Inawezekana kabisa mchezaji Cristiano Ronaldo akawa ndiye mchezaji wa soka anayeongoza kwa kutengeneza pesa nyingi katika mikataba ya kibiashara na umaarufu katika mitandao ya kijamii.
Lakini usimwondoe katika akili yako mchezaji Neymar Dos Santos Jr. Neymar anakumbukwa kwa kununua boti ya kifahari kuliko mchezaji yoyote yule akiwa bado yupo katika klabu ya Santos yaani kabla hajaanza kuifunga Madrid na vilabu vingine vikubwa.
Pamoja na umri wake mdogo anabaki kuwa mchezaji wa kizazi chake anayeishi Uronaldo na pengine unaweza kuwa sahihi kuamini kuwa anaweza kuja kufanya amkubwa zaidi hapo baadae.
Neymar anakaribia kusaini mkataba wa muda mrefu ndani ya Barcelona huku
akionekana kuandaliwa kuwa baba mwenye nyumba wa baadae wa klabu hiyo.
Lakini nje ya hilo Neymar anaonekana kuelekea kusaini mkataba mkubwa wa
chapa mpya ya vifaa (viatu) vya soka.
Neymar alionyesha kiatu chake kipya
cha Nike Hypervenom Phantom II ambacho ni maalumu kwa ajili yake, na
ambacho kimetengenezwa kwa ushirikiano na chapa ya mchezaji bora wa
zaamni wa NBA, Michael Jordan.
Neymar alipandisha katika mitandao ya
kijamii akiwa amelala kitandani kazungukwa na pea kadhaa za Nike chini
ya chapa ya Jordan huku akiwa ameshiikilia kiatu chake kipya chenye
wekundu na weupe.
Ilitangazwa kuwa Neymar atakuwa mchezaji
wa kwanza kwenye historia ya soka kuvaa viatu vya soka vyenye chapa
maalumu ya mchezaji bora wa mpira wa kikapu, Jordan’s zinazofahamika
kama ‘Jumpman’ zitakazokuwa kwenye viatu vyake.
Namba maarufu inayomuwakilisha Jordan
yaani 23 itakuwepo nyuma ya viatu vya mchezaji huyu katika mguu mmoja
pamoja na namba 10 ambayo inamuwakilisha Neymar akiwa timu ya Taifa
katika mguu mwingine.
Chapa za Nike na Jordan pia zimetoa toleo
maalumu la Neymar linalojulikana kama Jordan V Low ambalo ni kiatu
ambacho ndani yake kwenye ulimi wa iatu kutakuwa na jina la mchezaji
huyo wa Barcelona na Brazil.
Viatu vipya hivi vimewekwa sokoni kwa
manunuzi mwezi Oktoba tarehe 17 na bei yake ni kiasi cha £270 ambayo kwa
chenji za kitanzania ni zaidi ya laki saba na ishirini (Tzs 726982.65).
Neymar aliweka hili mtandaoni ikiwa ni
siku ambayo klabu yake ya Barcelona ilipotangaza kuwa itaingia naye
mkataba mkubwa siku ya Ijumaa.
Wachezaji kama Stephen Curry wamesifika
kwa kuhusika kupandisha chapa kama za UndeArmour kufika katika hatua
kubwa sana za kibiashara tofauti na ilivyokuwa mwanzo, hivyo Neymar naye
kutokana na ushawishi wake hii inaonekana kuwa njia yake mpya ya
kutengeneza fedha nyingi.
Chapa ya Jordan ni chapa maarufu zaidi
duniani kwa wavaaji wa viatu vinavyohusika na mchezo wa mpira wa kikapu
na ujio wake katika soka unaweza kumfanya akue zaidi kibiashara kwani ni
mwanamichezo anayeheshimika kotekote.
Si ajabu kuona Neymar kuwa mchezaji
aliyechaguliwa kuhusika kuwa sura ya chapa ya viatu vipya vya Jordan kwa
sababu ana ushawishi wa kibiashara.
Wakati klabu ya Barcelona ikijipanga
kuweka fedha nyingi kwenye akaunti yake, huku pia akiwa mchezaji
anayekaribia zaidi kutwaa tuzo kubwa duniani kwa wachezaji wa Umri wake
na kukiwa hakuna shaka kuwa ndiye baba ajae wa nyumba inayoitwa
Barcelona, Jordan hajakosea.
Neymar atakuwa zaidi ya hapa, jina lake
linauzika zaidi ya Griezman, Bale, Hazard, Pogba na wachezaji wengine
vijana waliopo. Huu ni ushindani mpya kwenye soko la biashara ya chapa
za viatu, na Jordan kaweka kwa binadamu anayejua soka, anayeijua fedha
inataka nini na anayejua namna biashara inavyotakiwa kuendeshwa. Neymar
ni nembo ya utajiri baada ya Ronaldo na anaweza kumzidi baadae.
Nicasius Nicholaus Agwanda (Coutinho Suso)
Tags
MICHEZO KIMATAIFA