuwa na sheria yao huku zoezi hilo kila mara likikumbwa na sababu
mbalimbali na kuahirishwa au kwa namna wanavyojenga hoja zao.
Hata hivyo ukiziacha kelele hizo
na kuanza kuusoma muswada huu kwa kina na kwa kutafakari makosa mengi
yanayofanywa na vyombo vya habari popote duniani utakubaliana nami kuwa
muswada huu, kama walivyosema pia Tanganyika Law Society na Twaweza, una
mambo mengi mazuri na ni bora zaidi kuliko ile ya awali.
Nilidhani wanahabari wangeshiriki
vyema katika kuboresha yale maeneo yenye changamoto badala ya kuwaachia
watu wa tasnia nyingine. Ni bahati mbaya wadau hawa wamechagua kuwa
wanaharakati zaidi badala ya wanataaluma.
Binafsi baada ya kuusoma muswada nimebaini masuala makubwa yafuatayo katika hili. Naomba tushirikiane.
- Sheria kutosajili mitandao
Awali nilipomsoma Mbunge Zitto
Kabwe nilistushwa kusikia kuwa sheria hii inalenga kubana hadi mitandao
ya kijamii. Hata hivyo sheria haisomwi kama gazeti.
Wakati Zitto alikuwa akisoma
tafsiri ya neno “media” na kuona limejumuisha mpaka mitandao ya kijamii,
ukweli ni kwamba ukiusoma muswada ule eneo ambalo sheria itahusika nalo
kwa maana ya uratibu ni sekta iitwayo “print media”
Kwa hiyo ni kujidanganya kusema
sheria hii itasajili mitandao ya kijamii na vitu vinavyofanana na hivyo.
Badala yake ukisoma kifungu cha 8(1) unauona ukweli huu.
- Habari ni taaluma
Kwangu mimi, sijui kwa wanahabari
wenyewe, muswada huu unaleta kwa mara ya kwanza mfumo madhubuti wa
kuifanya sekta ya habari kuwa taaluma kamili na itakayoheshimika na
kutambuliwa zaidi.
Ukiutazama mfumo unaopendekezwa wa
Bodi ya Ithibati katika ibara ya 10 utaiona “spirit” hii. Taaluma kuwa
taaluma moja ya sifa ni hii. Lazima wanataaluma hiyo wawe na Bodi
inayowasajili kwa viwango vilivyowekwa. Hata hivyo sijapata sababu kwa
nini sifa hazijaanishwa kwa sasa.
- Bodi kumilikiwa na wanahabari
Wakati nikiendelea kuusoma muswada
huu pia nilipatwa na wasiwasi kuhusu kuundwa kwa Bodi hiyo ya Ithibati
nikidhani ingejaa warasimu tunaowafahamu siku zote.
Hata hivyo kama kuna jambo lingine
la kuusifu muswada huu ni pamoja na muundo wa Bodi yake. Bodi itakuwa
na wajumbe 7 na kati ya hao wanne (4) watakuwa ni wanataaluma ya habari
akiwemo mwenyekiti wa Bodi.
Haya ni mapinduzi makubwa katika
uundaji wa Bodi za kitaaluma ambapo katika maeneo mengine ingezingatiwa
tu uwakilishi labda wa jinsi, umri au taasisi. Katika hili tuwapongeze
waliosanifu muundo wa Bodi hii.
- Bara Huru lenye meno
Hapa nianze kwa kusema muswada huu
umechelewa sana na hakuna hoja wala haja ya kusubiri tena. Wananchi
wanahitaji kuhudumiwa na sekta bora zaidi ya habari na kila mmoja wetu
anajua umuhimu huu.
Ukisoma kifungu cha 23 na
kuangalia majukumu yale ya Baraza Huru la Habari utakubaliana nami kuwa
tunahitaji Baraza hili Huru kuliko wakati wowote. Hilo Baraza
linalotajwa kuwepo ni NGO tu na Serikali yoyote duniani haiwezi
kuendeshwa na NGO.
Baraza linaloundwa humu nimeona
litakuwa na uhuru na haki ya kutunga kanuni za maadili za wanahabari na
kuhakikisha wenyewe wanazielewa katika kuwasimamia kwenye kazi zao. Hii
ni muhimu sana.
Ukienda Mahakamani inachukua
miaka. Ukienda MCT ya sasa hata wakitoa uamuzi chombo cha habari
kinakuwa na uhuru wa kuukataa au kuukubali uamuzi huo. Baraza hili kwa
kuwa limeanzishwa kisheria na lina nguvu za kisheria litakuwa na uwezo
wa kusimamia hata utekelezaji wa hukumu zake.
- Wanahabari kutunga kanuni zao
Katika hili niseme tu kwamba kama
kuna jambo wanahabari wamekuwa wakilikosa kwa muda sasa ni kwanza kuwa
na chombo kimoja kinachowaunganisha bila kuwabagua zaidi ya wao tu kuwa
wanahabari.
Katika Baraza linaloanzishwa
nimeona vifungu kuwa litakuwa na kazi nyingine muhimu na ya kipekee
(exclussive rights) ya kuandaa kanuni za maadili (media code of ethics).
Hii ni muhimu kwa sababu badala ya kutungiwa na watu wengine ni
wanahabari wenyewe watakaozitunga kwa sababu pia wanafahamu vyema kazi
yao.
- Kamati ya malalamiko
Kumekuwa na fikra miongoni mwa
watu kuwa kuipata haki mahakamani ni gharama kubwa sana na inayochukua
muda mrefu. Katikati ya keleleza za baadhi ya watu kuwa sheria hii haina
jema, ni muhimu kuona umuhimu wa kifungu hiki.
