Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akifungua
kongamano la vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini Oktoba 18,
2016 jijini Dar es salaam wakati wa wiki ya maadhimisho ya Umoja wa
Mataifa unaofikisha miaka 71 tangu kuasisiwa kwake. Maadhimisho ya hayo
yanaongozwa na kaulimbiu kwa upande wa Tanzania inayosema “Jukumu la
Vijana wa Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii”.
Mwakilishi wa Shirika Umoja wa
Mataifa nchini linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Annamaria Kiaga
akimkaribisha Mgeni Rasmi ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel kufungua
kongamano la vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini Oktoba 18,
2016 jijini Dar es salaam
Baadhi ya washiriki wa kongamano
la vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini wakimsikiliza Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole
Gabriel Oktoba 18, 2016 jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa
kongamano la vijana lililoandaliwa na Shirika Umoja wa Mataifa
linalishughulikia Maendeleo (UNDP).
Baadhi ya washiriki wa kongamano
la vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini wakimsikiliza Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole
Gabriel Oktoba 18, 2016 jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa
kongamano la vijana lililoandaliwa na Shirika Umoja wa Mataifa
linalishughulikia Maendeleo (UNDP).
…………………………………………………………………..
Na Eleuteri Mangi, WHUSM
Mataifa wanachama wa Umoja wa
Mataifa (UN) yanashiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii kuelekea
kilele cha maadhimisho ya miaka 71 ya umoja huo kinachofikia Oktoba 24
mwaka huu baada ya kuasisiwa kwake mwaka 1945.
Tanzania ambayo ni mwanachama hai
wa UN imeungana na umoja huo kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali
za kuunganisha nguvu za vijana na kuwajenga kimaadili, kiuchumi ili
waweze kujitambua na kujua mustakabali wao katika kujenga uchumi wa
nchi.
Kwa kuwa vijana ni nguzo kuu ya
kujenga taifa lolote duniani, Tanzania kwa kukushirikiana Umoja wa
Mataifa imeona umuhimu wa kuwashirikisha vijana kupitia kongamano la
vijana kutoka shule za sekondari na vyuo vikuu nchini lililofanyika
Oktoba 18 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu
Julius Nyerere (JNICC) uliopo jijini Dar es salaam.
Lengo la kongamano hilo ni
kuwashirikisha vijana kujadili namna watakavyoshiriki katika kutekeleza
Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kutafuta namna bora ya kutatua
changamoto zinazowakabili vijana nchini.
Vijana hao wamepata fursa ya
kukumbushana, kuelimishana na kubadilishana mawazo juu ya namna bora
inayowawezesha kutoa mchango wao katika masuala ya kiuchumi na maendeleo
ya kijamii nchini.
Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya
Maendeleo ya Viana ya mwaka 2007, ujana ni kundi mtambuka ambalo
linajumuisha vijana kuanzia miaka 15 hadi 35 ndio maana wanaitwa ni
nguvu kazi ya taifa kwa kuwa wengi wao kuanzia miaka 18, umri wa mtu
mwenye nguvu na uwezo mzuri wa kufikiri na kuchangia katika maendeleo ya
taifa kiuchumi na kijamii.
Akifungua kongamano hilo, Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole
Gabriel amewaasa vijana kuwa watakumbukwa kwa mchango wao watakaotoa
kwa jamii na si kwa nafasi zao kwa kuchangia uchumi na maendeleo ya
nchi, hivyo ni wajibu watambue umuhimu wao kwa taifa.
“Ikiwa kijana huna mchango katika
jamii, huna thamani yeyote, ni vema kujijengea uwezo wa kukumbukwa kwa
vitu ulivyofanya kwa taifa” alisema Prof. Ole Gabriel.
Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere, Prof. Ole Gabriel aliwaasa vijana kwa kusisitiza
“Baba wa Taifa aliwahi kusema, ni vema tujiulize, tumelifanyia nini
taifa na si taifa limenifania nini”
Kaulimbiu iliyoongoza kongamano
hilo inawataka vijana watambue nafasi yao katika kujenga uchumu wa nchi
“Jukumu la Vijana wa Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii”.
Kwa kuthamini nafasi ya kijana
katika taifa, Katibu Mkuu Profesa Ole Gabriel amewahimiza vijana nchini
kuwa na utamaduni wa kufanya kazi ili kuchangia uchumi wa taifa na
maendeleo ya jamii.
Profesa Ole Gabriel amewahimiza
vijana kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa kwa kushiriki
kufanya kazi zitakazowaletea maendeleo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa
(UN) neno “haki za binadamu” limetajwa mara saba katika Mkataba wa Umoja
wa Mataifa ambo ni ndio mwanzilishi na unafanya kazi ya kukuza na
kulinda haki za binadamu kwa kuzingatia kuwa huo ndio ufunguo huru wa
Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha Serikali zinawawajibika kwa haki za
binadamu.
Kwa miaka 15 iliyopita, Malengo
ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanaelezwa kufanikiwa katika masuala
mengi ambayo yalikuwa yakiathiri maisha ya watoto, vijana na familia
zao.
Mafanikio hayo yameonekana katika
kupunguza vifo vya mtoto, kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa kiume na
wa kike katika shule za awali, msingi na sekondari pamoja na vyuo
vikuu, kupunguza umaskini, upatikanaji wa maji salama na chakula bora.
Pamoja na mafanikio hayo, Umoja
wa Mataifa na wadau mbalimbali duniani umekuja na malengo mapya ya
Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyowekwa Septemba ya mwaka 2015 na viongozi
wa dunia ili kuleta mageuzi ya masuala mbalimbali kwa mustakabali wa
maendeleo ya binadamu hadi ifikapo mwaka 2030.
Katika kupanga malengo hayo, zaidi ya mamilioni ya watu walishiriki katika kuandaa ajenda mpya ya maendeleo endelevu.
Washiriki hao ni pamoja na
Serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, wasomi, mfumo wa Umoja wa
Mataifa na watu binafsi.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Annamaria Kiaga anasema kuwa
kila Oktoba 24, UN husherehekea kuanzishwa kwake ambapo huandamana na
shughuli mbalimbali kwa nchi wanachama pamoja na kukaa na wadau ili
kupata maoni yao yaweze kusaidia katika kuleta maendeleo.
Katika Malengo Endelevu 17
yaliyoainishwa na Umoja wa Mataifa, malengo matatu yanampa nafasi kijana
kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Lengo la 3 la SDGs linalenga
kuhakikisha vijana wanapata maisha yenye afya na kukuza ustawi wao
kifamilia kwa kuzingatia mazingira ya asili kwa ajili ya ukuaji na
ustawi ya wanafamilia wake wote hasa watoto, kwa kuwapa ulinzi na msaada
ili waweze kupata mahitaji yao kikamilifu ndani jamii yao.
Mshiriki wa kongamano hilo,
mwananfunzi Matilda Mashauri kutoka shule ya sekondari ya Gerezani
jijini Dar es Salaam anaiomba Serikali iungane na jamii kuwaelimishe
wazazi na walezi katika kusimamia ipasavyo haki na huduma kwa watoto ili
vijana waweze kufikia malengo yao na taifa kwa ujumla.
Mawazo hayo ya Matilda yanaendana
na lengo la nne (4) SDGs ambalo linalenga kuhakikisha umoja na usawa
katika utoaji wa elimu bora pamoja na kukuza fursa sawa ya kujifunza kwa
watoto wote ambapo inatarajiwa ifikapo 2030 wasichana na wavulana wote
wapate elimu ya msingi bure, kwa usawa na ubora wenye kuleta ufanisi
katika kujifunza.
Zaidi hayo, malengo ya maendeleo
endelevu yanahakikisha wanafunzi wote wanapata maarifa na stadi
zinazohitajika kukuza maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na haki za
binadamu, usawa wa kijinsia, kukuza utamaduni wa amani, kuthamini
utamaduni na mchango wa utamaduni.
Ili kujipambanua na mataifa
mengine Prof. Ole Gabriel anasema kuwa changamoto inayowakabili vijana
wengi nchini Tanzania ni fikra ya namna ya kujiletea maendeleo kwa
kutumia utamaduni chanya wa kufikiri kwa kutumia rasilimali zilizopo na
anawatahadharisha juu ya uvamizi wa teknolojia ambayo isipotumika vizuri
itabomoa vijana ambao ni tegemeo la taifa.
“Nchi yoyote duniani isiyokuwa na
maadili imeparanganyika, tusipokuwa na utamaduni mzuri taifa letu
halitakuwa salama” alisema Prof. Ole Gabriel.
Katika kuhakikisha utamaduni wa
Mtanzania unadumishwa Prof. Ole Gabriel anasema kuwa ni vema teknolojia
itumike vizuri ili kuwaletea vijana na taifa maendeleo endelevu ili
kuendana na Sera ya Taifa ya Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025.
Naye Mjasiriamali kijana Abdul
Faraji mzaliwa wa mkoani Tanga amemweleza Mgeni Rasmi Prof. Ole Gabriel
kuwa licha ya yeye kuwa na makazi yake jijini Dar es salaam, ameamua
kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana wa ukanda wa bahari waishio
mkoani Tanga kwa kuanzisha kituo kijulikanancho kama Vijana House ili
kurasimisha kazi zao za kiuchumi ziwe zenye tija kwa maendeleo yao.
Mawazo ya kijana Abdul Faraji
yamekuwa ni njia ya kulelekea kutekeleza lengo la tano (5) la SDGs
katika kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana
kutambua asili, hadhi na haki sawa ya wanafamilia wote kwa msingi wa
uhuru, haki na amani duniani ambapo taasisi yake itafanya kazi na vijana
wote bila kujali jinsia zao.
Akizindua Malengo ya 17 ya
Maendeleo Endelevu (SDGs) Septemba 29, mwaka 2015 jijini Dar es Salaam,
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania ambaye
pia ni Mwakilishi Mkazi wa UNDP Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa kwa
mara ya kwanza katika historia ya dunia, serikali zimekutana na
kukubaliana kupeana malengo kwa ajili ya kila mtu.
“Malengo haya yatasaidia mataifa
yote kushirikiana katika kuwezesha ustawi, kupunguza matumizi na
kuilinda dunia dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Katika hilo
watashughulikia viashiria vinavyohusu maendeleo endelevu; ukuaji wa
uchumi, ustawi wa jamii na kulinda mazingira.” Amesistiza Bw. Alvaro.
Malengo hayo 17 ya SDGs ni pamoja
na kuondoa umasikini, kumaliza tatizo la njaa duniani, afya njema na
ustawi miongoni mwa jamii, utoaji elimu bora, kuwepo na usawa wa
kijinsia, upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira pamoja na
uhakika wa kuwa na nishati nafuu na salama.
Mengine ni watu wapate kazi nzuri
yenye kukuza uchumi, kukuza viwanda, kuwepo ubunifu katika sekta
mbalimbali, na kuboresha miundombinu, kupunguza ukosefu wa usawa,
kuendeleza miji na jamii, kuimarika uwajibikaji, utumiaji na uzalishaji,
utunzaji wa hali ya hewa, utunzaji wa maisha ya viumbe hai chini maji
na maisha juu ya ardhi, kuwepo amani na kuwa taasisi imara za kusimamia
haki pamoja na uwepo wa ushirikiano kwenye malengo thabiti miongoni mwa
mataifa.
Tags
HARUSI & SHEREHE