Kwa kuanzishwa Kamati ya
Malalamiko chini ya Baraza Huru la Habari, sasa wananchi watapata pa
kulalamikia na tena penye meno. Lazima tukubali kuwa ama kwa ajenda
fulani au makosa ya kibinadamu, vyombo vya habari nchini vinawakosea
sana watu binafsi au taasisi.
Naamini ni vyema kuwapa wahusika
mahala pa kulalamika kwa sababu kwenda Mahakamani ni suala ambalo kila
mmoja, kwa sababu tulizokwishaeleza, asingependa kulichagua. Kamati hii
basi ikiundwa itoe uamuzi kwa haraka na iwe madhubuti.
- Bima ya Afya
Mwezi Novemba mwaka jana nilirejea
nchini kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka. Katika pita pita zangu jijini
Dar es Salaam nilikutana na matukio mawili ya wanahabari kuchangiwa na
wenzao.
Nilipofuatilia suala hili
nikaambiwa kuwa wanahabari hao hawakuwa na bima na walipopatwa na
maradhi ya muda mrefu ikawalazimu kuishi na kupata tiba kupitia michango
ya kujitolea ya wanataaluma wenzao.
Wapo pia waandishi ambao hadi sasa
wako hai lakini wanaishi kwa kutegemea misaada ya ndugu na jamaa kwa
ajili ya kupata huduma za afya. Nauona muswada huu unakuja kuwakomboa
wanahabari. Ni muswada unaokuja kuhakikisha kuwa si tu wanataaluma hii
wanafanya kazi zao kwa ufasaha lakini pia waweze kupata haki yao ya
matibabu na kuwekewa hifadhi ya jamii.
Iliniuma na leo tunapoona katika
kifungu cha 58 cha muswada huu kuna ulazima kwa wamiliki wa vyombo vya
habari kuwakatia bima watu wao, inashangaza kuona wapo wanahabari ambao
wanadai muswada huu haufai na kutaka urejeshwe nyuma.
- Haki za watu
Ukisoma Tamko la Haki za Binadamu
la 1948 utaona msingi wa haki kuwa umebebwa katika dhana ya haki ya mtu
mmoja hukoma pale utekelezaji wa haki hiyo unapoingilia uhuru au haki ya
mtu mwingine.
Nimeviona vifungu kadhaa vya
muswada huu vikiwa na mlengo huu wa kuhakikisha wakati, kwa mfano, haki
ya wanahabari kukusanya na kusambaza habari ikiwa ni muhimu, pia ziko
haki za watu wengine zinazopaswa kulindwa na wanahabari.
Kifungu cha 32 katika hili kwa
mfano kinaainisha au kukataza waandishi kuchapisha kashifa na
kuwashushia watu wengine hadhi zao bila sababu (wawe hai au wamekufa).
Hii ni muhimu sana.
- Usalama wa Nchi
Nikikumbuka jinsi vyombo vya
habari vilivyochangia katika machafuko katika nchi mbalimbali duniani
hasa Rwanda (1994) na Kenya (2007) nashawishika kuchekelea ninapousoma
muswada huu.
Ukiacha vifungu vinavyoainisha
uchochezi, nimeguswa zaidi na kifungu cha 55 cha Sheria kinapompa
mamlaka Waziri akijiridhisha kuwa kuna suala linalokwenda kukiuka
usalama wa nchi basi achukue hatua haraka.
Wanaharakati hupinga vifungu kama
hivi kwa hoja za juu juu tu za kutokuwaamini viongozi wanaoweza kupewa
madaraka hayo, lakini uhalisi kwamba mambo haya yameshatokea na kwamba
zipo nchi zimeshawahi kuingia katika umwagaji wa damu kwa vyombo vya
habari kuachwa huru watakavyo, mtu hawezi kubeza kuwekwa kwa vifungu
kama hivi.
Lipo pia kosa la uchochezi ambalo
wengi, bila kulitafakari, wanapiga kelele zilizokosa tafakuri. Unawezaje
kuwaacha watu watumie vyombo vya habari kuchochea vurugu, kuhamaisha
uasi na machafuko katika nchi? Kwangu mimi makosa kama haya ni muhimu
kwa usalama wa nchi na ni juu ya kila mmoja kutekeleza sheria.
- Kufutwa sheria ya Magazeti
Mimi nikiwa hapo nyumbani kwa
miaka mingi nimekisikia kilio cha wadau dhidi ya Sheria ya Magazeti,
1976. Sheria hii tumekua nayo, tumeishi nayo na tulianza kuzeeka nayo
lakini kila mwanataaluma akijua haikuwa sheria nzuri.
Kwamba leo inafutwa ni faraja kwa
tasnia na nilidhani wenzetu wengine badala ya kulaani jambo hili
wangeungana nasi kulishangilia. Kwangu, kama kuna jambo jingine kubwa
kwa wanatasnia kulishangilia ni kufutwa kwa sheria hii ambayo wengine
walifikia hatua ya kuiita “ya kikatili.”
Wakati nikiamini wabunge watakuwa
wamefanyiakazi changamoto nyingine na kuuboresha muswada katika maeneo
machache kama vile kukamatwa mitambo kabla ya uamuzi wa mahakama na
kuainishwa viwango vya taaluma, niwaase wanahabri nchi kuwa katika
ulimwengu wa utatuzi wa migogoro; mazungumzo ni muhimu.
Ni bahati mbaya kwamba katika hili
walichagua kutozungumza na Kamati ya Bunge na wakasusia na hatimaye
muswada huu ukipita utawahusu hata kama wao hawakushiriki kuutunga.
*Mwandishi wa makala haya
amejitambulisha kuwa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) kwenye
Chuo Kikuu cha Nottingham, Uingereza.
Tags
HABARI KITAIFA